CCM kuwabana watendaji wa Serikali Mbeya
Muktasari:
- CCM imesema itawachukulia hatua kali watendaji na wakuu wa idara za Serikali ambao hawatatimiza wajibu wao.
Mbeya. CCM imesema itawachukulia hatua kali watendaji na wakuu wa idara za Serikali ambao hawatatimiza wajibu wao.
Akizungumza wakati wa maadhimisho ya miaka 47 ya chama hicho yaliyoambatana na mkutano wa hadhara wa kusikiliza na kutatua kero za wananchi, Katibu mwenezi wa CCM mkoani humo, Christopher Uhagile amesema watachukua hatua kali viongozi wa Serikali wanaoshindwa kusikiliza na kutatua changamoto za wananchi.
“Huu ndio mwelekeo mpya wa CCM chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, anayetaka kuona wananchi wake wanapata huduma kwakuwa serikali imewekeza fedha nyingi katika miradi ya maendeleo,” amesema Uhagile.
Uhagile ameongeza kuwa katika kuhakikisha wananchi wanasikilizwa na kutatuliwa kero zao, CCM mkoani humo imeandaa ratiba ya kila wilaya kuhakikisha wanakutana na wananchi kusikiliza mahitaji yao.
“Kuanzia Februali 9 hadi 10 tutakuwa Chunya, Februari 12 na 13 Kyela, Februari 15 na 16 Rungwe na Februari 18 na 19 tutakuwa Mbarali hivyo wakurugenzi wote mnapaswa kuhakikisha mikutano hiyo inafanyika bila changamoto.
“Lakini niwaombe wananchi mjitokeze kwa wingi katika mapokezi ya kiongozi wetu Makonda ambaye atafanya ziara hapa Mbeya mjini na Mbarali kwa siku mbili kuanzia Februali 8 na 9,” amesema.
Katika hatua nyingine, Mjumbe wa Halmashauri kuu ya CCM Taifa (Mnec), Ndele Mwaselela amewatoa hofu wananchi mkoani humo kuhusu changamoto ya umeme, akieleza kuwa muda si mrefu tatizo hilo litaisha.
“Suala la umeme ni la kitaifa na tayari Rais ameshalitolea maelekezo, hivyo tuwe na uvumilivu muda wowote tunaenda kusahau changamoto hii, serikali ya awamu ya sita ipo makini kuhakikisha wananchi wake wanapata huduma zote,” amesema Mwaselela.