Wasichana waongoza matokeo kidato cha pili Zanzibar

Muktasari:
Wanafunzi 2,895 hawakufanya mtihani.
Zanzibar. Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar imetangaza matokeo ya mtihani wa kidato cha pili kwa mwaka 2017 ambayo wasichana wameongoza kwa kupata asilimia 60.34 ya ufaulu.
Waziri wa wizara hiyo, Riziki Pembe Juma ametangaza matokeo hayo leo Jumanne Januari 30,2018 alipozungumza na waandishi wa habari.
Amesema ufaulu kwa jumla umeongezeka kutoka asilimia 70.1 mwaka 2016 hadi asilimia 73.98 mwaka 2017.
Riziki amesema matokeo kwa jumla yanaonyesha watahiniwa 34,458 sawa na asilimia 73.98 wamefaulu kati yao wasichana wakiwa ni 20,793 sawa na asilimia 60.34 na wavulana ni 13,665 sawa na asilimia 39.66.
Amesema wanafunzi 46,580 sawa na asilimia 94.07 walifanya mtihani huo mwaka 2017 kati yao wasichana ni 26,061 sawa na asilimia 55.95 na wavulana ni 20,519 sawa na asilimia 44.05.
Waziri amesema wanafunzi walioandikishwa kufanya mtihani walikuwa 49,515 kati yao wasichana ni 27,239 sawa na asilimia 55.01 na wavulana 22,207 sawa na asimilia 44.99.
Amesema wanafunzi 2,935 sawa na asilimia 5.3 hawakufanya mtihani kwa sababu mbalimbali zikiwamo za maradhi, utoro, ndoa na vifo.
Riziki amesema wanafunzi 2,895 hawakufanya mtihani kutokana na utoro, 27 kwa ugonjwa, watano uhamisho, watano kutokana na ndoa na watatu walifariki dunia.