Vita mpya Waziri Silaa, wenyeviti wa mitaa

Waziri wa Ardhi nyumba na maendeleo ya Majazi, Jerry Silaa (kushoto) akikagua ramani wakati alipokagua ujenzi wa kituo cha mafuta kata ya Mawrnzi Manispaa ya Moshi. Picha na Florah Temba

Dar/mikoani. Agizo la Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, kupiga marufuku wenyeviti wa serikali za mitaa na vijiji kujihusisha na uuzaji wa ardhi (viwanja na mashamba), limepingwa na wenyeviti hao na wanasheria, wakieleza utekelezaji wake utaongeza migogoro.

Akizungumza juzi katika kikao na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Jerry Silaa alisema kazi hiyo itafanywa na maofisa ardhi wa wilaya.

Alikuwa akizungumzia siku 100 katika wizara hiyo, tangu ateuliwe kushika wadhifa huo Agosti 30 na kuapishwa Septemba Mosi, mwaka huu.

Mbali ya kutoa agizo hilo, Silaa alitaka wananchi wasikubali kutoa asilimia 10 kuwapa viongozi hao wanapofanya mauziano ya ardhi.


Walichosema wenyeviti

Mwenyekiti wa Kijiji cha Munge, wilayani Siha Mkoa wa Kilimanjaro, Isack Mollel alisema hatua hiyo si sawa na endapo Serikali haitakuwa makini, hilo litachangia kwa kasi ongezeko la migogoro ya ardhi.

"Tunafahamu ardhi iko chini ya Serikali za Mitaa na si vijiji, maana yake ni kwamba wenyeviti wa vijiji ndio wasimamizi wa ardhi hizo na ndio wanawafahamu wamiliki wake, sasa leo wakiondolewa kushiriki kwenye uuzaji wa ardhi, nani ambaye atasimamia, ambaye anafahamu kwa usahihi maeneo hayo?” alihoji Mollel na kuongeza:

"Katika hili Serikali iwe makini, maana tukisema wasimamie viongozi wa ardhi kutoka halmashauri na watendaji wa mitaa au vijiji, wale wote ni wageni wa maeneo hayo, hivyo wauzaji ardhi wanaweza kuwadanganya kwa masilahi yao binafsi na kuchochea ongezeko la migogoro ya ardhi, hususan vijijini ambako changamoto ni kubwa."

Mwenyekiti wa Mtaa wa Matindigani, Manispaa ya Moshi, Amos Chibago, alisema wenyeviti wa vijiji na mitaa ni wenyeji wa maeneo husika, hivyo kutowashirikisha kwenye uuzaji wa ardhi kutaibua utapeli na kuongeza migogoro ya ardhi.

Alishauri Serikali ije na utaratibu wa kuboresha zaidi na si kuwaondoa kushiriki.

Alisema: "Katika kumaliza tatizo la migogoro ya ardhi, Serikali inapaswa kuja na mfumo shirikishi, kwa maana ya kwamba mtu akitaka kuuza eneo lake, mbali na mwenyekiti wa kijiji kushiriki, watendaji na maofisa ardhi nao washirikishwe ili kuhakiki wote kwa pamoja."

Mwenyekiti wa Mtaa wa Tunduma, Mussa Mwambogolo alisema uamuzi huo unaenda kuongeza tatizo kwenye jamii, kwa kuwa wao ndio wanafahamu maeneo kwa historia.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mtaa wa Mlalakuwa, uliopo Mwenge jijini Dar es Salaam, Suleiman Masare, alisema msimamo wa waziri uko sahihi, kwani ni kweli wenyeviti wa Serikali za Mitaa hawana dhamana ya kuuza ardhi, bali walikuwa wasimamizi tu.

“Viongozi wa Serikali za Mitaa ndio wana wajibu na migogoro yote ya mtaa, ardhi ipo kwenye mtaa, kwa nini mwenyekiti asijihusishe, hii si sawa, wakisema ni kwa sababu anauza ardhi wenyeviti hawawezi kuuza ardhi,” alisema.

Kisaga Mbalu, mwenyekiti wa serikali ya mtaa wa Kileleni, katani Vibaoni wilayani Handeni alisema marufuku hiyo inaonyesha kushindwa kuwajibika, akishauri wenyeviti wenye matatizo ndio washughulikiwe.

“Kuna baadhi ya wenyeviti wanahusika na migogoro ya ardhi na wengine hawahusiki, kwa hivi walivyotamka bado migogoro itaongezeka zaidi si vijijini tu hata mijini; watu watauziana kwa ushahidi wa majirani, watu wanatapeliwa,” alisema.


Wabunge, wanasheria

Mbunge wa Kigamboni, Dk Faustine Ndugulile alisema masuala ya mauzo ya ardhi isiyopimwa bado ni changamoto.

Dk Ndugulile alisema mauzo ya ardhi kusimamiwa ngazi ya wilaya si kila kijiji au kitongoji kipo karibu na makao makuu ya wilaya na si kila wilaya ina maofisa mipango miji na ardhi.

“Tuangalie jinsi ya kuimarisha mifumo iliyopo na kuongeza wigo wa uwajibikaji kwa wale tutakaowapatia majukumu ya kusimamia,” alisema na kuongeza:

“Tutumie teknolojia kutambua ardhi yote nchini, anayemiliki, au kusimamia ardhi anapofanya uhamishaji wa umiliki kwenda kwa mtu mwingine kupitia mfumo anaonekana.”

Rais wa zamani wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), John Seka alisema changamoto iliyopo ni viongozi wa vijiji na mitaa kujitwika majukumu ya kuthibitisha mauzo ya ardhi na kuchukua asilimia ya mapato kama sehemu ya biashara iliyofanyika.

“Hiyo fedha wanayochukua yenyewe inaleta changamoto, wanaposhiriki kwenye mchakato wa mauzo kunapokuwa na migogoro baadaye inaonekana Serikali imehusika kwenye mgogoro huo,” alisema.

Wakili Seka alisema wenyeviti wabaki kwenye utatuzi wa migogoro ya ardhi, wasiwe sehemu yake.

“Kama watu wanaingia mauziano waende kwa watu wanaohusika kuthibitisha mikataba,” alisema.

Wakili Seka alisema viongozi hao wa mitaa na vijiji wamekuwa wakiandaa mikataba ya mauziano kama Serikali ndiyo inauza ardhi, jambo ambalo si sahihi kwa mamlaka kuandaa mikataba hiyo.

Kwa upande wake, wakili Paul Kisabo alisema hata kama maofisa ardhi watahusika lazima wataenda kwa wenyeviti wa Serikali za Mitaa kwa sababu wao ndio wanaishi huko.

“Nafikiri labda hawatapata nafasi ya kugonga mihuri, majina yao hayataonekana lakini huwezi kuwaondoa kabisa kwenye ununuzi wa ardhi, kinyume cha hapo utauziwa mbuzi kwenye gunia,” alisema.


Alichosema Silaa

Waziri Silaa juzi aliwataka wananchi wasikubali kulipa asilimia 10 ya fedha ya ununuzi wa viwanja na mashamba kwa viongozi wa mtaa au vijiji, akisema ardhi ya kijiji haiuzwi.

“Ili kuwa kwenye mipango miji wananchi epukeni kununua ardhi kwa wenyeviti wa kijiji na ikitokea unataka kununua basi hakikisha unaitishwa mkutano wa kijiji na taratibu zote zinafuatwa, watakueleza masharti yao ikiwezekana chukua video ya huo mkutano siku mambo yakiharibika tuthibitishe,” alisema Silaa.


Mtazamo tofauti Dar

Mwenyekiti wa wenyeviti wa Serikali za Mitaa Mkoa wa Dar es Salaam, Juma Mwingamno, alisema jambo hilo wamelipokea na watalitekeleza kwa kuwa waziri ndiye mwenye dhamana na ardhi.

Hata hivyo, alisema wana mpango kuanzia wiki ijayo kwenda halmashauri kwa maofisa ardhi kupata mwongozo wa kipengele ambacho mwenyekiti anatakiwa atie saini kwenye fomu baada ya watu kuuziana ardhi.

Alisema kuna haja ya kuondolewa ili wasije wakajikuta baadaye wanaingia kwenye hatia kwa kushiriki jambo ambalo limekatazwa.

“Waziri ndiye kiongozi mwenye dhamana, hawapaswi kupingwa, lakini swali ni je, kutaleta tija au la! Kwa kuwa ninachojua mwenyekiti wa serikali ya mtaa ni shuhuda muhimu kuhakikisha kama mtu anayenunua eneo hilo ni la muuzaji halali,” alisema na kuongeza:

“Lakini pia mwanasheria anapaswa kuhusika katika hili, je, anajua eneo vizuri, ikiwemo mipaka au hata huyo ofisa ardhi? Hili linaenda kuleta shida kwa nyumba za kurithi, ndugu mmoja kuuza bila wengine kuwa na taarifa, lakini pia kuna watu ambao wamekuwa wakiongeza mipaka kwenye viwanja vya wenzao.”

Alihoji: “Mgogoro utakaotokea hapo je, maofisa ardhi wenyewe wataweza kuutatua bila uthibitisho wa wenyeviti?”

Alishauri kosa linapofanyika aadhibiwe aliyekosa na si kuweka watu wote kwenye kapu moja.


Ardhi mfupa mgumu

Hata kabla ya Silaa kuteuliwa kuongoza wizara hiyo, migogoro ya ardhi nchini imekuwa mfupa mgumu.

Mei 25 aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk Angelina Mabula, alitaja mambo matatu kuwa ndiyo chanzo cha matatizo ya migogoro ya ardhi.

Mambo hayo ni watumishi wanaojitolea, ulipaji wa fidia na umilikishaji ardhi kwa watu zaidi ya mmoja ambapo mikoa iliyoathirika zaidi ni Dar es Salaam na Dodoma.

Aliyasema hayo wakati akiwasilisha hotuba ya makadirio ya bajeti 2023/24 bungeni jijini Dodoma.

Waziri Mabula alisema matatizo hayo hukolezwa zaidi na watumishi wanaofanya kazi za kujitolea bila kuwa na mishahara, lakini maeneo mengine wanakabidhiwa mifumo, licha ya kuwa hawana hata mikataba ya utumishi.

Alitolea mfano wa Jiji la Dodoma alipokwenda kuwatimua watumishi 126 waliokutwa wanafanya kazi bila kuwa hata na mikataba, lakini wanaendesha maisha yao vizuri huku wakiijua mifumo kama waajiriwa wengine.

“Watumishi wengi wanafanya kazi za kujitolea, hawana mikataba lakini wanaendesha maisha yao vizuri tu, Dodoma peke yake tuliwakuta 126 lakini tulipowahoji ilionekana wapo kwenye mfumo,” alisema Dk Mabula.

Imeandikwa na Baraka Loshilaa na Nasra Abdallah (Dar), Flora Temba (Moshi), Habel Chidawali na Rachel Chibwete (Dodoma).