VIDEO: Polisi mstaafu aliyejichimbia kaburi ajinunulia jeneza

Askari mstaafu wa Jeshi la Polisi, Patrick Kimaro (wa kwanza kushoto) akiwaongoza kuingiza jeneza lake ndani ya nyumba yake jana Jumatatu Machi 4, 2024. Picha na Ombeni Daniel

Hai. Askari mstaafu wa Jeshi la Polisi, Patrick Kimaro maarufu kwa jina la Sabasita ameweka historia nyingine katika maisha yake, baada ya kukamilisha kutengeneza jeneza litakalotumika kumuhifadhi siku atakapofariki dunia.

Jeneza hilo lililogharimu Sh3 milioni, tayari liko nyumbani kwake na amelihifadhi katika chumba maalumu, litakapokaa hadi siku atakayofariki dunia.

Kupelekwa nyumbani kwa jeneza hilo lililotengenezwa Barabara ya Kibosho Wilaya ya Moshi, kuliibua mshangao kwa baadhi ya wananchi wanaoishi vijiji jirani, huku wengi wakijiuliza nani kafariki dunia eneo hilo.

 Jeneza hilo lililobebwa kwenye gari maalumu la kubeba maiti, wakati likipita viunga vya vijiji jirani baadhi ya wananchi walipata mshangao kwa kuwa hawakuwa na taarifa za msiba huku baadhi yao wakilisogelea.

Hata lilipofikishwa nyumbani kwa Sabasita, baadhi ya wananchi walisogea karibu kulishuhudia na ndipo walipobaini halina mwili.

Sabasita tayari ameshachimba kaburi lake ambalo amelijenga na ameendelea kuliboresha na mpaka sasa limegharimu Sh10 milioni baada ya kubadilisha mfuniko wa zege na kuweka msalaba mkubwa wenye taa ndani.

Polisi mstaafu aliyejichimbia kaburi anunua jeneza

Nyumbani kwake kulivyo

Nyumbani kwa Sabasita ukiingia, kabla ya kukuta geti kushoto unakutana na nyumba ambayo ndani ndipo kipo chumba maalumu alichohifadhi jeneza lake na baada ya mita chache ndipo unakutana na geti la kuingia katika nyumba yake kubwa.

Ukiingia tu, upande wa kulia utaona kaburi lake alilolijenga mwaka mmoja na nusu uliopita.

Pia, ukiingia katika chumba hicho ambacho amehifadhi jeneza, juu ya jeneza hilo ameweka mashada ya maua, ukutani ameweka picha zake tatu za muonekano tofauti, redio ambayo wakati huo ilikuwa ikiimba nyimbo za dini na ukutani ameandika “Yesu nitie nguvu nimalize mwendo salama.”

Akizungumza na waandishi wa habari waliofika nyumbani kwake, Sabasita alisema yuko kwenye maandalizi ya mwisho ya kukamilisha wosia kisha kuundaa historia yake itakayosomwa baada ya yeye kufariki dunia.

Sabasita aliyestaafu kazi ya polisi Februari 2023, baada ya kuitumikia kwa miaka 36, alisema kazi kubwa ilikuwa ni kukamilisha kaburi na jeneza na sasa kilichobaki ni kukamilisha wosia na kuandika historia yake ili kuondoa usumbufu kwa watoto na ndugu zake, siku ambayo Mungu ataamua kuvuna mavuno yake.

“Familia yangu ilipoona kaburi ilishtuka, wakakimbia halafu wakarudi wakalizoea na niliposema habari ya jeneza waliona siwezi kulileta nyumbani sasa nimelileta na nimeliweka katika chumba maalumu naamini nalo wataliona na kulizoea,” alisema Sabasita.

Askari mstaafu wa Jeshi la Polisi, Patrick Kimaro akionyesha kaburi alilojitengezea. Picha na Ombeni Daniel.

Alisema chumba hicho ni maalumu kwa ajili ya jeneza na kitafunguliwa na mtu maalumu kwa wakati maalumu na kwa sababu maalumu.

“Kama mnavyoona kumetangulizwa na maneno mazuri yameandikwa Yesu nitie nguvu nimalize mwendo salama, kwa sababu hii bado ni safari mimi ninahema bado ni binadamu nahitaji maisha,” alisema Sabasita.

Akizungumzia wosia na historia yake aliyoanza kuiandaa, Sabasita alisema itasomwa baada ya kifo chake na anafanya hivyo kwa kuwa yeye ndiye anafahamu alikopita na alichofanya katika maisha yake ya hapa duniani.

“Sasa nimefunga ukurasa wa kaburi na jeneza langu, kinachofuata ni kukamilisha wosia nilioutayarisha, imebaki vitu vichache ni wa tofauti kidogo maana ninashirikisha watoto wangu waupitie na baada ya hapo wakiridhika nao, nitampa kila mmoja nakala yake,” alisema Sabasita.

“Nategemea kuandika historia yangu, historia ile ile ambayo marehemu anasomewa baada ya kufa, mimi nitataka ionekane kwenye chumba hiki nilichohifadhi jeneza.

“Mimi ndiye ninafahamu baada ya kuzaliwa nilifanya nini nilitoka hapa kwenda wapi, nilisoma shule gani na baada ya hapo nilienda wapi na nilifanya nini mpaka nilikofikia sasa,” alisema Sabasita.

“Pengine wakitengeneza historia wakati mimi nimezimika wanaweza wakasema uongo, lakini mimi nitatengeneza mwenyewe maana nafahamu nilikopita, nitaandaa historia yangu na kuacha sehemu ndogondogo ambazo kimsingi watakaokuwa hai watajaza kwa mfano tarehe ya kufa.”

Alisema ameamua kuwashirikisha watoto wake katika wosia huo ili kuondoa minong’ono, kwa kuwa watu wanaweza kujitokeza na hata ndugu kuleta shida baada ya yeye kufariki dunia.

Pia, Sabasita anaeleza kuwa, aliguswa kufanya maandalizi yake ili kupunguza adha na usumbufu kwa watoto wake baada ya yeye kufariki na kwamba asingependa wapitie yale ambayo yeye alipitia wakati wazazi wake wanafariki dunia mwaka 1995.

“Nilitaka kufanya hivi kwa sababu ya kupunguza adha ambayo niliiona wakati namzika baba yangu na mama yangu mwaka 1995, nikiwa mtoto wa kwanza nyumbani nilipata shida sana na maziko yale yalinifanya nisononeke, kwani vitu vya kuzikia viliazimwa kwa watu ikiwamo mbao na hata uchimbaji kaburi ulisumbua kuanza kutafuta watu,” alisema Sabasita.


Mtaalamu wa saikolojia

Akizungumzia kujitengenezea jeneza, Msaikolojia Dk Isack Lema alisema hakuna sababu za moja kwa moja za kisaikolojia kwa kuwa ni uamuzi wa mtu kujiandaa na mara nyingi suala hilo linatokana na utamaduni.

“Mara nyingi hivyo vitu vinaendana na culture (utamaduni), hivyo moja kwa moja kisaikolojia hatuwezi kusema chochote, kwa sababu amejiandaa, lakini mara nyingi watu katika hali ya kawaida wanakimbia kifo, ukiona anakifuata inawezekana amejiandaa juu ya hicho kifo,” alisema.


Fundi jeneza afunguka

Michael Kweka ambaye ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Mr Coffin ambako Sabasita ametengeneza jeneza hilo, alisema jeneza hilo ni daraja A na linaweza kukaa hata miaka 50 bila kupata shida.

“Jeneza hili tumelitengeneza kwa kutumia mbao ya mbunduki, ni mbao ngumu ambayo haishambuliwi na wadudu, haipindi ni mbao ambayo inaweza kukaa hata miaka 50.

“Ni jeneza la daraja A, kwa sababu mbao tuliyotumia ni bora kuanzia chini mpaka juu, tumeweka kioo na tumetumia miezi sita kulikamilisha kwa sababu ya kazi ya kuunganisha mbao kuliunda na hata umaliziaji, ili baadaye lisilete shida.

“Jeneza hili ndilo la kwanza kutengeneza katika ubora huu katika ofisi hii, ubora wake ni mkubwa na gharama zake ni kubwa, limegharimu Sh3 milioni kutokana na vifaa vilivyotumika na uimara wake,” alisema.


Sabasita ni nani

Patrick Kimaro maarufu kwa jina la Sabasita, ambaye alizaliwa Februari 2, 1963, aliajiriwa Jeshi la Polisi mwaka 1987 na amefanya kazi kwa miaka 36.

Amepitia vyeo mbalimbali na mpaka anastaafu Februari mwaka jana, alikuwa Superintendent of Police (SP).