Dk Karl Peters: Mfano mbaya wa matumizi mabaya ya madaraka
Muktasari:
Mwanzoni Serikali ya Ujerumani haikumuunga mkono, lakini baadaye iliridhia na akafanikiwa kuanzisha koloni la Wajerumani la Afrika Mashariki.
Dk Karl Peters alizaliwa mwaka 1856 akiwa mtoto wa nane wa mchungaji wa Kilutheri. Baada ya masomo ya sekondari alisoma historia na falsafa katika vyuo vikuu vya Gottingen, Tubingen na Berlin alipohitimu shahada yake ya uzamivu.
Kwa muda wote aliokuwa chuoni, alivutiwa zaidi na falsafa ya Udarwini wa Kijamii ambao moja ya mafundisho yake ni kutoa haki kwa wenye nguvu na wababe duniani kuwatawala na kuwakandamiza watu dhaifu.
Mafundisho haya kwa kiasi kikubwa yaliathiri tabia yake na kumuondolea roho ya ubinadamu.
Suala la Ujerumani kutokuwa na koloni hadi muda ule lilimsikitisha na aliamini kuwa Ujerumani kama taifa kubwa barani Ulaya, ilistahili kuwa na makoloni mengi kama ilivyokuwa Uingereza.
Mnamo Machi 1884 alianzisha Shirika la Ukoloni wa Kijerumani. Baada ya hapo aliandaa safari yake ya Afrika kipindi ambacho mataifa ya Ulaya yalikuwa yakiandaa mkutano wa Berlin kuhusu makoloni.
Alipofika Afrika Mashariki baada ya kupata idhini kutoka kwa Sultani wa Zanzibar, aliingia mikataba ya kilaghai na machifu wa Usagara, Uzigua, Nguru na Ukami na katika muda mfupi, yaani kuanzia tarehe 23 Novemba hadi 17 Desemba 1884, alijipatia jumla ya eneo la kilometa 140,000 za mraba.
Mwanzoni Serikali ya Ujerumani haikumuunga mkono, lakini baadaye iliridhia na akafanikiwa kuanzisha koloni la Wajerumani la Afrika Mashariki.
Wanahistoria wengi wanamkumbuka Karl Peters kama mtu katili,m asiyekuwa na hata chembe ya ubinadamu. Alijijengea umaarufu mkubwa miongoni mwa wenyeji hasa kutokana na matendo yake ya ukatili dhidi ya wananchi.
Kutokana na ukatili wake wananchi wakambatiza jina la Mkono wa Damu. Alifanya maovu mengi ambayo kama ingekuwa katika zama tulizonazo pengine angeburutwa katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC).
Mwaka 1891, akiwa na cheo cha kamishna wa Kaisari katika eneo la Kilimanjaro, alifanya kituko kimoja ambacho ni mfano mbaya kabisa wa matumizi mabaya ya madaraka.
Akiwa kiongozi alikuwa na tabia ya kuwa na mabinti wengi wenyeji aliowatumia kama wapenzi wake. Usiku wa tarehe 18 Oktoba 1891 alimfumania mmoja kati ya wapenzi aitwaye Yagodja akiwa na mtumishi wake wa kiume aitwaye Mabruk.
Akiwa na hasira kali, mara moja Peters akaitisha mahakama ya kijeshi akiwa yeye mwenyewe hakimu na kumhukumu Mabruk anyongwe hadi afe. Yagodja alikimbia lakini alikamatwa mnamo Januari 1892 akahukumiwa adhabu ya viboko na kunyongwa hadi afe. Haikuishia hapo, akaamuru kijiji alichotoka Yagodja katika eneo la Rombo kichomwe moto. Ilipofika hapo Wachagga hawakukubali. Walinyanyua juu silaha zao na kupambana na Wajerumani. Kama si ujasiri wa Kapteni Emmil von Wissmann Wajerumani wangeng’olewa eneo la Kilimanjaro.
Aprili 1892, Gavana Julius von Soden akiwa Dar es Salaam alipokea barua kutoka kwa Mmisionari wa Kiingereza aliyekuwa Kilimanjaro ikieleza kuwa sababu ya vita kule Kilimanjaro ni unyama alioufanya Peters.
Kitendo hiki kilimchefua Gavana na kuharibu kabisa uhusiano wake na Peters. Kwa kuwa Peters alikuwa ni mteule wa Kaisari Gavana hakuwa na mamlaka ya kumwondoa kwenye cheo chake.
Gavana aliwasiliana na serikali yake jijini Berlin akieleza kuwa adhabu za kifo hazikuwa za haki na Peters alitumia madaraka yake vibaya kwa kiburi na kisasi binafsi. Shinikizo zilipozidi, Peters alijiuzulu mwaka 1893.