Wananchi watakiwa kutunza daraja la Mto Ruhuhu

Muktasari:

Wakazi wa vijiji vya Lituhi na Kipingu wameshauriwa kulinda miundombinu ya daraja la Mto Ruhuhu ambalo linaunganisha mikoa ya Ruvuma na Njombe kwa kuhakikisha wanazuia wizi wa vyuma hivyo pamoja na uharibifu.

Nyasa. Wakazi wa vijiji vya Lituhi na Kipingu wameshauriwa kulinda miundombinu ya daraja la Mto Ruhuhu ambalo linaunganisha mikoa ya Ruvuma na Njombe kwa kuhakikisha wanazuia wizi wa vyuma hivyo pamoja na uharibifu.

Wito huo umetolewa na mkuu wa kitengo cha mipango Tanroads,  Mhandisi Msama Msama wakati alipofanya ziara ya kutembelea daraja hilo kwa lengo la kukagua matengenezo ya kawaida  kwenye  daraja hilo ambalo limegharimu Sh9 bilioni kujenga msini na kutandika vyuma.

Amesema daraja hilo ni mkombozi kwa wakazi wa wilaya hizo hivyo wananchi wajitahidi kulinda miundombinu hiyo ili liweze kuendelea kuwasaidia  katika shuguli mbali mbali za kiuchumi  lakini pia limesaidia kurahisisha usafiri kwani wananchi kwa sasa wameweza kuvuka bila tatizo  tofauti na awali walikuwa wakipata changamoto ya kuliwa na mamba pamoja na voboko pindi mitumbwi inapopinduka   wakati wanapovuka.

“Kwa sasa daraja hili limekamilika na wananchi wanaweza kuvuka  bila tatizo tena nyakati zote za usiku na mchana hivyo kila mmoja ajitahidi kuwa mlinzi wa mwingine, ingawa tumeweka mlinzi ila sisi wananchi ndio tuwe wakwanza kulinda daraja hili ni mali yetu, kwani limekuwa mkombozi mkubwa ," amesema

Mkazi wa Kipingu, Fabian Mapunda amesema kukamilika kwa daraja hilo kumesaidia kuwarahisishia wananchi usafiri hasa akina mama wajawazito ambao walikuwa wakienda kujifungua ambao walikuwa wakitumia mitumbwi kuvuka kwenda kujifungua hospitali ya Litui hivyo wamemshukuru mkandarasi na wataalamu waliokamilisha ujenzi huo.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kampuni ya Jambela LTD, James Mbeya amesema kukamilika kwa ujenzi wa daraja hilo kutarahisiha shuguli za uchumi kwa wakazi wa miko ya Ruvuma na Njombe hivyo kuchochea kukua kwa uchumi na kuwapunguzia adha wakulima na wananchi kusafirisha mazao yao.

Amesema amefurahi kuwa  limekamilika na limejengwa na  Mtanzania kwani ilikuwa ndoto yake kuona Watanzania wakivuka kwa miguu kwenye mto huo badala ya mitumbwi na vivuko kwa kuwa mto huo umejaa mamba wengi na viboko na ndio maana alijitahidi kwa kushirikiana na wataalam  wa Tanroads kufanya kazi usiku na mchana  ilikukamilisha ujenzi wa daraja.