Wajawazito walazimika kwenda na maji hospitali kujifungua

Mkuu wa Wilaya ya Geita, Hashim Komba akimtwisha ndoo ya maji mkazi wa Wigembya Wilayani Geita..wananchi hao hawakuwahi na maji safi na salama na badala yake waliishi kwa kutegema maji ya visima vifupi.
Muktasari:
- Zahanati hiyo inayotegemewa na wananchi zaidi ya 13,000 wa vijiji vya Ikulwa na Wigembya haina huduma ya maji hivyo kuwalazimu kina mama wanaojifungua kutoka na maji nyumbani ili waweze kuopata huduma kwa hali ya usafi.
Geita. Wajawazito katika kijiji cha Ikulwa kilichopo katika Kata ya Ihanamilo, Halmashauri ya Mji Geita wanalazimika kubeba maji kwa ndoo kwenda kupata huduma ya kujifungua katika zahanati ya Ikulwa kutokana na kijiji hicho kukosa huduma ya maji safi na salama.
Kutokana na hali hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Geita, Hashim Komba ametoa muda wa siku 45 kwa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Geita (Geuwasa) kufanya usanifu wa namna gani watafikisha huduma ya maji kwenye zahanati hiyo na kisha kutafuta fedha zitakazokamilisha mradi ili zahanati hiyo ipate maji.
Wakizungumza wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi wa mradi wa maji wa Wigembya – Ikulwa, wananchi wa eneo hilo wamedai vijiji hivyo vyenye wakazi zaidi ya 13,0000 havijawahi kuwa na huduma ya maji ya bomba na wanaishi kwa kutumia maji ya visima vifupi ambayo sio salama kwa afya.
Mkazi wa Ikulwa, Rehema Shija amesema kukosekana kwa maji kwenye eneo lao ni changamoto inayowafanya wabebe maji kichwani wanapokuwa na uchungu ili wapate huduma ya kujifungua kwenye mazingira salama.
“Sasa ninazeeka, nina watoto na wajukuu, hiki kijiji hakijawahi kuwa na maji ya bomba, nimezaliwa hapa na kusomea hapa, ili mwanamke apate huduma ya kujifungua zahanati lazima abebe maji kutoka nyumbani hata kama ni usiku wa manane, hii ni kero kubwa kwetu.
“Tuna shule ziko hapa, hazina maji, mabinti zetu wanapata shida sana, ukiwa eneo lisilo na maji huwezi kuwa msafi, maisha yenu yanakuwa ya uchafu wakati wote. Niiombe sana Serikali isaidie maji yatufikie huku…Tumeanza kuona mwanga lakini huu mwanga utamulika kama zahanati itapata maji na shule zetu pia,” amesema Rehema.
Diwani wa Kata ya Ihanamilo, Joseph Lugaila amesema wananchi wa eneo hilo wana changamoto ya maji na mradi wa Wigembya – Ikulwa ulisimama kwa muda mrefu na sasa umeanza kutekelezwa upya, anaamini kuwa wananchi watapata maji safi na salama.
“Tunaomba sana maji haya yasambae yafike hadi zahanati, kina mama wanapokwenda kujifungua wanalazimika kubeba ndoo za maji kichwani ili wapate huduma, hata kwenye shule yetu ya sekondari hakuna maji na hii ni kero kubwa kwa wanafunzi hasa wa kike,” amesema Lugaila.
Enock Kasoga, mkazi wa Wigembya amesema kukosekana kwa maji katika maeneo yao kunachangia mgogoro kwenye familia kutokana na kina mama kuamka usiku kutafuta maji na baadhi ya wanaume kutowaamini, hivyo kusababisha ndoa kuvunjika.
Akizungumzia mradi huo ambao ulianza kutekelezwa mwaka 2021 na kusimama baada ya fedha kukosekana, Mhandisi wa mradi huo, Yohana Msheria amesema mradi ulianza kutekelezwa mwaka 2021/22 kwa fedha za PBR lakini ulikwama kutokana na wafadhili hao kutotoa fedha.
Amesema usanifu wa mradi uliokuwa chini ya Wakala wa Maji Vijijini na Usafi wa Mazingira (Ruwasa ) ulikuwa utekelezwe kwa gharama ya Sh489.2 milioni lakini fedha zilizotolewa ni Sh37 milioni pekee, hivyo kusababisha mradi kusimama.
“Mradi wa maji wa Igembya-Ikulwa ulisanifiwa kuhudumia wananchi 13,400 kwa gharama ya Sh489.2 milioni kazi zilizopaswa kufanyika kuboresha visima viwili, ununuzi na ufungaji wa pampu mbili, ujenzi wa tanki la maji lenye ujazo wa lita 90,000.
“Kazi nyingine ni ununuzi wa bomba na ujenzi wa mtandao wa kusambaza maji kilomita 10.5, ujenzi wa mtandao wa kusafirisha maji kilomita 3 na ujenzi wa wa vituo 10 vya kuchotea maji, ufungaji wa sola na nyumba mbili za pampu,” amesema Msheria.
Mradi huo sasa unatekelezwa na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mjini Geita (Geuwasa) na hadi sasa wametumia Sh4.8 milioni na kufanikisha wananchi wa Wigembya wanapata maji.
Meneja wa Geuwasa, Frank Changawa amesema tayari wamepima kiwango cha maji kinachozalishwa kwenye chanzo na kubaini kina uwezo wa kuzalisha lita 5,000 kwa saa na kuwa kwenye eneo hilo mahitaji ni lita za ujazo 10,000 kwa siku.
Amesema wamehamisha uzalishaji kutoka umeme wa jua na kwenda kwenye umeme unaozalishwa na Tanesco ili kuwa na huduma ya kuaminika usiku na mchanana wamejipanga kufanya usanifu wa namna gani maji yatafika kwenye kijiji cha Ikulwa na kuhudumia Zahanati inayotegemewa na wannachi hao.
Mkuu wa Wilaya ya Geita, Hashim Komba amesema mradi huo uliolenga kuwafikishia huduma wananchi zaidi ya 13,000 kwa mwaka 2021/22, haukufanikiwa na kuwa kwa sasa wananchi wameongezeka na kuitaka Geuwasa kufanya kazi usiku na mchana ili kufanya usanifu wa namna gani maji yatafika kwenye zahanati ya Ikulwa.
Amesema tanki lililopo sasa ni dogo lenye uwezo wa kujaza maji lita 5,000, hivyo ni vema wakaongeza tanki litakaloweza kujaza maji lita 10,000 ili lisambaze maji sehemu kubwa zaidi.
Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917