Massabo afuata nyayo za Nondo kuwania uongozi ACT-Wazalendo

Julius Massabo

Muktasari:

  • Ngome ya vijana ya ACT-Wazalendo inaongozwa na Abdul Nondo anayemaliza muhula wake wa miaka minne.

Unguja. Naibu Msemaji wa Sekta ya Viwanda na Biashara, Baraza Kivuli la Chama cha ACT-Wazalendo, Julius Massabo ametangaza nia ya kuwania nafasi ya uenyekiti wa ngome ya vijana Taifa.

Kwa sasa mwenyekiti wa ngome hiyo ni Abdul Nondo, ambaye ameshatangaza kuwania tena nafasi hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari makao makuu ya chama hicho Vuga, Zanzibar leo Januari 6, 2024, Massabo amesema dhamira yake inasukumwa na uzalendo kwa nchi yake na mapenzi makubwa ya chama chake.

“Leo Januari 6, 2024 nimewaita kutangaza dhamira yangu inayosukumwa na uzalendo kwa nchi yangu na mapenzi makubwa kwa chama changu, dhamira ambayo inanisukuma kuwania nafasi ya uenyekiti wa Ngome ya Vijana Taifa,” amesema na kuongeza:

“Kwa kuitazama picha kubwa ya nchi yetu, kwa kuangalia mwelekeo wa chama chetu, imani kubwa ya Watanzania kwa chama chetu na kwa kuongozwa kwa misingi ya kizalendo, leo naomba niutangazie umma wa Watanzania, wanachama wenzangu na vijana wa chama chetu kwamba nitagombea nafasi hiyo.”

Massabo amesema atachukua fomu kwenye ofisi za makao makuu ya chama hicho Magomeni jijini Da er Salaam Februari 14, 2024 ambayo ni siku atakayotaja vipaumbele na matamanio yake kwenye ngome hiyo.

“Nawaomba wanachama waniunge mkono na kuniombea kwa Mwenyezi Mungu ili kwa rehema zake aniwezeshe kuongoza ngome yetu ya vijana kwa moyo wangu wote na kuhakikisha vijana wanakuwa Taifa la leo na kesho,” amesema Massabo.

Uchaguzi huo unatarajiwa kufanyika Februari 29, 2024, pia chama hicho kitafanya uchaguzi wa Ngome ya Wazee Machi mosi na Ngome ya Wanawake, Machi 2, 2024.

Baada ya chaguzi wa ngome hizo, uchaguzi wa viongozi wakuu wa kitaifa wa chama hicho akiwemo mwenyekiti na makamu wake utafanyika Machi 5, 2024.