Kuoa mapema, siri wanaume kuishi umri mrefu zaidi

Dar es Salaam. Ukiachana na masuala ya kiimani, wataalamu wa saikolojia wanasema mwanaume kuoa mapema humsaidia kutulia kiakili na hivyo uwezekano wa kuishi kwa muda mrefu huwa ni mkubwa.

Kauli ambayo inaungwa mkono na baadhi ya madaktari ambao wamezungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti kuhusiana na suala hilo, akiwamo Dk Ali Mzige.

Anasema mwanaume akitaka kuishi maisha marefu duniani, anapaswa kuoa mapema.

Daktari huyo anasema; “Kama mwanaume amefikia umri wa kuoa ni heri akaoa, kwa maana wengi wao wanaotimiza wajibu huo hupata utulivu, wanakuwa na afya nzuri kuliko wale ambao hawajao na kujikuta wakiishi ubachela.”

Dk Mzige alisema kuoa mapema tu hakutoshi, bali pia anatakiwa awe na uzito unaoendana na urefu wake, hali itakayomsaidia pia kujiepusha na maradhi yasiyo ya kuambukiza.

Wakati Dk Mzige akiyasema hayo, Daktari bingwa wa magonjwa ya fiziolojia ya homoni na mazoezi ambaye ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Muhas, Fredrick Mashili alipozungumzia hilo alisema suala la umuhimu wa tendo la ndoa na mazoezi kwa mwanaume linatajwa zaidi katika kuimarisha afya yake.

Anasema, “Tendo la ndoa lina umuhimu kwa mwanaume pia katika kujikinga na tezi dume, lakini ni ngumu kusema afanye mara ngapi kwa siku au hata mwezi. Lakini mazoezi pia ni sehemu ya kuondoa msongo wa mawazo kwake, hivyo anapaswa kuzingatia haya,” anasema Dk Mashili.

Suala hilo linaungwa mkono na msaikolojia Kimangale anayesema kuwahi kuingia katika uhusiana wa kindoa lina faida kubwa kwa mwanaume na kwa mwanamke pia.

“Ndoa inamfanya mwanaume kuwa na vipaumbele hasa pale anapokuwa na uhusiano wenye afya, hii maana yake anakuwa na mwenzake wa kubadilishana naye mawazo na kuelezana mambo kadha wa kadha.

“Pia anapokuwa kwenye ndoa hujua namna ya kuwekeza rasilimali zake ikiwemo fedha tofauti na yule ambaye hajaoa,” anasema.

Kwa mujibu wa Kimangale, mwanaume ambaye hajaoa ni rahisi kujiingiza katika maisha yanayoweza kumfanya aharibikiwe au kufa mapema.

Hivyo, anasema kuna umuhimu mkubwa kwa mwanaume kuushughulisha mwili na kuepuka tabia zisizofaa kama kunywa pombe pamoja na kutokula katika muda sahihi hususan chakula cha usiku.

Hata hivyo, Mtaalamu wa saikolojia, Josephine Tesha anasema si kila mwanaume anayeoa mapema anaweza kuishi kwa muda mrefu, bali inategemea uimara wa afya ya akili na uchumi wake.

“Utaishi maisha marefu kama upo kwenye ndoa yenye amani, kama ndoa inakusumbua, hautaweza kuwekeza na ukawa na afya bora ya akili, hivyo itakuwa rahisi kupata maradhi na kufanya uamuzi hatarisha kwa maisha yake mwanaume huyo,” anasema.


Kutokana na ukweli kwamba asilimia kubwa ya wanaume hufa mapema ikilinganishwa na wanawake, wataalamu wa afya pamoja na wanasaikolojia tiba nao wametaja vidokezo muhimu vya afya vinavyomwezesha mwanaume kuishi kwa muda mrefu.

Sambamba na hilo, wametaja aina za mazoezi na mtindo wa maisha utakaomfanya aendelee kubaki na uzito unaoshauriwa sambamba na kutozeeka mapema.

Wakati hayo yakielezwa, Shirika la Afya Duniani (WHO) linasema wastani wa umri wa kuishi binadamu duniani ni 72, lakini kwa mwanaume ni miaka 69 na miezi minane na mwanamke ni 74 na miezi miwili.

Wataalamu wanasema wakati wanaume wengi wangependelea kuwa na maisha marefu, kutokana na kukiuka au kutozingatia kanuni za afya, hujikuta wakifariki dunia mapema kwa magonjwa yasiyoambukiza kutokana na mtindo wa maisha.

Mtaalamu wa afya ya jamii, Dk Ali Mzige anasema mtindo bora wa maisha ni jambo la msingi kwa mwanaume yeyote anayehitaji kuwa na afya njema.

Anataja usingizi kuwa ni kitu cha muhimu kwa mwanaume yeyote, “Sijui wangapi wanajali kuhusu hili, inashauriwa mwanaume apate muda wa kulala wa saa 6 mpaka 8, itamsaidia mwili wake kupumzisha mwili na ubongo hali itakayomsaidia kuwa na afya njema.”

Hata hivyo, anasema wapo wanaume wenye changamoto ya kutopata usingizi wa kutosha kutokana na vinasaba.

Dk Mzige anasema mwanaume kama hanywi pombe, havuti sigara, anafanya mazoezi ya kutembea na anapata usingizi wa kutosha, afya yake huimarika zaidi.

Anasema ulaji wa vyakula vya asili kama ugali wa dona, mbogamboga, nyama chukuchuku na matunda kwa wingi huimarisha zaidi kinga zake za mwili tofauti na ikiwa atakula vyakula vya kukaangwa ama kuungwa na mafuta kila mara.

Kwa mujibu wa Dk Mzige, mwanaume anayeweza kuwa na afya nzuri ni yule anayejali afya yake, kama anaumwa atakwenda kutibiwa na anayezingatia kuushughulisha mwili wake kwa kazi mbalimbali.

Hata hivyo, Dk Mzige anataja pia suala la uchangiaji damu kuwa ni tabia inayosaidia kumfanya mwanaume kuwa na afya nzuri na ogani imara zaidi kwa sababu akifanya hivyo, damu yake hujizalisha upya.

Hata hivyo, Dk Mzige anataja pia suala la uchangiaji damu kuwa ni tabia inayosaidia kumfanya mwanaume kuwa na afya nzuri na ogani imara zaidi kwa sababu akifanya hivyo, damu yake hujizalisha upya.

“Uchangiaji wa damu pia husaidia kuboresha afya, tafiti zinaonyesha kati ya watu 100 Tanzania wenye uwezo wa kuchangia damu mara nyingi hujitokeza 56 kati yao, huu utafiti niliufanya mimi kupitia watu 10,000.

“Wanaume wengi hawaelewi umuhimu wa kuchangia damu katika kuboresha afya zao, unapochangia damu, inatengenezwa damu nyingine katika mfumo wako, changamoto wengi hawana huu uelewa,” anasema Dk Mzige.

Anataja pia umuhimu wa kupima afya mara kwa mara. Anasema kwa kufanya hivyo kunamsaidia mwanaume kufahamu afya yake kama ana mambukizo, aende kutibiwa hususan shinikizo la damu na kisukari.

Lakini anahimiza tabia ya unywaji maji mara kwa mara nayo inafaida zake, kwa sababu asilimia 60 ya uzito wa binadamu ni maji.


Msongo wa mawazo

Mtaalamu wa Saikolojia tiba, Saldin Kimangale anasema maisha na kifo havipo kwenye mikono ya mtu, isipokuwa binadamu amepewa nguvu ya vitu anavyovimiliki na anatakiwa kuendesha maisha yake kwa kufuata kanuni za kimaumbile.

Anasema mtu anapoishi kwa kutumia kanuni za kimaumbile, maana yake uthamani wa maisha yake utakua bora, akitolea mfano wa kuepuka vihatarishi na kufanya maisha yake yawe na thamani.

Anasema changamoto ya msongo wa mawazo kwa mwanaume huharibu kinga zake za mwili na kusababisha uwezo wa mwili kupambana na maradhi kuwa mdogo.

“Mwanaume ataishi katika hali ya udhaifu na kutokuwa na nishati ya kutosha, huyu mtu akipata maambukizo ni rahisi kwake kupoteza maisha, hivyo cha kufanya ni kudhibiti msongo wa mawazo kazi ambayo ni ngumu kwa wanaume wengi,” anasema.

Kimangale anasema wengi wao hawajajenga tabia ya kutafuta usaidizi ukilinganisha na wanawake wao ambao hujitafutia msaada wao wenyewe. Anasema hali hiyo huwasababishia msongo wa mawazo.

Mwanaume hupambana mwenyewe, mpaka watu waje kugundua tayari jambo limefika mbali, hiyo inawaweka wengi kwenye hatari ya kuishi katika maisha au afya duni kwa sababu hawatafuti msaada kwa wakati,” anasema.

Anasema takwimu zinaonyesha watumiaji wengi wa ulevi na mihadarati ni wanaume kwa sababu mbalimbali, mojawapo ni kuepukana na msongo wa mawazo.

Kimangale anasema wengi wanaingia huko kwa lengo la kuondoa msongo, kupata nguvu fulani au kutaka kukubalika katika kundi la watu, vitu vinavyomuweka kwenye hatari ya kupata maradhi au ajali za barabarani, maambukizo ya virusi vya ukimwi na mengineyo.

Anataja eneo lingine linalosababisha msongo wa mawazo kwa mwanaume ni uhusiano wa kimapenzi na mawasiliano.

“Ni wagumu kwenye kuwasiliana na hasa kuwasilisha hisia zake, kama mwanaume atajifunza namna bora ya kuwasilisha hisia na kuhusiana, atapunguza changamoto zinazoweza kuwafanya kupoteza maisha kwa kujinyonga, kuua na kujiua,” anasema.


Yanayopaswa kuepukwa

Unene uliopitiliza sambamba na kitambi, ni mwiba mwingine kwa wanawake walio wengi, lakini hali ni tofauti kwa wanaume ambao hali hiyo haiwaumizi kichwa.

Hata hivyo, wataalamu wa afya wameonya kuwa kitambi ni moja ya sababu inayomfanya mwanaume kupata magonjwa yasiyoambukiza na hivyo kufupisha maisha yake kwa kuugua.

Dk Mzige anataja uzito, unene uliozidi au uliokithiri kuwa chanzo kwa baadhi ya wanaume kupata magonjwa yasiyoambukiza.

“Lakini magonjwa ambayo yhmdhuru mwanamke kiafya, hata mwanaume hudhurika nayo pia.

“Mfano shinikizo la damu, sukari na hata saratani ambavyo mara nyingi wengi hudhania huwakumba zaidi  wanawake, lakini ni hatarishi hata kwao, hivyo kuna umuhimu mkubwa wa kupima afya mara kwa mara sambamba na kula mlo kamili kwa kuzingatia makundi matano ya chakula ili kuwa na uzito sahihi unaolingana pia na urefu wa muhusika,” anasema.

Daktari huyo anasisitiza kuwa afya ya mwanaume inaweza kutetereka kama atakuwa na tabia ya kujichua pia.

Anasema wapo badhi hawataki kuwa na uhusiano na mwanamke wa kimpanzi na anajenga tabia ya kujichua akidhani kuwa ndiyo atamaliza hamu ya kufanya tendo la ndoa lakini si kweli. “Tabia hii huleta athari mbaya kwa mwanaume ataanza kushindwa kutimiza haja pale afanyapo tendo la ndoa.”