Wajanja waanza kujineemesha stendi mpya ya Mwenge

Mwonekano wa stendi mpya ya Mwenge. Picha na Nasra Abdallah

Muktasari:

  • Stendi ilianza kujengwa mwaka 2020, imegharimu Sh10 bilioni zitokanazo na mapato ya ndani ya Manispaa ya Kinondoni.

Dar es Salaam. Wakati Manispaa ya Kinondoni ikisubiri wafanyabiashara wafungue biashara zao katika maduka yaliyopo stendi ya Mwenge na kuizindua rasmi, baadhi ya wafanyabiashara wamedaiwa kuendelea kuyapangisha mara ya pili maduka hayo.

 Hivi karibuni Ofisa Biashara wa Manispaa ya Kinondoni, Shedrak Mbonike, aliimbia Mwananchi Digital kuwa stendi hiyo ingefunguliwa kabla ya kumalizika kwa Januari 2024.

Stendi hiyo iliyoanza kujengwa mwaka 2020, imegharimu Sh10 bilioni zitokanazo na mapato ya ndani ya Manispaa ya Kinondoni na inatarajiwa kuzalisha Sh1.5 bilioni kwa mwezi.

Akieleza sababu ya kuchelewa kufunguliwa kwa stendi hiyo leo Februari 5, 2024, Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, Hanifa Hamza amesema wanawasubiri wafanyabaishara waliokodi majengo wamalize kupanga bidhaa zao ndipo waizindue rasmi.

Hata hivyo, uchunguzi uliofanywa na Mwananchi hivi karibuni umebaini huenda hilo likachukua muda kufanyika kutokana na baadhi ya waliopata maduka hayo sasa kuanza kusaka wateja wa kuwapangisha kwa bei za juu zaidi.

Kwa mujibu wa Manispaa ya Kinondoni, yapo maduka  yanayopangishwa kuanzia Sh299,000 hadi Sh4 milioni kwa mwezi, mtu hutakiwa kulipa kwa miezi 10 na kueleza kuwa tayari yote yameshachukuliwa.

Hata hivyo, Mwananchi limepata taarifa kuwa baadhi ya wafanyabiashara wamepangisha maduka hayo kwa kati ya Sh600,000 hadi Sh700, 000 mwa mwezi, huku maduka ya Sh4 milioni yakipangishwa kwa Sh6 milioni kwa mwezi.

“Pamoja na bei hiyo kubwa, bado kuna watu wanachukua kwa kuwa wanajua Mwenge kuna uhakika wa biashara endapo stendi itaanza kufanya kazi bila kujua kwamba wanapigwa kwa kuwa hiyo sio bei halisi,” amesema mmoja wa wafanyabiashara ambaye hakutaka jina lake litajwe.

Licha ya Manispaa hiyo kusema maduka yote yameshachukuliwa, pia Mwananchi imeshuhudia baadhi ya madalali wakiwa wanawazungusha watu wenye uhitaji kuangalia ambao walisikika wakimwambia mmoja wa wateja kuwa mpaka sasa zimebaki mbili za Sh600,000 na Sh800,000 na kuna baadhi ya watu wameahidi kurudi,  huku wakitaka alipie mapema kama ana fedha taslimu.

Hata hivyo, mkurugenzi wa manispaa hiyo, Hanifa Hamza alipoulizwa kuhusu hilo, amesema hawana taarifa.

"Hilo la kuwa kuna watu wanapangisha ndio hatuna taarifa nalo, ila tutalifuatilia na tukibaini kuna ukweli tutachukua hatua mara moja,” amesema.

Kuhusu kuongezewa muda wa mkataba, amesema “haitawezekana. Mpangaji aliyeingia pale tunaanza kumuhesabia tangu alipongia? Mfano mkataba wake unaanzia Januari itakapofika Januari ingine utakuwa umeisha na kutakiwa kuongeza kama atahitaji kuenendelea kuwepo.”

Baadhi ya wafanyabiashara waliofungua biashara zao katika stendi hiyo, wameiomba manispaa hiyo kuelekeza magari yote yanayopita Mwenge kuingia kwenye stendi hiyo, ili pachangamke wakati wakiwasubiri wafanyabishara wengine.

Mmoja wa wafanyabiashara hao aliyejitambulisha kwa jina moja la Richard, amesema ameamua kufungua kwa kuwa fedha aliyolipia kodi ni ya mkopo na siku zinazidi kwenda, hivyo anapaswa kuanza kufanya marejesho.

“Siwezi kusubiri hadi huo uzinduzi wao au wengine wafungue kwa kuwa kila mmoja anajua mahali alipozipata fedha za kodi na wengine tuna marejesho ya benki.

“Wito wangu Serikali ielekeze magari yote yanayopita hapa Mwenge kuingia humu ndani stendi walau tuweze kuuza kuliko ilivyo sasa unaneza kujikuta unaondoka na Sh10,000 hadi Sh15,000 ambayo ni hasara,” amesema mfanyabiashara huyo.

Naye Emmanuel Geofrey, amesema kuna haja ya manispaa kuangalia uwezekano wa kuwapa muda wa kuanza kulipa kodi kwa kuwa tangu wamelipia fremu hizo Novemba mwaka jana, imeshapita zaidi ya miezi mitatu sasa hakuna walichofanya.

Malina James, ameomba manispaa kuhakikisha walio na maduka wanapewa muda maalumu wa kuyafungua vinginevyo wapewe watu wenye nia ya kufanya biashara na kukumbushia yasije kutokea yale ya jengo la Machinga Complex lililopo eneo la Karume, ambalo licha ya wafanyabishara kuchukua maduka, walikwenda kufanyia biashara barabarani.

Kwa upande wa usafiri, tayari daladala zilizopangiwa safari eneo hilo zimeshaanza kazi, licha ya kuwa ni chache.

Mmoja wa madereva wa gari hizo, Omar Kija amesema bado hawapati abiria kama walivyotarajia kwa kuwa hapajaanza kufanya kazi, hivyo mara nyingi hufika kushusha watu hapo na kueleza daladala zilizopo hadi sasa hazidi 15 na wameanza kazi mwezi mmoja uliopita.