MZEE WA FACT: Acha walipwe mamilioni, wastahili

Muktasari:
- Linapokuja suala la malipo mastaa wa kigeni wamekuwa wakivuna hela nyingi Ligi Kuu Bara kutoakana na thamani zao, japo kila mtu anakuwa na mtazamo wake kutokana na malipo ya mastaa hao.
Dar es Salaam. Hatimaye sintofahamu ya nyota wa mabingwa wa Ligi Kuu 2023/24, Yanga SC, Stephane Ki Aziz, imekwisha baada ya kutangazwa rasmi kwamba atabakia Jangwani kuendelezea alichokianza tangu 2022 alipokuja nchini.
Hofu ilikuwa kubwa kwa mashabiki wa Yanga hasa pale Rais wa klabu hiyo alipofanya mahojiano na kusema hawana uhakika kama nyota huyo raia wa Burkina Faso mwenye asili ya Ivory Coast, atakuwa nao msimu ujao.
Kabla kauli hiyo haijapoa, zikatoka taarifa kwamba klabu ya CR Belouzdad ya Algeria ilimtengea mshahara wa zaidi ya shilingi milioni 90 kwa mwezi ili ajiunge nao.
Kama taarifa zile zilizosambaa kupitia mitandao ya kijamii zilikuwa sahihi, maana yake Yanga watakuwa walimpa Ki ofa kubwa zaidi ya hiyo.
Na kama hivyo ndiivyo ilivyo, maana yake mchezaji huyo analipwa hela nyingi sana, zaidi ya ambavyo ungeweza kufikiria.
Ni kiasi hiki cha pesa ndicho kilichonisukuma kuandika hiki unachosoma.
Duniani kote kumekuwa na mijadala ya kiasi cha pesa ambacho wachezaji mpira wanalipwa na vilabu vyao.
Watu wengi wanasema wachezaji wanalipwa pesa ya kufuru na hawalingani na malipo hayo.
Kimsingi ni kwamba, acha walipwe kiasi hicho wanacholipwa kwa sababu wanastahili, kama nitakavyoeleza hapa chini.
1. WABURUDISHAJI
Tunaishi kwenye dunia ambayo kipato chako hutegemea thamani yako kwenye jamii.
Thamani ambayo wachezaji kama Chama, Dube, Fei Toto wanayo ni kubwa kwa sababu wanatuburudisha.
Kuna watu hutoa hoja kwamba madaktari ni watu muhimu zaidi kwenye jamii kwa sababu wanaokoa maisha yetu kwa hiyo wanastahili kulipwa zaidi ya wanavyolipwa.
Ni kweli kabisa kwa sababu kuokoa maisha ni jambo muhimu zaidi ya kuburudisha.
Lakini tofauti ni kwamba mchezaji kama Chama analeta furaha kwenye sura na nyoyo za mamilioni ya watu kwa wakati mmoja.
Endapo daktari mmoja angekuwa anaokoa maisha ya mamilioni ya watu kwa mara moja, jambo ambalo haliwezekani, basi angeweza kulipwa pesa nyingi sana.
2. WANAZALISHA
Wachezaji wanastahili kulipwa mamilioni kwa sababu wanazalisha wao wenyewe.
Wachezaji wenye mvuto huvipatia pesa nyingi vilabu vyao kwa kuvutia wadhamini na watazamaji kwenye mechi.
Pesa wanazozalisha ndizo wanazolipwa, na kimsingi wanalipwa kidogo zaidi ya wanavyozalisha.
Timu zenye wachezaji wasio na mvuto au wenye mvuto mdogo, mechi zao hazizalishi pesa nyingi na wao hawalipwi vya kutosha, zitatoka wapi hizo pesa?
Ndiyo maana soka la wanawake, watoto au hata wale madaktari niliowatolea mfano pale juu, hawalipwi sana kwa sababu hawazalishi pesa nyingi. hii ndiyo kanuni ya ubepari.
3. HAWANA MBADALA
Bila kuzivunjia heshima kazi nyingine muhimu duniani, wachezaji huwa hawana mbadala.
Kuna watu wengi sana kila sehemu ambao wanaweza kuwa madaktari, endapo watapatiwa elimu lakini siyo wachezaji.
Mchezaji kama Ki, anaweza asipatikane kwa zaidi ya miaka 20 ijayo, hata mkisomesha watoto wangapi kuwaandaa.
Hii huwafanya wachezaji kuwa bidhaa adimu, na kanuni za biashara zinasema bidhaa ikiwa adimu, thamani yake inapanda.
4. WAMEJITOA KAFARA
Ili kuwa mchezaji, unatakiwa ujitoe kafara ili ufanikishe ndoto zako.
Unatakiwa ubadilishe aina ya maisha yako, ikiwemo kuwaepuka marafiki zako uliokuwa nao.
Unatakiwa kuacha aina ya vyakula ulivyovizoea na kuvipenda.
Unatakiwa kuzoea kuishi maisha yenye presha kubwa huku ukiandamwa na vyombo vya habari.
Nani anataka maisha ya aina hii? Wao wanayaishi maisha haya ili kufanikisha ndoto zao, ndiyo maana hata malipo yao lazima yawe makubwa.
HITIMISHO
Siko hapa kumsifu GSM namna anavyomwaga pesa kuilinda Yanga SC, hapana.
Nachojaribu kufanya ni kufungua kichwa changu na vya wenzangu na mimi ili kuelewa ni namna gani ilivyo halali kwa wachezaji kulipwa mamilioni.
Tanzania tunatoka kwenye itikadi za kijamaa na kuingia kwenye ubepari.
Tunavyojiimarisha kwenye soka la kulipwa maana yake tunaimarisha ubepari kwenye mpira wetu.
Ubepari katika ubora wake unataka mtu alipwe kwa kadri anavyoingiza.
Kwa namna Ki anavyovutia biashara kwa Yanga, anastahili kulipwa alicholipwa ili kusaini mkataba mpya.