Maajabu ya waah ya Diamond YouTube

Muktasari:
- Ikiwa na miezi minane tu tangu iachiwe, video ya wimbo wa ‘Waah’ wa Diamond Platnumz aliomshirikisha mkongwe wa muziki kutoka DRC Congo, Koffi Olomide imetimiza jumla ya watazamaji milioni 80 kwenye mtandao wa YouTube.
Dar es Salaam. Ikiwa na miezi minane tu tangu iachiwe, video ya wimbo wa ‘Waah’ wa Diamond Platnumz aliomshirikisha mkongwe wa muziki kutoka DRC Congo, Koffi Olomide imetimiza jumla ya watazamaji milioni 80 kwenye mtandao wa YouTube.
Hiyo ni rekodi kwa Diamond mwenyewe na tasnia ya muziki kwa ujumla kwani hakuna video yeyote ya muziki nchini Tanzania iliyowahi kukimbia kwa kasi namna hiyo.
Video hiyo iliachiwa Novemba 30 mwaka jana, na kulingana na spidi yake ya 5G, Mwananchi inafanya uchambuzi kuangalia ni kwa nini ‘Waah’ imekuwa ni wimbo wenye mafanikio makubwa mno ‘, maana yake kiuchumi.
REKODI ZA WAAH
Mbali na rekodi mpya iliyowekwa mwezi huu, ya kufikisha watazamaji milioni 80 ndani ya miezi 8 tangu kuachiwa kwake, na kuifanya kuwa video ya muziki nambari moja nchini kufikia idadi hiyo ya watazamaji kwa muda mfupi, pia Waah inashikilia rekodi nyingine nyingi.
Soma zaidi: Alikiba, Diamond, Harmonize kimeumana huko!
Moja ya rekodi ni kuwa video ya muziki Afrika iliyofikisha watazamaji milioni moja kwenye mtandao wa Youtube kwa muda mfupi zaidi.
‘Waah’ ilifikisha idadi hiyo ya watazamaji ndani ya saa nane na kuvunja rekodi iliyokuwa inashikiliwa na msanii Davido wa Nigeria kupitia wimbo wake wa ‘FEM’ ambao ulifikisha watazamaji milioni moja ndani ya saa tisa.
Soma zaidi:Kauli ya Diamond baada ya kukosa tuzo BET
Pia, ‘Waah’ inashikilia namba tatu katika orodha ya video za Diamond zilizotazamwa sana Youtube. Ya kwanza ikiwa ni ‘Yope Remix’ aliyoimba na Innoss B, ina watazamaji milioni 160, na nafasi ya pili ikishikiliwa na ‘Inama’ ambayo alimshirikisha Fally Ipupa ikiwa na watazamaji milioni 94.
Hata hivyo, kama ‘Waah’ itaendelea kwenda kwa kasi iliyoanza nayo, basi ni wazi itakamata nambari moja kabla ya kumalizika kwa mwezi Machi mwakani.
KWA NINI ‘WAAH’
Kuna mambo matatu makubwa yanayoifanya ‘Waah’ kuwa baba lao. Kwanza, ni ukubwa wa Koffi Olomide katika tasnia ya muziki. Koffi ni msanii mkubwa Barani Afrika ambaye amedumu kwenye muziki kwa zaidi ya miaka 30 na kwa kipindi chote hicho amefanikiwa kutengeneza mashabiki wa vizazi viwili tofauti, wa kisasa au vijana na wahenga au wakongwe. Kwa maana hiyo, kufanya kazi pamoja na Koffi ni kutengeneza bidhaa ambayo tayari ina walaji wanaoisubiri.
Pili ni ‘gap’ iliyopo kati ya wimbo wa mwisho kuachiwa na Diamond na ‘Waah’. Wimbo wa mwisho rasmi kuachiwa na Diamond ilikuwa ni ‘Jeje’, iliyoachiwa miezi 10 kabla ya kuachia kwa Waah. Kwa hiyo ni wazi kwamba wakati Diamond anaachia Waah mashabiki wake walikuwa na kiu ya kumsikia.
Baada ya kugundua hilo, Diamond na timu yake wakafanya jambo lingine ambalo ndilo la tatu, wakafanya matangazo kwa ukubwa.
Matangazo yalikuwa ni makubwa sana kiasi kwamba kila mtu alikuwa anafahamu Diamond anakaribia kutoa wimbo na Koffi kabla hata wawili hao hawajaingia studio. Na sio tu wimbo, walivyokuwa wanautangaza walikuwa wanatoa picha ya kwamba utakuwa ni wimbo mkubwa.
Timu ya matangazo ya Diamond ilikuwa inaujulisha umma kila hatua waliyofikia kwenye mradi wao huo; yaani tangu Koffi anatua uwanja wa ndege, anafika hotelini, anaingia studio, wanarekodi video, kila kitu. Bila kusahau matangazo ya mitandao na kwenye vyombo vingine vya habari na matokeo yake ndiyo haya, Waah inafanya maajabu.
INAMAANISHA NINI KIUCHUMI
Kwa mujibu wa Diamond mwenyewe amebainisha kuwa wimbo huo umemuingizia kiasi cha Sh89 milioni ulipofikia watazamaji 32 milioni. Aliyasema hayo Aprili mwaka huu kupitia ukurasa wake wa Instagram wakati akitoa somo la faida za watazamaji wa Youtube kwa msanii.
Wakati kwa hesabu tulizozifanya kupitia kikotoo cha mtandao influencer marketing hub, video hiyo inakadiriwa kukusanya jumla ya dola za kimarekani 148,227 mpaka sasa, sawa na Sh343.7 milioni.