Sababu za ganzi mwilini hizi hapa

Muktasari:

  • Uwepo wa ganzi miguuni na kuchomachoma ni moja ya chanzo cha  muathirika kupata michubuko au mikato au michaniko. Hii ni kutokana na upungufu wa hisia za fahamu miguu.

Ganzi au kuchomachoma kama pini butu au hisia ya pini ichomayo juu juu au hisia ya kuwaka moto inaweza kuhisiwa maeneo mbalimbali mwilini, ingawa mara kwa mara huwa ni miguuni.

Ganzi kitabibu hujulikana kama numbness, kuchomachoma ni tingling au hisia za kuwaka moto ni burning sensation. Maeneo mengine ya  mwilini ambayo hupata hisia hizi ni pamoja na mikononi, vidoleni, mabegani, shingoni na katika meno.

Uwepo wa ganzi miguuni na kuchomachoma ni moja ya chanzo cha  muathirika kupata michubuko au mikato au michaniko. Hii ni kutokana na upungufu wa hisia za fahamu miguu.

Hali hii ni hatari kwa mwenye kisukari cha aina ya pili, kwani ndio chanzo cha kupata vidonda vibaya visivyopona na matokeo yake kuwa katika hatari ya kukatwa mguu.

Zifuatazo ni sababu zinazoweza kusababisha dalili na viashiria vya ganzi au kuchomachoma au kuwaka moto.

Ulalo usio rafiki na kukaa mahali pamoja muda mrefu huweza  kugandamiza au kubana mishipa ya fahamu ambayo ndio yenye kupokea misisimko ya mfumo wa fahamu.

Kupata majeraha katika mgongo au kiuno ambako ndio mishipa mingi ya fahamu inayochomoza katika uti wa mgongo.

Uwepo wa mgandamizo unaoleta shinikizo katika mishipa ya fahamu inayotokea katika uti wa mgongo, mfano santuri za mgogo zinapochoropoka au kuhama.

Mishipa ya fahamu inaweza kuathirika kutokana na uvutaji tumbaku, unywaji pombe, matibabu ya chemotherapy na mionzi.

Kuumwa na wadudu wenye sumu kali kama vile nyoka, buibui, tandu na pia samaki wenye sumu au kuumwa na wanyama.

Shinikizo katika mishipa ya fahamu baada ya kugandamizwa mshipa wa damu uliotuna, uvimbe, kovu la tishu na uwepo wa uambukizi.

Upungufu wa vitamin B mwilini ni moja ya sababu ya mara kwa mara inayochangia kupata dalili hizi hasa kwa watu wenye umri mkubwa ambao miili yao ufanisi wa unyonyaji umepungua.

Damu kuwa chache au kutofikia sehemu fulani mwili ikiwamo kwa kujeruhiwa na theluji au kutokana na mishipa ya damu kuharibika.

Kuwa na kiwango kisicho cha kawaida cha madini ya kalisiamu, patasiamu na sodiamu.

Kukosa mtawanyo wa damu katika maeneo ambayo mishipa ya damu imeharibika kutokana na mrundikano wa mafuta mabaya au kutokana na kuungua na barafu au kupata shambulizi.

Kuugua magonjwa kama vile kisukari, kiharusi au kiharusi kilichotokana na kuziba kwa mishipa ya damu, mishipa ya damu  kuharibika, kifafa au degedege, matatizo ya tezi ya shingo na uvimbe katika ubongo.

Vile vile maambukizi ya virusi vya mkanda wa jeshi na kinga kushambulia tishu za ubongo.

Tatizo la mgandamizo wa mishipa ya fahamu katika kiganja cha mkono, hali inayojulikana kitabibu kama carpal tunnel syndrome.

Tatizo hili hutibika kutegemeana na chanzo au kisababishi kilichobainika na huwa ni kawaida pia chanzo kutokujulikana na tatizo likawa la kudumu.

Mfano kama una carpal tunnel au matatizo ya chini ya mgongo daktari anaweza kukupa mazoezi tiba.

Mwenye kisukari anaweza kutibiwa kwa udhibiti kiwango cha sukari kwa dawa  au kwa mazoezi mepesi na vyakula.

Kwa mwenye upungufu wa vitamin B au madini anaweza kupewa tembe za virutubisho tiba.

Hizi ndio sababu zinazochangia dalili hizi, fika katika huduma za afya kwa ushauri zaidi.