Waziri Mwigulu: Tozo inauma lakini…

Waziri wa Fedha na Mipango nchini Tanzania, Dk Mwigulu Nchemba akizungumzia kuhusu tozo leo jijini Dodoma

Muktasari:

Waziri wa Fedha na Mipango nchini Tanzania, Dk Mwigulu Nchemba ametetea tozo zinazotozwa kwenye miamala ya kifedha akisema kama taifa kuna majukumu ya msingi ambayo kila Mtanzania anatakiwa kuyabeba.

Dar es Salaam. Waziri wa Fedha na Mipango nchini Tanzania, Dk Mwigulu Nchemba ametetea tozo zinazotozwa kwenye miamala ya kifedha akisema kama taifa kuna majukumu ya msingi ambayo kila Mtanzania anatakiwa kuyabeba.

Dk Mwigulu ameyasema hayo leo Alhamisi Septemba Mosi, 2022 jijini Dodoma wakati akitoa ufafanuzi kuhusu tozo ambazo zimekuwa zikilalamikiwa na wadau mbalimbali wakiwemo wananchi wa kawaida kila kona.

Amesema tozo hizo zilizoanzishwa kwenye bajeti ya mwaka 2021/22, zimekuwa msaada mkubwa kwa taifa kwa sababu zimesaidia kuchochea maendeleo kupitia miradi mbalimbali inayotekelezwa hapa nchini.

Waziri Mwigulu: Tozo inauma lakini…

Dk Mwigulu amesema wanatambua machungu yanayotokana na tozo lakini lazima Watanzania wabebe jukumu la msingi la kuleta maendeleo ya taifa hasa kupitia miradi ya kimkakati ya maendeleo inayotekelezwa.

“Ni tozo, ndiyo, ina maumivu ya hapa na pale, ndiyo na tunatambua kweli kwamba inavuruga ‘purchasing power’ ya mtu mmoja mmoja lakini tuna majukumu ambayo kama nchi na sisi wote kama wazazi tunawajibika kuyabeba kama wajibu wetu,” amesema Dk Mwigulu.

Waziri huyo amesisitiza mapato ya tozo katika mwaka wa fedha 2021/22, Sh221 bilioni zilikwenda kugharamia mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu na Sh117 bilioni zilikwenda kujenga vituo vya afya.

“Tozo hii si kodi ya biashara wala si kodi inayotokan na faida ya biashara, bali chimbuko lake ni ushirikiano wa pamoja kuunganisha nguvu ili tuweze kupata rasilimali tutekeleze majukumu hayo ambayo ni ya lazima,” amesema.

Dk Mwigulu amesisitiza tozo hizo zimeendelea mwaka huu wa 2022/23 kwa sababu kuna majukumu ya msingi ambayo serikali haiwezi kuyaahirisha. Amewataka wananchi kuendelea kushiriana na serikali katika ujenzi wa miradi ya maendeleo.

“Mwaka huu tuliendelea tena kwa sababu tuna majukumu ya msingi ambayo hatuwezi kuyaahirisha. Hapa tulipo hatuwezi kuahirisha bwawa la Nyerere, hatuwezi kuahirisha reli ya kisasa, na matunda yake mtayaona baadaye,” amesema waziri huyo.

Amesema mwaka huu Serikali imepanga kujenga madarasa yasiyopungua 8,000 mwaka huu ili wanafunzi watakaojiunga na kidato cha kwanza mwaka 2023, waweze kukaa vizuri kwenye madarasa.