Wenye vibali ruksa kufyatua fataki mwaka mpya

Muktasari:
Jeshi la Polisi Mkoani Mbeya limeonya wananchi kutojihusisha na ufyatuaji holela wa fataki usiku wa mkesha wa Mwaka Mpya 2022 na kwamba wenye vibali pekee ndio watakaoruhusiwa kwa maelekezo maalumu katika mkoa huo.
Mbeya. Jeshi la Polisi Mkoani Mbeya limeonya wananchi kutojihusisha na ufyatuaji holela wa fataki usiku wa mkesha wa Mwaka Mpya 2022 na kwamba wenye vibali pekee ndio watakaoruhusiwa kwa maelekezo maalumu katika mkoa huo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Urlich Matei amelieleza Mwananchi leo Ijumaa Desemba 31, 2021 huku akitoa angalizo kwa wenye vibali kuepuka upigaji wa fataki katika maeneo yenye makazi ya watu ili kuepukana na taharuki inayoweza kujitokeza.
''Wapo ambao wanaendekelea kuchukua vibali vya kupiga fataki ikiwa ni ishara ya kusherekea sikuu ya kuvuka mwaka 2021 na kuukaribisha mwaka mpya wa 2022 hivyo tabia za wananchi kupiga ovyo hazitaruhusiwa ''amesema
Kamanda Matei amepiga marufuku uchomaji wa matairi barabarani, kuziba kwa mawe barabara na kupiga madebe kwa lengo la kulinda hali ya usalama wa raia na mali zao na kwamba Polisi wataimarisha ulinzi katika maeneo mbalimbali ikiwamo katika nyumba za ibada.
Kamanda Matei amewataka watendaji na wenyeviti wa Serikali za mitaa kushirikiana na wananchi katika kuimarisha vikundi vya ulinzi shirikishi.
Mwenyekiti wa Mtaa wa sabasaba, Ally Mbika amesema kuwa hali ya ulinzi itaimarishwa licha ya kuwepo kwa changamoto ya vifaa hususan filimbi na kuliomba Jeshi la Polisi kuona umuhimu wa kutoa kwa viongozi wa ngazi za kata.