Wanawake kujadili uelewa wa bima nchini

Naibu Kamishna wa Bima, Khadija Said.
Muktasari:
- Wanawake waliopo katika sekta ya bima wataadhimisha siku ya wanawake duniani visiwani Zanzibar kwa kujadili mchango wao kwenye sekta hiyo na kuongeza uelewa kuhusu bima nchini.
Dar es Salaam. Kuelekea kilele cha siku ya wanawake duniani, zaidi ya wanawake 300 katika sekta ya bima wanatarajiwa kukutana Zanzibar Alhamisi wiki hii katika kongamano lenye lengo la kutambua mchango wa wanawake katika kuongeza uelewa juu ya bima nchini.
Kwa mujibu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Bima Tanzania (Tira), wanawake wa sekta hiyo wamekuwa mstari wa mbele kuhamasisha wanawake wenzao kujiunga na bima mbalimbali hususani za vikundi ili waweze kubadilisha maisha yao.
Naibu Kamishna wa Bima, Khadija Said, amesema kuna idadi kubwa ya wanawake wasomi katika sekta hiyo ambao baadhi yao wamejiajiri wenyewe kama mawakala wa bima, ingawa kuna changamoto kadhaa.
“Katika mkutano huo mada mbalimbali zitawasilishwa na wataalamu wa bima zitakazoendana na kaulimbiu ya mwaka huu inayozungumzia masuala ya ubunifu, ili watu wengi zaidi wafikiwe na huduma za bima ni lazima teknolojia ichukue nafasi yake,” amesema Khadija.
Amesema kabla ya kilele, mamlaka hiyo imeandaa mikutano ya kupokea maoni kuhusu huduma za bima, ambayo tayari ilishafanyika Pemba na itafanyika pia Unguja Machi 8.
Kwa upande mwengine mwenyekiti wa kamati ya shirika hilo Fikira Ntomola amesema kongamano hilo pia litahudhuriwa na watu maarufu mfano wake wa viongozi wa rais wa zamani lengo ni kuonesha mchango wa wanawake katika sekta hiyo na kujadili nini kinapaswa kuwa. kufanyika zaidi ili elimu ya bima iweze kufika mbali zaidi.
“Tunawaomba wadau wote kujumuika nasi katika kongamano hili muhimu na kujifunza mengi kutoka kwa wataalamu wa bima, tuliwashukuru washirika wetu kwa msaada wao katika kuhakikisha linafanyika Zanzibar,” amesema Fikira.