Zabuni ukarabati Mto Msimbazi kufunguliwa Julai

Naibu Waziri wa Tamisemi, Josephat Kandege (kulia) akizungumza na Mbunge wa Mbulu Vijijini, Flatei Massay walipohudhuria kikao cha 47 cha mkutano wa Bunge la Bajeti, jijini Dodoma leo. Picha na Edwin Mjwahuzi
Muktasari:
Kauli hiyo imetolewa leo bungeni na Naibu Waziri Tamisemi, Josephat Kandege
Dodoma. Naibu Waziri wa Tamisemi, Josephat Kandege amesema zabuni ya ukarabati wa Mto Msimbazi jijini Dar es Salaam itafunguliwa Julai 20, 2018.
Kandege amesema hayo leo Julai 8, 2018 bungeni mjini Dodoma wakati akijibu swali la nyongeza la mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Susan Lyimo.
Lyimo amehoji ni lini miundombinu ya Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (Dart) eneo la Jangwani inahamishwa kwa kuwa mvua zikinyesha eneo hilo hujaa maji na kuwa katika hali mbaya.
Akijibu swali hilo Kandege amesema, “mvua za safari hii zimekuwa nyingi kuliko miaka ya nyuma. Kuondoa gereji ya pale Jangwani sio ngumu ila tunataka kuimarisha na tuna mpango mahususi kwa jiji la Dar es Salaam.”
Amesema mpango huo ni pamoja na kuimarisha bonde la Mto Msimbazi, kwamba Julai 20, 2018 watafungua zabuni ya kandarasi ya ukarabati mkubwa wa bonde hilo na kumtaka Susan kuwa na subira.
Mbunge wa Kondoa Mjini (CCM), Edwin Sanda amehoji ni lini Serikali itajenga daraja la Kingale ambalo limevunjika kutokana na mvua kubwa.
Katika majibu ya swali hilo, Kandege amesema, “fedha zote zilizotengwa kwa dharura, yaani theluthi mbili ya fedha za dharura zilizotengwa kwa Tarura zimetumika kurudishia miundombinu ya jiji la Dar es Salaam.”