Zungu: Ilala kuwa Jiji ni pigo kwa wapigaji
Muktasari:
Mbunge wa Ilala (CCM), Mussa Azzan Zungu amesema uamuzi uliofanywa na Rais John Magufuli wa kulivunja Jiji la Dar es Salaam na kuipandisha hadhi manispaa ya Ilala kuwa Jiji la Dar es Salaam utawaudhi wapigaji wengi na kuwafurahisha wananchi.
Dar es Salaam. Mbunge wa Ilala (CCM), Mussa Azzan Zungu amesema uamuzi uliofanywa na Rais John Magufuli wa kulivunja Jiji la Dar es Salaam na kuipandisha hadhi manispaa ya Ilala kuwa Jiji la Dar es Salaam utawaudhi wapigaji wengi na kuwafurahisha wananchi.
Zungu ameyasema hayo leo Alhamisi Februari 25, 2020 mbele ya Rais John Magufuli ambaye leo yupo katika siku ya pili ya ziara yake ya siku tatu na amezindua soko la Kisutu na studio za televisheni ya Channel 10 na redio Magic FM.
“Wapigaji wamekasirika lakini wananchi tumefurahi sana mheshimiwa Rais, kuna watu mnapitapita mnatafuta vyeo jamani msililie ndizi mkungu si wenu,” ametahadharisha Zungu.
Zungu amemwambia Rais Magufuli kuwa pamoja na kupandishwa hadhi Ilala ina changamoto katika majimbo yake matatu kwani miundombinu bado, kuna maeneo mvua zikinyesha kunakuwa na shida ya barabara.
“Miradi ya DMP namba mbili utusaidie tupate barabara katika jimbo hili mtandao wa barabara ni kilomita 133 katika hizo, kilomita 55 lami inayoridhisha lakini 17 ni lami mbaya, kilomita 52 za barabara za vumbi.”
“Nikuombe kwa huruma yako ukienda hili ulitizamie, biashara nyingi zimekufa wawekezaji hawaji mjini kwa sababu miundombinu si rafiki halmashauri hii mpya miundombinu ikikamilika hujengi barabara kunawekeza,” amesema Zungu.
Awali mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Aboubakar Kunenge amesema wakati Rais Magufuli anaingia madarakani hospitali na vituo vya afya vilikuwa vichache lakini kwa sasa kuna ongezeko.
“Hospitali zilikuwa saba sasa tunazo 11 ikifika Mei mwaka huu tunatarajia Temeke itajenga hospitali za wilaya kwa fedha zake za ndani, Kinondoni tumejenga kwa fedha za ndani mwishoni mwa Machi tutaanza kutoa huduma.”
“Vituo vya afya vilikuwa nane kwa sasa vipo 20, zahanati zilikuwa 94 kwa sasa 121, upatikanaji wa dawa ulikuwa asilimia 81 sasa ni 94,” amesema Kunenge.