Wanavyowafahamu wapya, walioachwa ukuu wa mkoa

Muktasari:

  • Wadau wa siasa na biashara Kanda ya Ziwa wametoa maoni tofauti kuhusu uteuzi wa wakuu wa mikoa wapya watano katika eneo hilo, huku baadhi yao wakihoji kigezo kilichotumika kumrejesha Albert Chalamila, ambaye uteuzi wake ulitenguliwa Juni mwaka jana.

Mwanza/Musoma. Wadau wa siasa na biashara Kanda ya Ziwa wametoa maoni tofauti kuhusu uteuzi wa wakuu wa mikoa wapya watano katika eneo hilo, huku baadhi yao wakihoji kigezo kilichotumika kumrejesha Albert Chalamila, ambaye uteuzi wake ulitenguliwa Juni mwaka jana.

“Najiuliza ni nini alichofanya Chalamila akaonekana hafai kuwa mkuu wa mkoa wa Mwanza na kitu gani alichokifanya sasa hadi akapata sifa za kuwa mkuu wa mkoa wa Kagera?” alihoji John Heche, Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema

“Hivi unawaambiaje watu wa Kagera kuwa aliyetumbuliwa Mwanza ana sifa za kuwaongoza wao,” alihoji.

Akifafanua, Heche ambaye pia ni mbunge wa zamani wa Tarime Vijijini alisema mfumo wa sasa wa uteuzi unaotoa mamlaka makubwa kwa Rais, unajenga jamii ya watu wanaoishi kwa kujipendekeza ili wateuliwe, hali aliyosema inapunguza uwajibikaji katika masuala ya msingi yenye masilahi kwa umma.

Wakati maoni ya mitandaoni yakielezea Ali Hapi alicheleweshwa kuondolewa, Mwenyekiti wa Chemba ya Wafanyabiashara wa Viwanda na Kilimo (TCCIA) mkoa wa Mara, Boniface Ndengo alisema alijitahidi kusimamia matumizi ya fedha za umma, japo hakuweza kuifikia sekta binafsi ambayo ndio injini ya maendeleo na uchumi.

Hata Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Samuel Kiboye alisema Hapi alimudu kudhibiti nidhamu ya watumishi na matumizi ya fedha za umma, hivyo akamtaka mkuu mpya wa mkoa, Raphael Chegeni kuendeleza alipoishia mtangulizi wake.

Baadhi ya kauli za Ally Hapi akiwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa wakati wa utawala wa Rais wa awamu ya tano, Hayati John Magufuli zinatajwa kumgharimu.

Chalamila na mtihani mpya

Mkuu mpya wa Mkoa wa Kagera, Albert Chalamila ana kibarua kizito cha kudhibiti kauli zake tata ambazo zimekuwa zikimgharimu kisiasa na kupoteza uaminifu kwa mabosi wake.

Baada ya kukaa nje ya utumishi kwa kipindi cha siku 412, Chalamila amerejea akichukua nafasi ya Meja Jenerali Charles Mbuge.

Kwa nyakati mbili tofauti akiwa Mbeya na Mwanza aliwahi kupewa tahadhari na wakuu wake wawili, Hayati John Magufuli na Samia Suluhu Hassan kutokana na kauli zake tata na katika hotuba zake ambazo zimejaa uchangamfu wa kupitiliza.

Akiwa mkoani Mbeya katika moja ya ziara za Hayati Magufuli katika mkutano uliofanyika Uwanja wa CCM Ruanda Nzovwe, Chalamila alimshukuru Rais kwa kumlipa mshahara mzuri unaomtosha hata kukaa na mchepuko.

Kauli hiyo ilichekesha wengi, lakini ilionekana kumkera JPM. Baadaye akiwa ziarani Chunya ambako pia Chalamila alitamka maneno yanayofanana na hayo akimshukuru kwa kumletea Mkuu wa Wilaya mzuri, Rais alisema mkuu wa mkoa anapenda michepuko baada ya kutekeleza maagizo.

Katika moja ya hafla za kuwaapisha viongozi aliowateua Rais Samia alimtolea mfano Chalamila kama kiongozi mwenye papara kwenye baadhi ya maamuzi yake, hivyo kumpa tahadhari.

Pamoja na hayo, mwanazuoni Dk Paul Luisilie alimwelezea Chalamila kama mchangamfu katika hotuba zake, lakini uchangamfu huo unapitiliza na kusababisha kupoteza nafasi yake kama kiongozi kijana aliyeaminiwa.

Baadhi ya maoni ya watu yanamtaja kama mtendaji mzuri, lakini kinachomgharimu ni kauli zake kwa kuwa hajui kuchunga ulimi wake.

Chalamila aliteuliwa kuwa mkuu wa mkoa wa Mwanza Mei 15, 2021 akitokea Mbeya alikodumu kwa takribani miaka minne tangu Julai 29, 2018 alipoteuliwa na Hayati John Magufuli.

Kabla ya kushika wadhifa wa mkuu wa mkoa alikuwa mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa, wadhifa alioupata Desemba 5, 2017 baada ya kushinda katika uchaguzi wa ndani wa chama hicho.

Kabla ya kuibukia katika siasa, Chalamila alikuwa mhadhiri msaidizi katika Chuo Kikuu cha Tumaini mkoani Iringa na amewahi kuwa mwalimu katika shule mbalimbali.

Chegeni, kukosa ubunge hadi ukuu wa mkoa

Aliyekuwa mbunge wa Jimbo la Busega mkoani Simiyu, Dk Raphael Chegeni alikosa ubunge mwaka 2020 baada ya jina lake kutoteuliwa, licha ya kuongoza katika kura za maoni.

Chegeni alipata kura 209 kati ya 673 za wana CCM wa jimbo la Busema mkoani Simiyu.

Katika kinyang’anyiro hicho, Chegeni, aliyekuwa akitetea nafasi yake alimwacha mbali mshindani wake kisiasa, Dk Titus Kamani aliyepata kura 84, akifuatiwa na Simon Songe aliyepata kura 49, lakini akateuliwa na CCM kugombea na kushinda ubunge Busega.