Wanachama 70 warejesha fomu kuutaka uspika, mmoja aingia mitini

Muktasari:

Wanachama 70 wamerudisha fomu za kuomba kuteuliwa kukiwakilisha Chama Cha Mapinduzi (CCM) kugombea nafasi ya Spika wa Bunge la Tanzania.

Dodoma. Wanachama 70 wamerudisha fomu za kuomba kuteuliwa kukiwakilisha Chama Cha Mapinduzi (CCM) kugombea nafasi ya Spika wa Bunge la Tanzania.

Akito taarifa baada ya kufungwa mchakato wa kuchukua na kurejesha fomu leo Jumamosi Januari 15, 2022 Msaidizi Mkuu Idara ya Oganaizesheni CCM Taifa, Solomon Itunda amesema wanachama 71 walichukua fomu na waliorejesha ni 70 huku mmoja akishindwa kurejesha mpaka muda uliowekwa kuisha.

Amesema idadi hiyo ni baada ya wanachama watano waliojitokeza leo Jumamosi ambapo waliochukua fomu katika ofisi za chama hicho Dar es Salaam wakiwa wanne huku mmoja akichukua Dodoma” amesema Itunda

“Leo ni siku yetu ya mwisho ya kutoa na kupokea fomu za wanachama wetu walioomba kuteuliwa kugombea nafasi ya Spika, jumla tuna wanachama 71 waliochukua mpaka tunahitimisha leo” amesema nakuongeza

“Katika wanachama hao wanaume wako 60 lakini wanawake wapo 11” amesema Itunda

Amewataja waliowaliojitokeza kuchukua fomu leo Dodoma ni Samweli Magero Magero huku Dar es Salaam wakijitokeza wanachama wanne ambao ni Rahim Rashid Ismail, Alex Mwita, Semistocles Rwegasira pamoja na Gragrey Nyalohala

Uchukuaji na urejeshaji fomu hizo ulianza Jumatatu 10, 2022 na kuhitimishwa leo Jumamosi na baada ya hapo hatua zingine zitafuata za kumpata mwanachama mmoja wa kukiwakilisha chama hicho.

Akitangaza ratiba ya chama hicho ya kumpata mgombea wa nafasi hiyo Jumapili Januari 9 katika ofisi Kuu za CCM Kisiwandui Zanzibar, Katibu Itikadi na Uenezi wa CCM, Shaka Hamdu Shaka alisema mchakato huo utahitimishwa Januari 31.

Shaka alisema Januari 17 sekretarieti ya halmashauri kuu ya Taifa itakutana kwa ajili ya kujadili wagombea na kuishauri kamati kuu ya halmashauri kuu ya taifa juu ya wagombea waliojitokeza.

Januari 18 hadi 19 kutakuwa na kazi ya kuchuja na kufanya uteuzi wa mwisho ambapo kamati kuu ya halmashauri kuu itafanya kazi hiyo.

Alisema kuanzia Januari 21 hadi 30 wabunge wa CCM watapiga kura kumpata mtu atakayekwenda kusimama bungeni kwa ajili ya kuomba kuchaguliwa kuwa Spika wa Tanzania.