Mfumo benki wafeli, wanafunzi wachota mabilioni

Benki ya Biashara ya Ethiopia

Muktasari:

  • Kiasi kilichochotwa kutokana na hitilafu iliyosababisha wateja wa benki hiyo kuwa na uwezo wa kutoa fedha bila kikomo kupitia ATM, ni zaidi ya Dola 40 milioni za Marekani (Sh102.08bilioni) zimechukuliwa.

Dar es Salaam. Benki ya Biashara ya Ethiopia (CBE) inayomilikiwa na Serikali inaendelea kupambana kurejesha mabilioni fedha yaliyochotwa na wateja wake mwishoni mwa wiki, wengi wao wakiwa wanafunzi, baada ya kutokea kwa hitilafu katika mifumo yake.

Kiasi kilichochotwa kutokana na hitilafu iliyosababisha wateja wa benki hiyo kuwa na uwezo wa kutoa fedha bila kikomo kupitia ATM, ni zaidi ya Dola 40 milioni za Marekani (Sh102.08bilioni) zimechukuliwa.

Kiasi hicho cha fedha ukikipanga kwa noti za Sh10,000 zinaweza kwenda urefu wa kilometa 1,428 ambayo ni safari ya kutoka Dar es Salaam hadi Bukoba, mkoani Kagera.

Duru kutoka nchini Ethiopia zinadai kuwa hitilafu hiyo ilitokea mwishoni mwa wiki iliyopita na kundi ambalo linatajwa kuchota fedha nyingi zaidi ni wanafunzi wa vyuo mbalimbali nchini humo.

Rais wa Benki hiyo, Abie Sano ameeleza kuwa kwenye ATM za vyuo mbali kulikuwa na foleni kubwa kuliko kawaida za vijana waliokuwa wakitoa pesa na wengine walihamishia fedha hizo katika benki nyingine za kibiashara.

Inaelezwa kuwa wanafunzi walikuwa wakitumiana ujumbe juu ya mchongo huo na foleni katika ATM zilidumu kwa saa kadhaa siku ya Jumamosi, mpaka pale Polisi nchini humo walipoingilia kati kuzuia watu kutumia huduma za ATM na baadaye huduma za benki zikasitishwa nchi nzima kwa saa kadhaa.

Kufuatia hatua hiyo, vyuo vikuu kadhaa vimewataka wanafunzi kurudisha fedha ambazo si zao, huku ikiripotiwa kuwa atakayerejesha fedha hizo kwa hiari hatashtakiwa kwa makosa ya jinai, suala ambalo linadaiwa huenda lisiwe rahisi.

Benki Kuu ya Ethiopia, ambayo inasimamia sekta yake ya fedha imesema changamoto hiyo ilitokana na ukaguzi wa usalama wa mfumo wa fedha na si tukio la uhalifu wa kimtandao ambao unatishia usalama wa benki, wateja wake na mfumo mzima wa kifedha.Kwa masaada wa mashirika mbalimbali ya habari