Wawili jela maisha kwa kumbaka mtoto wa miaka sita

Muktasari:

  • Wawili wafungwa maisha kwa kubaka mtoto wa miaka sita kwa nyakati tofauti katika kijiji cha Mkulani Wilayani Masasi.

Mtwara. Wakazi wawili wa Kijiji cha Mkulani, wilayani Masasi, wamehukumiwa kutumikia kifungo cha maisha jela, baada ya kukutwa na hatia ya kumbaka mtoto wa miaka sita kwa nyakati tofauti.

Akizungumza na waandishi habari leo Desemba 06, 2023 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Nikodemus Katembo amesema kuwa watu hao walifikishwa mahakamani kwa tuhuma za kubaka mtoto huyo mwenye umri miaka sita kwa nyakati tofauti.

Kamanda Katembo amewataja watu hao kuwa ni Omary Salum (70) maarufu baba Hasnath na Emmanuel Chihote (32) maarufu kama baba Mary.

Wakati Salumu ametiwa hatiani kwa kosa la kumbaka mtoto huyo Novemba 17, 2022 saa 11 jioni kijijini kwao, Chihote ametiwa hatiani kwa kosa la kumbaka mtoto huyohuyo  Novemba 21, 2023 saa 9 alasiri.

Kwa mujibu wa kamanda huyo, watuhumiwa hao walikamatwa katika Kijiji cha Mkulani na baadaye kufikishwa mahakamani ambapo walikutwa na hatia na kuhukumiwa kifungo cha maisha jela.

“Jeshi la Polisi linapenda kutoa wito kwa wananchi wote kuendelea kutoa ushirikiano ili kukomesha kabisa matukio ya kihalifu hasa unyanyasaji dhidi ya watoto, hatua kali za kisheria zitaendelea kuchukuliwa ili kuufanya mkoa huu kuwa sehemu salama ya kuishi,” amesema Kamanda Katembo.