Mahakama kuamua DC Chemba anayedai talaka

Wednesday September 18 2019

 

By Tausi Ally, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Mahakama ya Mwanzo ya Ukonga Dar es Salaam leo Jumatano Septemba 18, 2019 itatoa hukumu ya kesi ya madai ya talaka namba 181/2019 iliyofunguliwa na Mkuu wa Wilaya ya Chemba (DC) mkoani Dodoma, Simon Odunga dhidi ya mke wake wa ndoa ya kanisani Medilina Mbuwuli.

Hukumu hiyo itatolewa na Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo, Christina Luguru.

Hatua hiyo ilifikiwa mahakamani hapo baada ya Luguru kusikiliza ushahidi uliotolewa na mashahidi wa upande zote mbili na kufunga ushahidi wao.

Odunga na Mbuwuli wanadaiwa kufunga ndoa ya Kikristu katika Kanisa la Sabato Sinza Dar es Salaam mwaka 2000 na kupata cheti cha ndoa  A no 00140917.

Katika ndoa yao hiyo, mdai na mdaiwa wanadaiwa hawajawahi kuchuma mali yoyote na hawana mgogoro na hilo. Hata hivyo, Mbuwuli aliieleza mahakama hiyo kwamba Odunga amechuma mali na kahaba wa nje ya ndoa.

Advertisement

Mbuwuli anadai mumewe huyo hajawahi kutoa matunzo ya mtoto wao wa kike mwenye umri wa miaka 18 tangu akiwa chekechea hadi sasa yupo kidato cha sita.

Hata hivyo, Mbuwuli  alieleza licha ya mumewe kutotoa matunzo hayo, hayupo tayari kupewa talaka kwa sababu ndoa yao ni takatifu ya kanisani na kwamba bado anampenda mume wake huku akidai anajua hizo ni changamoto tu zimempitia.

Alidai katika ndoa yao Odunga amekuwa akikaa kwake akiwa hana fedha na akipata fedha anaishi kwa mwanamke huyo wa nje ya ndoa na kwamba ana mashahidi wa kutosha.

Alisema mumewe ana tabia ya kwenda kwake kila Julai muda ambao hata serikali haina fedha.

Kuhusu mtoto Mbuwuli aliomba mahakama iamuru Odunga amlipe gharama alizotumia kumtunza mtoto wao huyo wa kike mwenye umri wa miaka 18 tangu akiwa chekechea hadi alipo sasa kidato cha sita na kutoa risiti ambazo zinaonyesha gharama za ada alizotumia anazo.

Pia ameiomba mahakama iamuru Odunga amuhudumie yeye kama mke  na mtoto wao.

Kwa upande wa Odunga ambaye ni madai katika kesi hiyo yeye anaomba mahakama iivunje ndoa hiyo kwa sababu hapati haki ya ndoa.

Alidai  Mbuwuli ni mke wake wa ndoa ya Kikristu na kwamba walitengana rasmi mwaka 2003.

Alidai wana mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 18 sasa ambaye anaishi na mama yake na kwamba hakuna mali yoyote waliyochuma.

Advertisement