Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wabainisha sababu za wafungwa waliosamehewa kurejea uhalifu

Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) Simon Sirro

Muktasari:

Wameeleza kuwa katika hali ya kawaida ni vigumu kubainisha moja kwa moja sababu za wafungwa hao kurudia makosa yaliyowafanya watupwe gerezani ingawa wakati mwingine yanaweza kuchangiwa na wenyewe, magereza waliyokuwamo na jamii inayowazunguka uraiani.

Dar es Salaam. Wataalamu wa masuala ya ustawi wa jamii na urekebishaji wafungwa wameelezea mazingira yanayoweza kusababisha wafungwa waliopata msamaha wa Rais lakini baadaye wakarudia matukio ya uhalifu na kusema kuna mengi yapo nyuma yao.

Wameeleza kuwa katika hali ya kawaida ni vigumu kubainisha moja kwa moja sababu za wafungwa hao kurudia makosa yaliyowafanya watupwe gerezani ingawa wakati mwingine yanaweza kuchangiwa na wenyewe, magereza waliyokuwamo na jamii inayowazunguka uraiani.

Wataalamu hao wameeleza hayo baada ya kutakiwa kutoa maoni yao baada ya juzi, Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) Simon Sirro kusema kuwa wafungwa watano ambao ni miongoni mwa waliopata msamaha wa Rais Aprili 26, waliuawa na wananchi kutokana na kile kilichoelezwa kuwa ni kujiingiza tena kwenye matukio ya kihalifu.

Kwa maana hiyo, aliwaonya wale wanaofaidika na msamaha wa Rais kutoitumia vibaya fursa hiyo akisisitiza kuwa Jeshi la Polisi liko tayari ‘kuwashughulikia’.

Katika mahojiano ya gazeti hili, mhadhiri wa Chuo cha Ustawi wa Jamii, Salma Fundi ambaye amewahi kufanya kazi katika magereza akiwa mtoa huduma za urekebishaji wahalifu, alisema mtu aliyefungwa anaweza kujikuta akirudia tena kwenye matukio ya kihalifu kutokana na kusukumwa na mambo mengi.

Alisema ingawa kwenye magereza mengi kumekuwa na programu zinazoendeshwa kwa ajili ya kuwanufaisha wafungwa hao, wakati mwingine haziendani na uhalisia wa maisha yaliyoko uraiani.

“Magerezani kunafanyika mambo mengi ya kuwawezesha wafungwa ikiwamo kuwapa ujuzi kama vile ufundi seremala, lakini unakuta mtu aliyefundishwa kazi hiyo anapoachiwa kutoka gerezani kile alichojifunza kule hawezi kuendelea nacho uraiani kutokana na mazingira kutokuwa rafiki kwake...,” alisema.

Alisema baadhi ya magereza yanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa rasilimali kuwezesha programu zinazotolewa kwa wafungwa kuwa na manufaa, hivyo nyingi zinakuwa jumuishi bila kuzingatia mahitaji halisi ya wafungwa.

“Mtu anapelekwa gerezani ina maana kwamba amekuwa na tabia zisizokubalika sehemu husika au amekwenda kinyume na sheria za nchi, hivyo kupelekwa kule ni kwenda kumrekebisha ili akirudi uraiani awe raia mwema. Lakini wakati mwingine huduma za urekebishaji tabia zinazotolewa gerezani zinakabiliwa na changamoto ndiyo maana unaweza kukuta baadhi ya wafungwa wanarudia makosa yao wanaporudi uraiani,” alisema.

Lakini kwa upande mwingine, alisisitiza kuwa jamii wakati mwingine ndiyo inayopaswa kulaumiwa kwa kuwa na mtazamo hasi juu ya wafungwa wanaopewa misamaha kurejea uraiani.

“Jamii nayo inapaswa kubadilika maana unaweza kukuta mtu alifungwa na baadaye akapata msamaha lakini akirudi uraiani jamii hiyo inaendelea kumtenga na kuwa na hofu juu yake. Hili jambo lipo sana, watu hawajui pengine kwa mtu kukaa gerezani kumemfanya abadilike na kuwa mwema. Hawataki kumpa ushirikiano na wanaweza kumzushia jambo lolote na hata kumwua,” alisema.

Ofisa katika Gereza la Isanga lililopo Dodoma, Rashidi Twaha alisema wafungwa wanaopata msamaha wamegawika katika makundi mawili; wale wanaotoka kwa msamaha wa Rais na wale wanaopewa msamaha kupitia kamati ya Parole.

“Mara nyingi gereza tunaletewa waraka kutoka Ikulu unaosema wafungwa wa makosa ya aina haya, waliotumikia kifungu cha muda fulani au wafungwa wenye sifa hizi watatolewa kwa msamaha wa Rais. Na wale wanaotoka kwa msamaha wa Parole huwa kunakuwa na mchakato unaoanzia gerezani, mtaani kwa mfungwa unakwenda hadi ngazi ya wilaya, mkoa na taifa kisha inapothibitika kwamba mfungwa ameonyesha mwenendo mzuri anasamehewa,” alisema.