Wananchi waandamana kudai maji Mwanza

Baadhi ya wakazi wa Mtaa wa Stone Town wilayani Ilemela mkoani Mwanza wakiwa wamebeba ndoo tupu za maji kuelekea katika ofisi za Mwauwasa zilizopo Kata ya Isamilo mkoani Mwanza kushinikiza kufikishiwa huduma hiyo. Picha na Mgongo Kaitira
Muktasari:
- Wananchi hao waliokuwa wakipita mitaa mbalimbali ya wilaya hiyo hadi ofisi za Mamlaka ya Maji na usafi wa Mazingira (Mwauwasa) zilizoko Mtaa wa Maji, Kata ya Isamilo Mkoani Mwanza huku wamebeba ndoo tupu.
Mwanza. Wakazi wa Mtaa wa Stone Town Wilaya ya Ilemela Mkoani Mwanza, wameandamana hadi ofisi za Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira (Mwauwasa) wakilalamikia kukosekana kwa huduma ya maji kwenye eneo lao.
Huku wakiimba nyimbo mbalimbali zinazoashiria kuhitaji huduma hiyo wakiwa na ndoo tupu kichwani, wamesema wanatumia wastani wa Sh3, 500 kwa siku kununua maji ya madumu.
“Shida ya maji ni kubwa sana, tunayafuata mbali mno, tunaomba Serikali na Waziri wa Maji, Jumaa Aweso aje atutue ndoo kichwani,” amesema Julieth Kilato, mkazi wa Mtaa wa Stone Town.

Mkazi mwingine, Gerald Kowero licha ya kueleza kuwa amewashuhudia baadhi ya watendaji wa Mwauwasa wakichimba mitaro katika mtaa huo na kulaza mabomba, amesema mpaka sasa mambomba ahayo hayajulikani yamepekwa wapi.
“Tuliona ajabu sana kwamba yale mabomba yalikuja kukusanywa tena na hatujui yalikopelekwa, tulishaandika barua kwenda Mwauwasa kuhusu suala la maji wakatuahidi kwamba watatuletea lakini hawajatimiza, ni kama tumetelekezwa,” amesema Kowero.
Huku akikumbusha maagizo yaliyotolewa na Makamu wa Rais Dk Philip Mpango alipozulu wilayani Ilemela kuwa Mwauwasa isambaze maji kwa wakazi hao, Kowero amesema anaamini bado Mwauwasa ina uwezo wa kutatua kero hiyo.
“Wengine tulishajaza mpaka fomu tukatayarisha mabomba kwenye makazi yetu na kuzipeleka ofisi ndogo za Mwauwasa zilizopo Nyakato lakini hadi leo (jana) hatujaona huduma,” amesema.
Mwenyekiti wa kundi la Stone Town, Rama Matoke amesema wanawake wanaoishi mtaa huo wenye kaya zaidi ya 200, ndio waathiriwa wakuu wa changamoto ya ukosefu wa maji na wanapoteza muda mwingi kusaka huduma hiyo badala ya kufanya shughuli za kuzalisha kipato.
“Ukimya huu umefanya sasa tuchukue uamuzi wa kwenda kuuona uongozi kuukumbusha wajibu wao na tunataka majibu kwanini hawakatimizi ahadi yao, tunajua Serikali yetu ni sikivu, tunaona mradi wa tanki umekamilika lakini tunashangaa kwa nini hatupati maji,” amesema.
Majibu ya Mwauwasa
Kufuatia suala hilo, Kaimu Mkurugenzi wa Mwauwasa, Neli Msuya amesema baadhi ya maeneo ya wilaya hiyo yamechelewa kupata maji kutokana na mvua kubwa zilizokuwa zinanyesha mkoani Mwanza.
Amesema mvua hizo zimechelewesha utekelezwaji wa mradi wa mtandao wa maji wenye urefu wa kilometa 48, unaogharimu zaidi ya Sh4.7 bilioni.
Hata hivyo, Msuya amesema baada ya mvua kupungua, shughuli ya kulaza na kuunganisha mabomba inaendelea huku shughuli hiyo ikitarajiwa kukamilika Mei 30, 2024 kwa kile alichodai kipande cha kilometa 2 ndicho ambacho mabomba hayajalazwa na utekelezaji wake ukiendelea.
“Tupo Mtaa wa National Housing, Buswelu ambako maunganisho ya bomba la maji yanafanyika kwenda Stone Town ambao ndio wa mwisho wa utekelezaji wa mradi huu wenye mtandao wa zaidi ya kilometa 48 ndani ya eneo la Buswelu,” amesema Msuya.
Ameongeza “kila tunapomaliza sehemu moja wananchi wanaendelea kupata huduma badala ya kusubiria tumalize mradi wote, kwa hiyo kuanzia kesho jioni (Alhamisi) wananchi wa eneo hili wanaanza kupata huduma.
Kuhusu mabomba yaliyohamishwa, amesema ilikuwa kipindi cha mvua, yalipelekwa katika eneo la tenki, kwa hiyo yapo mengine na ndio maana wanasema kufikia Mei 30, mwaka huu mradi utakuwa umekamilika.”