Profesa Lipumba wa jana, si wa leo

Dar es Salaam. Unaweza kusema kauli za hivi karibuni za mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba ni tofauti na alizokuwa akizitoa miaka miwili iliyopita baada ya kurejea katika chama hicho.

Katika mikutano yake miwili na waandishi wa habari aliyoiitisha ndani ya wiki moja iliyopita kuzungumzia sakata la uchaguzi wa serikali za mitaa, Profesa Lipumba ameonyesha kutoridhishwa na mwenendo wa masuala kadhaa ya kitaifa na kuiikosoa vikali Serikali kwa kusababisha maisha ya wananchi wa kawaida kuwa magumu na kuminya demokrasia nchini.

Profesa Lipumba, ambaye amepata kugombea urais katika uchaguzi mkuu kwa tiketi ya CUF mwaka 1995, 2000, 2005 na 2010, ameenda mbali zaidi katika ukosoaji wake hata kugusa mamlaka za juu.

“Kwa sisi ambao tulishakuwa wakubwa wakati wa kupigania uhuru wa taifa hili na kushiriki vuguvugu hilo tutakumbuka kwamba katika historia ya nchi hii hakujawahi kutokea uchaguzi wa kihuni kama huu wa serikali za mitaa,” alisema Profesa Lipumba wakati wa mkutano wake na wanahabari uliofanyika makao makuu ya chama hicho, Buguruni, Novemba 6.

“Kilichotokea ni utumiaji mbaya wa madaraka na fedha za umma kwa maslahi ya chama kimoja. Huu ni ufisadi na wanaouendekeza ufisadi huu hawawezi kudai kupambana nao kwenye maeneo mengine.”

Profesa Lipumba amefikia hadi kutaka uchunguzi ufanyike ndani ya Serikali akidai uvurugwaji wa uchaguzi wa serikali za mitaa ni dalili moja tu ya uwepo mkubwa wa ufisadi. “Unapolazimisha kutumia mbinu za kifisadi ili wagombea wako wakwepe ushindani kwenye uchaguzi, ni wazi kwamba utatumia mbinu hizo hizo za kifisadi kufanikisha mambo mengine...”

Wakati wa kutangaza kujitoa kwa CUF kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa, Profesa Lipumba alidai kwamba inaonekana sasa kuna mkakati wa wazi wa kuua ushindani wa kisiasa nchini.

Alisema “na bila shaka, na sijamsikia Rais akilikemea jambo hili, inaonekana kwamba katika kile kikao cha Rais na watendaji kata ndiyo mpango ulisukwa pale. Na ndiyo maana unaona watendaji huko chini wana kiburi sana hata wanapopewa maagizo na waziri hawayatekelezi.”

Kujitoa kwenye uchaguzi

Hatua yenyewe ya kususia uchaguzi imewashangaza wengi ukizingatia ukweli kwamba CUF imekuwa ikishiriki kwenye chaguzi ndogo kadhaa za udiwani na ubunge, chaguzi ambazo zilikumbwa na kasoro nyingi zilizosababisha vyama vyote vikubwa vya upinzani kususia.

Ukiacha ushiriki wake kwenye chaguzi hizi, CUF pia imekuwa na uhuru wa kiwango fulani wa kufanya shughuli zake ukilinganisha na vyama vingine vya upinzani, hoja inayopingwa vikali na msemaji wa chama hicho, Abdul Kambaya anayesema kwamba, kama ilivyo kwa upinzani kwa ujumla, CUF haijaweza kukwepa kuonja joto ya jiwe.

Hata hivyo, inajulikana kwamba CUF imefanya baadhi ya mikutano ya hadhara, imewahi kufanya ziara hasa mwaka 2016 katika mikoa ya Kusini na kuzindua matawi huku vyama vingine vya upinzani vikizuiwa. Na hivi karibuni ilifanya ziara maeneo mbalimbali nchini.

Profesa Lipumba na timu yake pia walipokea ruzuku kwa Msajili wa Vyama vya Siasa wakati ambao kambi iliyokuwa ikiongozwa na katibu mkuu wake, Seif Sharif Hamad ilinyimwa.

Haya ni baadhi tu ya masuala yanayomfanya mhadhiri mstaafu wa historia Profesa Abdul Sharif kusema kwamba hashangai kuona CUF ikichukua hatua inazochukua sasa kwani anasema hiyo ni njia pekee chama hicho kinadhani kinaweza kuwarejesha wanachama na wafuasi wake wa zamani.

“CUF wanafahamu kwamba hakuna mfuasi wa kweli wa upinzani atamuunga mkono mwanasiasa anayeonekana kuwa ni kibaraka wa Serikali au chama tawala. Ili iwapate, CUF ni lazima ichukue msimamo thabiti dhidi ya serikali,” anasema Profesa Sharif.

“Kuna ile taswira kwamba Lipumba ni kibaraka wa Serikali na inaonekana kama amepania kuwahakikishia watu kwamba hiyo si kweli. Baada ya kuona wagombea wa chama chake wameenguliwa kwenye kinyang’anyiro cha uchaguzi, Lipumba hakuona maana tena ya kukaa kimya kwani kunyamaza kungeathiri juhudi zake za kujenga chama,” anaongeza Profesa Sharif.

Kambaya, kwa upande wake, anakanusha madai ya Profesa Lipumba kutumika kama kibaraka wa Serikali kuivuruga CUF akisema kwamba mgogoro wa chama hicho ulikuwa ni wa kikatiba zaidi na Serikali haikuhusika hata kidogo. “Hivi kwa unavyomjua Profesa Lipumba ana njaa sana mpaka awe tayari kutumiwa na Serikali au kufanikisha mipango yake? Huo ni utoto,” anasema Kambaya.

Ujenzi wa chama

SOMA ZAIDI

Hoja ya ujenzi wa chama iliyoibuliwa na Profesa Sharif ndiyo hoja ambayo hata Profesa Lipumba mwenyewe amedokezea katika matamko yake ya hivi karibuni.

Katika moja ya mikutano yake na wanahabari, Profesa Lipumba aliwaasa wanachama wa chama hicho kwamba sasa si muda wa kukata tamaa, akiahidi kuchukua hatua madhubuti za kujenga chama hata kama mazingira ya kufanya hivyo ni magumu.

“Ni lazima tujenge chama. Utakapojenga chama kikawa imara, hiyo inakusaidia kufanya maagizo yako kutekelezwa unapoyatoa. Kwa sababu hii basi, viongozi wote wa chama watashiriki katika mpango wa kujenga chama na kuzunguka nchi nzima. Tutakwenda kuonana na wananchi na kuwaeleza hali halisi ya nchi, kiuchumi na kisiasa.”

Dk Paul Luisulie, mchambuzi wa masuala ya siasa kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) anasema matamko ya hivi karibuni ya Profesa Lipumba yanaashiria kwamba msomi huyo ameanza kuangalia masuala katika uhalisia wake. Tofauti na nadharia ya Profesa Sharif kwamba Profesa Lipumba “ametelekezwa,” Dk Luisulie anadhani kwamba hatua ya mwenyekiti huyo wa CUF ilikuwa ni ya kutegemewa baada ya mzozo ndani ya chama hicho kumalizika.

“Mapambano sasa si baina ya Lipumba na Maalim Seif bali CUF na CCM. CUF imetambua kwamba kama itaendelea na mwenendo wake wa miaka miwili mitatu ya hivi karibuni na kujifanya rafiki na serikali itapoteza ufuasi na kufa. Ilipaswa wachague adui, kitu ambacho ni cha kawaida kwenye siasa,” anasema Dk Luisulie.

Kambaya anasema kwamba kuikosoa Serikali si kitu kigeni kwa chama hicho, akisema kwamba huo ni utaratibu uliokita mizizi katika utamaduni wa CUF kama taasisi.

Akizungumzia pongezi za hivi karibuni kutoka kwa baadhi ya wananchi kwa Profesa Lipumba, Kambaya anasema:

“Nafikiri ni suala la uelewa tu. Kama umekuwa ukifuatilia kwa karibu utagundua kwamba kumekuwa na juhudi kubwa za kumchafua Profesa Lipumba kwa kutunga kila aina ya ‘propaganda.’ Watu wamekuwa wakiziamini ‘propaganda’ hizi na hii ni bahati mbaya sana kwamba uwezo wa kufikiri wa hao wanaoziamini ndiyo umeishia hapo,” anasema Kambaya.

SOMA ZAIDI