Wakazi wa Lukobe waomba kituo cha afya kifanye kazi saa 24

Muonekano wa Kituo cha Afya cha Lukobe baada ya kukamilika na kuanza kutoa huduma za afya wa wananchi wa kata za Lukobe,  Mayanga na Kihonda. Picha Hamida Shariff

Muktasari:

 Imeelezwa kuwa kama Kituo cha Afya cha Lukobe kingeweza kutoa huduma za afya saa 24 kingekuwa msaada mkubwa

Morogoro. Wakazi wa Kata ya Lukobe, Manispaa ya Morogoro wamesema licha ya kujengewa kituo cha afya,  kinashindwa kutoa huduma kwa saa 24 badala yake kinahudumia mchana.

Wakizungumza na Mwananchi Digital,  baadhi ya wakazi wa kata wamesema kituo hicho kama kingeweza kutoa huduma za afya saa 24 kingekuwa msaada mkubwa sio tu kwa wananchi bali hata kata ya jirani ya Mayanga iliyopo wilayani Mvomero.

Akizungumzia leo Ijumaa Machi 29, 2024, mkazi wa kata hiyo,  Shani Mohamed amesema awali kabla ya kukamilika kwa Kituo cha Afya cha Lukobe walikuwa wakipata huduma Kituo cha afya Mazimbu, zahanati za Kihonda na Magereza  kwa gharama kubwa zilizotokana na usafiri wa kufika huko.

"Tulivyoona tunajengewa kituo cha afya tuliamini tutapata huduma muda wote, huku kwetu kutokana na jiografia ilivyo, mtu akiugua usiku inakuwa changamoto kufika hospitali, tunajua ugonjwa siku zote usiku ndio unazidi; sasa hiki kituo chetu kinatoa huduma mchana tu sijui viongozi wanatufikiriaje kutusaidia," amesema Shani.

Ameongeza kuwa, pamoja na kutoa huduma za afya za kawaida,  kinapaswa kuimarisha huduma ya uzazi hasa  usiku kwa kuwa wajawazito wamekuwa wakipata shida na wengine kujifungulia njiani au nyumbani.

Mkazi mwingine,  Musa Rashid ameiomba Serikali kuongeza watoa huduma katika kituo hicho pamoja na dawa ili wagonjwa wanaofika kupata matibabu waweze kuhudumiwa kwa haraka na kupata dawa kulingana na magonjwa wanayougua.

"Suala kubwa ni dawa, tunaomba Serikali iongeze nguvu kwenye kuleta dawa, haitakuwa na maana kama tutakuwa na kituo cha afya chenye majengo mazuri halafu hakina dawa, mara nyingi tukienda kwenye zahanati na hivi vituo vya afy,  tunafuata maandishi ya daktari tu kwa sababu tukienda kwenye dirisha la dawa tunapewa dawa chache nyingine tunaambiwa tukanunue," amesema Rashid.

Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya cha Lukobe Christina Lufungulo amekiri kituo hicho kutoa huduma mchana tu hali inayosababishwa na upungufu wa watoa huduma.

"Kweli hiki ni kituo cha afya lakini tunashindwa kutoa huduma kwa saa 24 kwa sababu wahudumu tuko wachache, lakini naamini siku sio nyingi tutaongezewa wahudumu na hapo ndio tutakuwa kunatoa huduma wakati wote," amesema Christina.

Hata hivyo, amesema licha ya kufanyakazi mchana tu, kituo hicho kinatoa huduma zote muhimu ikiwamo huduma ya mama na mtoto, chanjo na magonjwa mengine.

Diwani wa Lukobe,  Selestine Mbilinyi amesema mbali ya uchache wa wahudumu kunakofanya kituo hicho kishindwe kutoa huduma saa 24, pia zipo changamoto kubwa ambayo ni kukosekana kwa umeme na maji.

Amesema kwa sasa kituo hicho kinatumia gharama kubwa kununua maji ya maboza kwa ajili ya matumizi kutokana na kutounganishwa na huduma ya majisafi na salama.

Kuhusu umeme, Mbilinyi amesema tayari gharama za kuunganisha zimeshalipwa lakini bado Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) hawajafikisha huduma hiyo.

Hata hivyo, amesema akiwasiliana nao mara kwa mara na anaamini siku sio nyingi umeme utaunganishwa kituoni hapo.