Tukabiliane na mabadiliko ya tabianchi kulinda vyanzo vya maji

Kuna uhusiano mkubwa kati ya mabadiliko ya tabianchi na utatuzi wa changamoto za maji, hii inaonyesha umuhimu wa kuhifadhi na kusimamia vyanzo vya maji kwa faida ya vizazi vijavyo.
Uhusiano kati ya maji na mabadiliko ya tabianchi ni wa karibu na una athari kubwa kwa mifumo ya maji ya dunia.
Mabadiliko ya tabianchi yanaweza kusababisha mzunguko wa maji usio wa kawaida, kama vile ongezeko la ukame katika maeneo fulani na mafuriko katika maeneo mengine.
Kwa mujibu wa taarifa za Shirika la UNESCO, kati ya mwaka 2002 na 2021, ukame uliathiri zaidi ya watu bilioni 1.4, ukisababisha vifo vya karibu watu 21,000.
Kuyeyuka kwa barafu na theluji, kunaweza kusababisha kupungua kwa vyanzo vya maji safi na yale ya kunywa kwa mamilioni ya watu wanaotegemea mito inayotokana na barafu.
Ongezeko la joto la dunia pia linaweza kusababisha upungufu wa mvua au zile zisizotabirika, zinazoweza kuathiri uzalishaji wa chakula na kuathiri vyanzo vya maji.
Kwa hiyo, mabadiliko ya tabianchi yanaweza kusababisha migogoro ya maji, upungufu wa maji safi, na hatari kwa usalama wa chakula na afya ya binadamu.
Kuna hatua kadhaa zimetajwa kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi kwenye vyanzo na upatikanaji wa maji nchini Tanzania.
Serikali inaendelea kuchukua hatua muhimu kutimiza lengo lake la kutoa maji safi na salama kwa asilimia 85 ya wakazi wa vijijini na asilimia 95 ya wakazi wa mijini ifikapo mwaka 2025.
Kwa dhati, tunapongeza jitihada zinazofanywa na serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi katika kuhakikisha wananchi wanapata maji salama kwa uhakika na unafuu.
Kwa upekee mkubwa, naipongeza Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira (Tanga UWASA) kwa kuzindua hivi karibuni uuzaji wa hati fungani ya kijani yenye thamani ya Sh53 bilioni. Kitendo cha mamlaka hiyo kutafuta uwezeshaji wa kifedha mbadala ni cha kuigwa na taasisi zote nchini.
Kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi kwenye vyanzo na upatikanaji wa maji nchini, kunahitaji hatua za haraka na mikakati endelevu. Hapa kuna baadhi ya hatua muhimu zinazoweza kuchukuliwa.
Kwanza ni uhifadhi wa misitu na mazingira asilia. Misitu ni muhimu kwa kudhibiti mzunguko wa maji na kuhifadhi vyanzo vya maji.
Kupanda miti na kulinda misitu itasaidia kudhibiti mmomonyoko wa udongo, kuhifadhi maji ya mvua, na kuhifadhi bioanuai.
Kwa hili napenda kuipongeza kampuni ya Mwananchi na Taasisi ya Aga Khan Foundation kwa kitendo chao cha kupanda miti jijini Dar es Salaam. Kitendo hiki ni cha kuigwa na kinapaswa kufanywa na wadau wote wa maendeleo nchini.
Kuongeza ufanisi wa matumizi ya maji. Kupunguza matumizi ya maji kwa njia ya ufanisi zaidi katika kilimo, viwanda na matumizi ya kaya kunaweza kusaidia kudumisha vyanzo vyake.
Kwa hili tunapongeza hoteli zote ambazo zina sera ya udhibiti wa matumizi kwa kuwaomba wageni wao kutumia maji kwa uangalifu.
Uendelezaji wa miundombinu ya uhifadhi wa maji, kujenga na kuboresha miundombinu ya uhifadhi kama vile mabwawa, mifereji na mifumo ya uhifadhi wa maji ya mvua, itasaidia katika kudhibiti mafuriko na kuhifadhi maji kwa matumizi ya baadaye.
Kuendeleza kilimo cha mseto na kinachoweza kustahimili ukame ni muhimu. Kilimo cha umwagiliaji na matumizi ya mazao hayo kunaweza kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi kwenye kilimo na usalama wa chakula.
Kuimarisha sera na sheria za usimamizi wa mazingira na rasilimali za maji, pamoja na kusimamia matumizi bora na udhibiti wa uchafuzi wa maji ni muhimu katika kuhifadhi na kusimamia vyanzo vyake.
Hata hivyo, itolewe elimu kwa umma ufahamu wa mabadiliko ya tabianchi na umuhimu wa uhifadhi vyanzo vya maji.
Kuwahamasisha watu kutumia maji kwa ufanisi zaidi na kuchukua hatua za kuhifadhi mazingira ni sehemu muhimu ya kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi kwenye vyanzo vya maji.
Kwa kuchukua hatua hizi na kutekeleza mikakati ya kudumu, Tanzania inaweza kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi kwenye vyanzo na upatikanaji wa maji.
Muhimu ni kuhakikisha rasilimali muhimu ya maji inalindwa kwa vizazi vijavyo. Maji hi uhai, maji ni afya, maji ni chakula na maji ni chanzo cha utulivu na amani duniani.
Frank Abel ni mdau wa maendeleo endelevu, akiangazia zaidi mabadiliko ya tabianchi. Anapatikana kwa namba ya simu +255 753 73 23 55.