SMZ yaweka mkazo kuimarisha Tehama

Muktasari:

  • Serikali imeweka kipaumbele maalumu katika kuimarisha huduma sahihi za teknolojia ya habari na mawasiliano (Tehama) kwa lengo la kuwajengea uwezo watu wake, bodi hii itakua na jukumu kubwa la kusimamia sera za ICT, pamoja na kusimamia miundombinu, bajeti na matumizi ya shirika katika kuhakikisha malengo ya Serikali yanafikiwa

Unguja. Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Zanzibar, Dk Khalid Salum Mohamed amezindua bodi mpya ya Shirika la Mawasiliano visiwani humo huku akitaka kuimarisha sekta hiyo na hivyo kwenda sambamba na mabadiliko ya kiulimwengu.

Dk Mohamed ametoa wito huo leo Novemba 18, 2023 katika hafla maalum ya uzinduzi wa bodi hiyo iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Wizara ya Ujenzi Kisauni, huku akibainisha mipango ya Serikali katika kuimarisha huduma za teknolojia.

“Serikali imeweka kipaumbele maalumu katika kuimarisha huduma sahihi za teknolojia ya habari na mawasiliano (Tehama) kwa lengo la kuwajengea uwezo watu wake, bodi hii itakua na jukumu kubwa la kusimamia sera za ICT, pamoja na kusimamia miundombinu, bajeti na matumizi ya shirika katika kuhakikisha malengo ya Serikali yanafikiwa," amesema.

Aidha, Waziri huyo amesema Serikali imeona ipo haja ya kuanzisha shirika hilo ili kutoa nguvu zaidi liweze kujiendesha kibiashara na kuongeza faida.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa bodi hiyo  Dk Mahmoud Abdulwahab Alawi amemshkuru Rais wa Zanzibar na kwa kumuamini na ameahidi kuwa atahakikisha shirika hilo linafikia malengo na madhumuni ya kuanzishwa kwake, katika ukuaji na kujiendesha kwa kujitegemea.

Pia, Dk Mahmoud amewaomba wajumbe wa bodi hiyo pamoja na wafanyakazi kutoa ushirikiano wao hasa katika utendaji wa kazi zao za kila siku ili kufikia lengo la kutoa huduma bora za mawasiliano.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Zanzibar, Shukuru Awadhi Suleiman ametoa pongezi zake kwa Serikali na uongozi wa Wizara ya Ujenzi kwa kuwateua wajumbe wa bodi.

Amesema kuteuliwa kwa bodi hiyo kutasaidia kutoa msukumo katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya shirika hilo ambayo kwa sasa ipo katika mchakato wa utekelezaji.

Pamoja na Mwenyekiti, wajumbe wa bodi hiyo ni Said Seif Said, Mohamed Khamis Mussa, Abdulrahaman Ali Hassan, John Mahundi, Chai Ali Mohamed na Shukuru Awadhi Suleimani ambao wameteuliwa kwa mujibu wa sheria nambari nne  ya mwaka 2023.