Edna Lema: Yanga Princess itakuwa tishio

Dar es Salaam. Idadi kubwa ya timu zinazoshiriki Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania Bara, zinafundishwa na makocha wanaume na ni chache tu ambazo zimeamua kutoa fursa hiyo kwa wanawake.
Miongoni mwa timu hizo ni Yanga Princess ambayo ni timu ya wanawake ya Yanga, inayonolewa na kocha Edna Lema 'Mourinho' ambaye alipewa jukumu la kuiongoza timu hiyo msimu huu akitokea Geita Gold inayoshiriki Ligi ya Championship.
Kwa Yanga, Edna Lema siko jina geni kwani tayari alishaiongoza Yanga Princess kabla ya kuachana nayo baada ya kumalizika kwa msimu wa 2022/2023 hivyo kiuhalisia amerejea nyumbani.
Matumaini yalikuwa makubwa kwa Wanayanga baada ya kurejea kwa Edna Lema, Wanayanga wengi wakiamini kwamba kocha huyo mzoefu wa mpira wa miguu kwa wanawake Tanzania, lakini hata hivyo mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo unaonekana kutoiendea vizuri Yanga Princess.
Timu hiyo hadi sasa inashika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi tisa ambazo imekusanya katika mechi saba, ikishinda mbili, kutoka sare tatu na kupoteza michezo miwili.
Kabla ya mechi ya jana ya Mashujaa Queens na Simba Queens, Yanga Princess ilikuwa imepitwa kwa tofauti ya pointi nane na JKT Queens na ilikuwa imetanguliwa kwa tofauti ya pointi saba na Simba Queens.
Msimamo huo unatoa matumaini finyu kwa Yanga Princess kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Wanawake msimu huu lakini kocha Lema anaamini bado nafasi wanayo.
"Msimu huu ni wa kujenga msingi bora wa timu lakini pamoja na hilo hatuwezi kukata tamaa kwa vile ni mapema hivi sasa kuamini kwamba mbio za ubingwa zimeisha kwa vile ndio kwanza tupo katika mzunguko wa kwanza.
"Ni kweli JKT Queens na Simba Queens wametuacha kwa idadi kubwa ya pointi lakini kuna uwezekano wa wao kuangusha pointi na sisi tukaziba pengo lililopo hivyo hatuwezi kukata tamaa hadi mwisho," alisema Edna Lema.

Yanga Princess imara inakuja
Kocha huyo anasema kuwa mashabiki wa Yanga wanapaswa kuwa na uvumilivu kwa vile uongozi kwa kushirikiana na benchi la ufundi wapo katika mchakato wa kujenga timu imara na tishio zaidi.
"Suala la kujenga timu ya ushindani na yenye ubora mkubwa sio jambo rahisi na linahitaji uvumilivu. Nashukuru uongozi wa Yanga umekuwa ukinipa sapoti kubwa mimi na benchi langu la ufundi katika kutimiza mipango ambayo umeweka.
"Tunaelekea pazuri na mashabiki wa Yanga nina imani furaha iko karibu inakuja. Ukiangalia usajili ambao tunaendelea kuufanya unaona mwanga kuwa mbele kutakuwa kuzuri," anasema Edna.
JKT Queens, Simba Queens sio nyepesi
Edna Lema anakiri kwamba timu za JKT Queens na Simba Queens zinamnyima hasa usingizi kwa vile zina vikosi vyenye wachezaji wazoefu.
"Simba Queens na JKT Queens zina wachezaji ambao wamekaa pamoja kwa muda mrefu na wana uzoefu hivyo sio rahisi kushindana nazo na ukizingatia zimekuwa na muendelezo wa kufanya vizuri.
"Kibarua kwetu ni kuhakikisha tunapunguza pengo la ubora lililopo baina yetu na wao na naamini ndani ya muda mfupi ujao, tutakaa juu yao," anasema Lema.
Wito kwa wachezaji
Edna Lema anawataka wachezaji wa Yanga Princess kuendelea kucheza kwa bidii zaidi ili waipe thamani na heshima timu yao.
"Yanga ni klabu kubwa na muda wote watu wanahitaji ifanye vizuri hivyo wachezaji wanapaswa kutambua hili. Kujituma kwao na kucheza vizuri ndio kunaweza kuifanya timu ifanye vizuri.
"Nina imani kubwa na wachezaji wangu na uwezo wa kufanya vizuri wanao. Muhimu ni kuendelea kuishi katika misingi sahihi kama wachezaji wa timu kubwa," alisema Lema.