Waendesha baiskeli 200 waanza rasmi safari Twende Butiama 2025

Dar es Salaam. Waendesha baiskeli zaidi ya 200 wameianza rasmi safari ya zaidi ya kilomita 1,500 utakaopita katika mikoa 11 kutoka jijini Dar es Salaam hadi mji wa Butiama.
Msafara huo umeanza safari hiyo juzi, ikiwa ni sehemu ya kumbukumbu ya Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere, ambaye urithi wake wa fikra na maono unaendelea kuiongoza Tanzania.
Washiriki walikusanyika nyumbani kwa Mwalimu Nyerere ili kupata baraka kutoka kwa mjane wake, Mama Maria Nyerere, ikiwa ni ishara ya kuaga kwa heshima kabla ya kuanza safari.
Akizungumza wakati wa tukio hilo, Agapinus Tax, Mkurugenzi wa Viatarishi na Uzingatiaji wa Sheria kutoka Vodacom Tanzania, alieleza msafara wa mwaka huu utapita katika mikoa 11 na utahusisha waendesha baiskeli wa kimataifa kutoka Kenya, Uganda, Burundi, DRC, Zambia na Malawi.
“Zaidi ya waendesha baiskeli 200 watashiriki safari hii kutoka Dar es Salaam hadi Butiama. Kati yao, 50 watarudia njiani huku 150 wakitarajiwa kufika hadi mwisho wa safari,” alisema Tax.
Msafara wa mwaka huu umekusanya washiriki kutoka kila kona ya Tanzania ikiwemo Arusha, Kilimanjaro, Tanga, Lindi, Mbeya, Kagera, Dodoma, Pwani na Tabora, pamoja na wale wa kimataifa kutoka Kenya, Uganda, Burundi, Botswana, DRC, Zambia, Malawi, Afrika Kusini, Marekani, Uholanzi na Nigeria.
Katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, msafara wa Twende Butiama umetoa mafanikio makubwa ikiwemo kupanda miti zaidi ya 100,000, kufikia watu 23,000 kupitia huduma za afya kwa njia ya kliniki tembezi, kugawa madawati 1,900 kwa shule 32 za umma na kutoa baiskeli 50 kwa wanafunzi waishio mbali na shule.
Mwaka huu, waandaaji wanalenga kufikia shule 10 zaidi, kupanda miti 50,000 na kuwafikia Watanzania zaidi ya 700,000 wakiwemo watoto, vijana na wazee.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa wakati wa kuzindua safari hiyo, alisema msafara huu si tu kwa ajili ya kumuenzi Mwalimu Nyerere, bali pia ni chombo muhimu cha kuhamasisha afya na maendeleo ya jamii.
Mwanzilishi mwenza wa msafara huo, Gabriel Landa, alisema safari hiyo itaambatana na shughuli mbalimbali za kijamii zenye kugusa maisha ya wananchi, zikiongozwa na maono ya Mwalimu ya kupambana na ujinga, maradhi na umasikini.
“Waendesha baiskeli watashiriki katika shughuli za utunzaji wa mazingira ikiwemo upandaji miti kwenye maeneo ya Mlima Kilimanjaro na chanzo cha Mto Pangani ili kusaidia kuhifadhi mazingira,” alibainisha.
Kwa upande wa Wilmot Ishengoma, Mkuu wa Idara ya Hatari kutoka Benki ya Stanbic Tanzania, alisisitiza mchango wa msafara huo katika kuhamasisha maisha yenye afya na ushiriki wa jamii:
“Msafara huu unaendelea kuhamasisha jamii, hasa katika kuhimiza mazoezi na afya njema,” alisema.