Zaidi ya wanajeshi 40 wauawa Ukraine, mataifa yalaani

Muktasari:

  • Wakati taarifa za kuongezeka kwa idadi ya watu waliofariki baada ya Russia kuivamia Ukraine leo, viongozi mbalimbali duniani wametoa matamko ya kulaani uvamizi huo wakitaka usitishwe mara moja.

Wakati taarifa za kuongezeka kwa idadi ya watu waliofariki baada ya Russia kuivamia Ukraine leo, viongozi mbalimbali duniani wametoa matamko ya kulaani uvamizi huo wakitaka usitishwe mara moja.

Karibu watu 18 na wanajeshi 40 wa Ukraine wameripotiwa kuuawa katika mashambulizi ya anga yaliyofanywa na Russia leo Alhamisi Februari 24, 2022 asubuhi katika mji wa Odessa ulio pwani ya Black Sea, serikali imesema.

Taarifa zinasema zaidi ya wanajeshi 40 na raia 10 wamefariki katika saa za mwanzo za uvamizi huo, Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine aliwaambia waandishi.

"Najua kwamba zaidi ya wanajeshi 40 na maelfu wengine kujeruhiwa. Ninajua kuwa raia kumi wamepoteza maisha," amesema msaidizi wa rais, Oleksiy Arestovych alipozungumza na waandishi.

Wakati viongozi wakiendelea kulaani huku nchi wanachama wa Umoja wa Kujihami (Nato) wakipanga kukutana kesho kuchukua hatua, Russia imesema itaendelea kuunga mkono waaasi wa Ukraine na majeshi yake yataendelea kuwa nchini humo hadi watakapoona matokeo.

Msemaji wa serikali ya Russia, Dmitry Peskov alisema "idadi kubwa" ya Warussia wanaunga mkono waasi wa mashariki mwa Ukraine. "Ndio maana tunaweza kutegemea kuwa hili litaungwa mkono pia," amesema Peskov.

Hakusema ni muda gani majeshi ya Russia yataendelea kuwa Ukraine, akisema kuwa uamuzi wa Rais Vladimir Putin utategemea "matokeo."

Rais Putin alizindua uvamizi huo leo na kusababisha wananchi kukimbia makazi yao.

Mashambulizi ya anga ya Russia yalilenga vituo vya kijeshi nchini humo, na majeshi ya ardhini yaliingia kutokea kaskazini, kusini na mashariki, na kuamsha matamko ya kulaani kutoka kwa viongozi wa nchi za Magharibi.

Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky alitangaza kutumika kwa sheria za kijeshi na kusema Russia inashambulia miundombinu ya kijeshi ya nchi yake na kuwataka wananchi wasiwe na taharuki na kuahidi ushindi.

Jeshi la Ukraine limesema limepokea maagizo kutoka kwa Zelensky kuwa "lisababishe hasara kubwa kwa wavamizi".

Rais wa Marekani, Joe Biden alizungumza na mwenzake wa Ukraine, Zelensky mara baada ya uvamizi, akiahidi kumuunga mkono na kumsaidia.

Biden amelaani uvamizi huo ambao haujatokana na kuchokozwa na usio halali na kuahidi kuwa Russia itawajibishwa.

Jijini Brussels, mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya (EU), Josep Borrell amesema Russia inakabiliwa na hali ya kutengwa ambayo haijawahi kutokea kwa kuwa EU itaweka vikwazo ambavyo haijawahi kuweka.

Jijini Rome, waziri mkuu wa Italia, Mario Draghi amesema leo kuwa uvamizi wa Russia hauna uhalali na hauwezi kuhalalishwa, akisema Ulaya na Nato zinafanyia kazi hatua za haraka.

"Serikali ya Italia inalaani shambulio la Russia kwa Ukraine. Hauna uhalali na hauwezi kulalalishwa. Italia iko pamoja na wananchi wa Ukraine na serikali katika muda huu mgumu," amesema Draghi katika taarifa yake.

Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron anatarajiwa kulihutubia taifa kuhusu uvamizi wa Russia leo.

Pia Korea Kusini imesema itaungana na nchi nyingine kuweka vikwazo vya kiuchumi vya kimataifa dhidi ya Russia kutokana na uvamizi huo.

"Uhuru, heshima ya mipaka na utaifa la Ukraine lazima uhakikishwe," alisema Rais Macron katika taarifa yake iliyotolewa na Ikulu.

Korea Kusini itaunga mkono na kushiriki katika jitihada za jumuiya ya kimataifa, zikiwemo za vikwazo vya kiuchumi," aliongeza.

Nayo Uturuki imesema uvamizi wa Ukraine haukubaliki na kuishauri Russia kuacha uvamizi huo usio halali na unaokiuka sheria.

"Tunachukulia shughuli hizo za kijeshi kuwa hazikubaliki na tunazikataa," inasema taarifa ya wizara ya mambo ya nje.

Nayo Israel imelaani uvamizi huo ikisema ni ukiukwaji wa sheria za kimataifa, huku ikionyesha uhusiano wake wa karibu na nchi zote mbili.