Wizara yataka wanawake kugombea kwa wingi uchaguzi ujao

Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Mwanaidi Ali Khamis, akizungumza katika uzinduzi wa Programu ya TELS (Think Equal Lead Smart) iliyoanzishwa na Umoja wa Maofisa Watendaji Wakuu wa kampuni (CEO Roundtable) leo Aprili 18, 2024.

Muktasari:

  • Katika nafasi ya uwaziri idadi ya wanawake imeongezeka hadi kufikia asilimia 37 ya Baraza la Mawaziri ikilinganishwa na asilimia 15 iliyokuwapo mwaka 2005

Dar es Salaam. Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Mwanaidi Ali Khamis amewataka wanawake kujitokeza kwa wingi kuwania uongozi katika uchaguzi wa Serikali za mitaa na uchaguzi mkuu mwakani ili kufanikisha malengo ya kuwa na usawa wa kijinsia katika nafasi za uongozi.

Tanzania ambayo kwa sasa inaongozwa na Rais mwanamke (Samia Suluhu Hassan) inatarajia kufanya uchaguzi wa Serikali za mitaa mwishoni mwa mwaka huu na uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani mwishoni mwa mwaka 2025.

Akizungumza katika uzinduzi wa Programu ya TELS (Think Equal Lead Smart) iliyoanzishwa na Umoja wa Maofisa Watendaji Wakuu wa kampuni (CEO Roundtable) leo Aprili 18, 2024, Mwanaidi ambaye ni Mbunge wa viti maalumu (CCM) amesema serikalini kuna hatua imepigwa katika uongozi wa wanawake.

"Wote tunaelewa hivi karibuni tutakuwa na uchaguzi, kina mama mjitokeze kwa wingi ili kumsaidia Rais katika kufanikisha usawa wa 50/50 katika nafasi za uongozi. Napendekeza mradi kama huu tunaouzindua leo uwafikie wanawake wengi zaidi, hususani wa vijijini," amesema.

"Katika usawa wa nafasi za uongozi serikalini hatua imepigwa, kuna uwakilishi katika nafasi mbalimbali kwa wastani wa asilimia 30," amesema Mwanaidi akisisitiza hali ilikuwa tofauti takribani miongo miwili iliyopita.

Ametoa mfano katika nafasi ya uwaziri idadi ya wanawake imeongezeka hadi kufikia asilimia 37 ya Baraza la Mawaziri ikilinganishwa na asilimia 15 iliyokuwapo mwaka 2005.

Kwa upande wa wabunge na wawakilishi, idadi imeongezeka kutoka asilimia 22 ya wanawake hadi asilimia 38 hivi sasa.

Mkurugenzi Mtendaji wa CEO Roundtable, Santina Benson amesema katika mradi huo wataangazia masuala ya sera na utamaduni, ambayo yanamkwamisha mwanamke kushika nafasi za uongozi, pia kuwa na mchango mkubwa kwenye uchumi.

"Maelfu ya wanawake wanatarajiwa kunufaika na mradi wa TELS, lengo ni kuongeza uwepo wa wanawake katika uongozi na kuongeza mchango wao katika uchumi. Hii ni mpaka kwetu maana kati ya wanachama wa CEO Roundtable wanawake ni asilimia 18 tu, hivyo kuna haja ya kuongeza idadi yao," amesema Benson.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Chama cha Waajiri nchini (ATE), Suzanne Ndomba amesema ili kufikia malengo ya kuwa na usawa wa kijinsia katika nafasi za uongozi kuna haja ya kuoanisha baadhi ya sheria na kuwa na sera bora za mahali pa kazi.

Ametoa mfano wa masuala yahusuyo umri wa mtu mzima na likizo ya uzazi.

"Katika suala la utu uzima kuna sehemu miaka inafofautina pengine 18 sehemu nyingine 21 lakini binafsi siamini kama mtoto wa miaka 14 anaweza kuwa na uamuzi sahihi wa kuolewa. Kadhalika katika masuala ya mahali pa kazi sheria ya kazi inatoa wiki 12 za likizo ya uzazi na miezi sita ya kunyonyesha, kuna haja ya sera za mahali pa kazi kuboreshwa na kuongeza zaidi ya hapo ili kumfanya mwanamke kuwa na tija zaidi," amesema Ndomba.

Mwenyekiti wa Vodacom Foundation, Harriet Lwakatare amesema ni muhimu kuthamini safari ya mabadiliko na uwezeshaji wa wanawake.

"Kwa pamoja ni kuleta mabadiliko tunayotamani kwa watu tunaowahudumia. Wanawake wana nafasi kubwa ya kutengeneza kesho iliyobora kwa watu wote," amesema.