Vuguvugu Katiba Mpya latikisa mtandao wa Twitter

Vuguvugu Katiba Mpya latikisa mtandao wa Twitter

Muktasari:

  • Watu wa kada mbalimbali nchini Tanzania ni kama wameanzisha vuguvugu la kudai Katiba Mpya kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter kwa lengo la kuishinikiza Serikali kuendelea na mchakato huo.



Dar es Salaam. Watu wa kada mbalimbali nchini Tanzania ni kama wameanzisha vuguvugu la kudai Katiba Mpya kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter kwa lengo la kuishinikiza Serikali kuendelea na mchakato huo.

Kupitia vuguvugu hilo lililopewa jina la “KatibaMpyaMovement”, wananchi wamekuwa wakitoa maoni yao tofauti kueleza umuhimu wa kuwa na katiba mpya hapa nchini na wameitaka Serikali kurejea mchakato huo.

Katiba Mpya ni moja ya ajenda za vyama mbalimbali vya siasa nchini kikiwemo Chadema na CUF ambavyo vimekuwa vikipigania mabadiliko hayo kuwa pamoja na kuwa rais atapunguziwa madaraka, haki itatendeka katika chaguzi.

Hata hivyo, Rais Samia Suluhu Hassan katika moja ya hotuba zake baada ya kuwaapisha aliowateua alitaja neno katiba kisha akasema “sijui nina maradhi gani na katiba, suala la katiba mpya lisubiri.”

 Gervas Sulle ameandika katika ukurasa wake,”katika Tanzania tulihitaji katiba kwa nyakati mbalimbali kwa kuwa ni muhimu. Kwa sasa katiba mpya ya wananchi ni lazima na sio ombi kwa maendeleo ya Taifa letu.

Anayekataa Katiba Mpya anataka tubaki na mtazamo wa maendeleo wa 1977. Ni CCM tu wanahofu kwa maslahi yao ya kisiasa.”

Mwananchi mwingine, Kumbusho Dawson amenukuu maneno katika kitabu cha Hayati Benjamin Mkapa cha My Life, My Purpose akiandika, “Iundwe tume huru ya uchaguzi itakayokubalika na vyama vyote vya siasa ndio chachu hasa ya kulea na kukuza demokrasia nchini.”

Dk Chris Cyrilo amesema, “hakuna Katiba Mpya kwa njia ya amani. Hakuna CCM wapo radhi kwa chochote wabaki na katiba hii inayolinda maslahi yao ya kiutawala na kiuchumi. Natamani tunaotaka katiba mpya tuliweke hili akilini.”

Ntele Benjamin amesema, “wasomi wa vyuo vikuu wana wajibu mkubwa wa kuamsha umma kudai katiba mpya. Katiba mpya sio matakwa ya Serikali ni matakwa ya wananchi. Ni wakati sasa vyuo vikuu kutoka walipojifungia na kupaza sauti Kuhusu Katiba mpya.”