Wadau waeleza wanachotamani kifanyike Wizara ya Uwekezaji Zanzibar

Muktasari:
- Shariff Ali Shariff alikuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (Zipa) kwa kipindi cha miaka 3 tangu Rais Mwinyi aingie madarakani.
Wakizungumza na Mwananchi Digital kwa nyakati tofauti, baada ya uteuzi huo leo Februari 21, 2024, walisema Shariff amepelekwa kwenye wizara ambayo atakwenda kuleta mabadiliko kwa sababu ndicho kitu alichokuwa akikifanyia kazi.
Taarifa iliyotolewa leo Jumatano Februari 21, 2024 kwa vyombo vya habari na Katibu Mkuu Kiongozi, Zena Said imesema uteuzi huo unaanza leo na ataapishwa kesho Ikulu Zanzibar.
Kabla ya kuteuliwa kuwa Waziri, Februari 12 mwaka huu, Rais Mwinyi alimteua kuwa mwakilishi wa Baraza la Wawakilishi, hiyo ni kwa mujibu wa uwezo wa Rais aliopewa chini ya kifungu namba 66 cha katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 na anapewa nafasi 10 za kumteua mtu yeyote anayeona anafaa kuwa mjumbe wa baraza hilo.
Shariff alikuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (Zipa) kwa kipindi cha miaka 3 tangu Rais Mwinyi aingie madarakani.
Mchambuzi wa masuala ya uchumi, Profesa Haji Semboja amesema kuwa Wizara ya Uwekezaji ni mtambuka inayohusisha sekta zote hivyo inahitaji sera zinaendana na nyingine ili kufanikisha kinachokusudiwa.
“Mambo anayopaswa Shariff kama waziri wa wizara hiyo ni Serikali kutunga au kuwa na sera na sheria za kisasa zinazoendana na mahitaji ya maendeleo visiwani.”
“Pia kuwahitaji wengine kuwa na sera ambazo zinazoendana na ya kwake kwa sababu huwezi kuweka sera ya uwekezaji nzuri wakati zilizopo kwa wengine zinakuwa zimepitwa na wakati.
Amesema katika kila analofanya ahakikishe kinasapoti sera kubwa ya nchi ya uchumi wa buluu. “Unajua kisiwa kidogo huwezi kuzungumza uwekezaji kwenye kilimo, viwanda. Uwekezaji mkubwa ni kwenye huduma za kisasa ambapo sehemu kubwa ni za utalii, biashara kuu ambazo zipo visiwani humo, badala ya Watanzania kufikiria kwenda kufanya manunuzi Dubai, waanze kufikiria kwenda Zanzibar.”
“Muhimu pia kuongeza nguvu kwenye uwekezaji utakaosaidia tasnia nzima ya masuala ya bandari, meli na kwa ujumla masuala yanayohusiana na bahari na bandari zake,”amesema Profesa Semboja ambaye ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu Cha Taifa Zanzibar (Suza).
Kuhusu matumaini ya kufanya vizuri kutokana na alikotoka Profesa Semboja amesema alikuwa kwenye taasisi iliyokuwa na jukumu la kusaidia kutangaza uwekezaji ndani wa nchi, hivyo kupelekwa kwenye wizara ya uwekezaji ni kama wasemavyo Waswahili unalolijua njoo ulieleze hadharani kwa kulitenda.
“Mimi binafsi nashukuru kuteuliwa kwenye wizara hii kwa kuwa anajua cha kutenda, akiwa Zipa alikuwa anashindwa wakati mwingine kukosoa kwani alikuwa anapewa maelekezo, sasa zile kasoro alizokuwa akiziona amepata fursa ya kuzirekebisha.”
“Binafsi na wengi huwa tunatamani waziri anayehusika na wizara fulani awe anatoka chini hasa kwenye nchi za kimasikini zinazoendelea kama ya kwetu, huyu mfano mzuri nashukuru Rais kwa kufanya uteuzi wa kuzingatia taaluma, kuliko kumteua mtu kutoka katika sekta nyingine na kumuweka akatekeleze majukumu asiyoyajua kabisa kitakachotokea atavurugana sana na watendaji,”amesema Profesa Semboja.
Akilizungumzia hilo, mchambuzi wa siasa Abdulla Shaame amesema, “alipokuwa (Zipa) alikuwa akisimamia sekta wakati mwingine lazima apewe miongozo kutoka wizarani, sasa anakwenda kuyasimamia mwenyewe kwa hiyo atatoa dira nzuri ya mwelekeo wa Taifa hili.
Amesema kwa sasa sekta ya uwekezaji inaangaliwa sana na Serikali kwani kumekuwa na mwamko mkubwa wa wazawa na wageni kutaka kuwekeza nchini
Mchambuzi mwingine wa siasa, Ali Said Ussi amesema Shariff ameingia kwenye nafasi hiyo wakati ambapo tayari sheria ya uwekezaji imeshatungwa, hivyo itamuongezea mwanya mpana kurahisisha kazi zake.
Amesema Shariff alipewa nafasi kubwa kuchukua nafasi hiyo kutokana na uzoefu wake katika sekta uwekezaji ambapo ameonekana kufanya kwa ufanisi na kuleta tija.
Sheria ya uwekezaji ya mwaka 2023 imepitishwa na baraza la wawakilishi mwaka jana na Februari mwaka huu Rais Mwinyi aliisaini tayari kuanza utekelezaji wake.
Pamoja na mambo mengine sheria hiyo inatoa fursa kwa wawekezaji wa ndani lakini kuwabana wawekezaji ambao wameshikilia ardhi kwa muda mrefu bila kuiendeleza.
Awali, wizara hiyo ilikuwa inaongozwa na Mudrick Ramadhan Soraga ambaye Januari 26, 2024 Rais Mwinyi alimteua kuwa Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale, baada ya aliyekuwa ameshikilia nafasi hiyo, Simai Muhamed Said kujiuzulu.
Hivi Karibuni wakati wa uzinduzi wa miradi mbalimbali ikiwa ni kusherehekea miaka 60 ya Mapinduzi, Rais Mwinyi aliipongeza Zipa iliyokuwa ikiongozwa na Shariff kwamba inafanya kazi nzuri katika masuala ya uwekezaji.
Mamlaka hiyo kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia mwaka 2020 hadi Novemba 30, 2023, imesajili miradi 296 yenye mtaji wa Dola za Marekani 4.5 bilioni sawa na Sh11.3 trilioni.
Miradi hiyo inatarajiwa kuzalisha ajira zaidi ya 17,479 kati ya hiyo inayohusisha uwekezaji katika sekta ya hoteli ni 112, biashara ya majengo 56, viwanda 36 na mingine ni ya sekta nyinginezo.
Katika kipindi chake Shariff, vimewekezwa visiwa vidogo 16 kati ya 20 vilivyotangazwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuvikodisha, vimepata wawekezaji vikiwa na thamani ya Dola za Marekani 384.5 milioni sawa na Sh970 bilioni.