Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Tatizo si Muungano wenyewe bali kasoro katika muundo wake

Siku zimepita kama moshi, wiki zimehesabika kama vidole, miezi imekatika kama zilikumbwa na dhoruba na sasa tunahesabu miaka 55 ya kuungana Tanganyika na Zanzibar hapo Aprili 26, 1964.

Nchi hizi zilipoungana idadi ya watu wake ilikuwa milioni 11 sasa inakadiriwa zaidi ya milioni 50 (Zanzibar ilikuwa 300,000 na sasa takriban milioni 1.6).

Muungano huu umepitia mitihani na mitikisiko mingi, lakini zaidi si juu ya kuundwa kwake bali mfumo wake.

Wakati zipo nchi za Afrika na kwingine ziliungana kwa raha na furaha lakini haikuchukua muda kuwa karaha na kila moja kwenda njia yake, Muungano wa Tanzania bado unahimili vishindo.

Kwa sasa hakuna dalili za Muungano wetu kusambaratika. Hata hivyo si vyema kufumbia macho nyufa zilizopo ambazo zinataka ukarabati, maana usipoziba ufa utajenga ukuta.

Kinachosikika ni mafanikio yake, hasa ya kuwaleta pamoja watu wa Bara na Visiwani, lakini malalamiko yanayosikika hata katika Bunge na Baraza la Wawakilishi, hayapewi uzito unaostahiki.

Mara nyingi zimeundwa kamati kubwa na ndogo, tume za uchunguzi na za ushirikiano kutafuta undani wa malalamiko, lakini hali ni ileile vilevile na mapendekezo ya nini kifanyike hutiwa kapuni na kusahaulika.

Katika kikao cha karibuni cha Bunge zilisikika kelele za Wabunge wa Zanzibar juu ya utendaji kazi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) unaoiumiza Zanzibar kiuchumi na mwananchi wa kawaida. Hata viongozi husikika wakisikitikia hizo kero zisizomalizika.

Waasisi wa huu Muungano, Mwalimu Julius Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume, pia walionyesha kuwa Muungano ulikuwa na matatizo.

Mwalimu alisema muungano ulikuwa wa hiari na si wa kulazimishana. Mzee Karume alisema Muungano ni kama koti ambalo ukilichoka unalivua.

Mfano, Karume hakulipenda Azimio la Arusha la 1967 kwa kuwa Zanzibar haikuhusishwa katika utayarishaji wake.Alisema: “Mwisho wa Azimio ni kisiwa cha Chumbe”.Kisiwa hiki kipo nje kidogo ya Unguja unaposafiri kutoka Dar es Salaam .

Bara kulikuwapo mtafaruku na wabunge 55 waliotaka ‘ifufuliwe’ Tanganyika. Wengi wa hawa walipoteza nyadhifa zao serikalini na wapo waliotangazwa kuwa si raia.

Miongoni mwa kauli zinazowakera watu wa Visiwani ni za kusema Zanzibar ni sawa na wilaya ndogo ya Bara na haistahili kuangaliwa kama nchi.

Vilevile yamesikika malalamiko ya Zanzibar kutokuwa huru kujiamulia mambo inayoona ni ya maslahi na kwake, ikiwamo kukopa au na kuchagua viongozi wake.

Bara tumesikia watu wanaodai Zanzibar inadekezwa na inafaidika zaidi na kwamba Wazanzibari bungeni hujadili mambo ya Bara wakati wenzao wa Bara hawashiriki mijadala ya Zanzibar.

Katika sekta za fedha na biashara pia yapo malalamiko. Haya ni pamoja na bidhaa zinazozalishwa Zanzibar, kama sukari, kuwekewa vikwazo kuingia Bara wakati bidhaa zinazotoka nje ya Tanzania haziwekwi vikwazo.

Rais mstaafu, Jakaya Kikwete katika kile kilichoonekana kama kujibu hoja aliwahi kusema Wapemba wamejazana Bara na wanalima vitunguu.

Wazanzibari walimwambia na watu kutoa Bara wamejazana Visiwani. Hawa ni pamoja na mafundi cherehani na wamachinga.

Hata kuondolewa hati za usafiri kati ya Bara na Visiwani kunalalamikiwa na Zanzibar kwa vile kumetoa nafasi ya kuingia kiholela watu kutoka nchi jirani na kufanya uhalifu.

Muungano ulipoundwa, Rais wa Zanzibar alikuwa moja kwa moja Makamu wa Kwanza wa Rais na kama Rais angelitoka Visiwani mwenzake wa Bara angekuwa Makamo wa Kwanza wa Rais.

Kuondolewa kwa makubaliano haya kunalalamikiwa na wapo wanaoona yamefanywa zaidi kisiasa kuliko kuzingatia maslahi ya nchi.

Suala la uchimbaji wa mafuta lilileta mtafaruku , lakini hatimaye imekubaliwa kwa kila upande wa ushughulikie mafuta yaliyopo eneo lake.

Nchi nyingi nchi ziliungana baada ya watu wake kuulizwa, lakini muungano wetu haukupita njia hiyo na wapo watu wanaoiona hiyo ni dosari.

Muungano ulikuja ghafla, kama kimbunga, bila ya hodi. Aprili 26, 1964 la Mwalimu na Karume alitia saini mkataba wa Muungano bila ya taarifa za awali za mpango huo.

Aliyekuwa Spika wa Bunge la Muungano, Pius Msekwa, alikiri mara kadhaa kuwa makubaliano ya Muungano yalifanywa kwa siri na haraka kutokana na upepo wa kisiasa na usalama.

Aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Zanzibar, Wolfango Dourado aliwekwa kizuizini na Tanzania Bara kwa kueleza mara nyingi kwamba yeye na mawaziri hawakushirikishwa juu ya kuungana na Tanganyika.

Zipo kauli tofauti za nani kati ya Mwalimu na Karume alitoa ushauri wa kuungana na hili limebakia siri ambayo waasisi hawa walikufa nayo.

Muungano ulipoundwa ulikuwa na sura ya kisiasa na ulibeba maeneo 11, ikiwa pamoja na mambo ya ndani na nje. Fedha, biashara, kilimo, elimu, afya, mafuta na mawasiliano hayakuwamo katika orodha hiyo.

Ushirikiano wa kimataifa haukuwa katika orodha hio na ndio maana Zanzibar chini ya utawala wa Rais mstaafu, Salmin Amour ilijiunga na Jumuiya ya Nchi za Kiislamu (OIC).

Hatua hii ilizusha mtafaruku na hatimaye Zanzibar ililazimishwa kujitoa baada ya kuahidiwa Tanzania ingejiunga. Sasa ni karibu miaka 25 na suala hili halizungumzwi.

Hata hivyo, watu wa nchi hizi mbili kubaki kuwa wamoja ni hatua ya kupongezwa kwa sababu wengi waliojaribu kufanya kama Tanzania walishindwa njiani.

Ukichunguza utaona Watanzania wengi, Bara na Visiwani, hawauoni Muungano kuwa tatizo. Kinachowasumbua ni mambo gani ni ya Muungano na yapi siyo.

Hivi karibuni tumesikia kelele juu ya muundo wa Muungano. Wapo wanaosema mfumo wa serikali mbili uendelee, wapo wanaotaka serikali moja na wengine wameshauri tuunde shirikisho la serikali tatu.

Tume ya Katiba iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba, baada ya kukusanya maoni ya wananchi na vingozi mbali mbali, ilipendekeza mfumo wa serikali tatu. Lakini siku hizi suala hili halisikiki kama vile hapakuwepo umuhimu wa kukusanya maoni ya wananchi na kuunda Bunge la Katiba.

Ni vizuri wakati tunafurahia mafanikio ya Muungano pia tusifumbie macho kero na malalamiko yaliopo.