Mtoto wa Trump atua Tanzania, aahidi kuwa balozi

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mohamed Mchengerwa (kushoto) akizungumza na Trump Junior ambaye ni mtoto wa aliyekuwa Rais wa Marekani, Donald Trump.

Muktasari:

  • Donald Trump Junior amefika nchini kutembelea vivutio ya utalii na hasa katika eneo linalosimamiwa na Mamlaka ya Usimamizi Wanyamapori (TAWA) la Lake Natron wilayani Longido mkoa wa Arusha. Huku akiahidi kuwa balozi mzuri.

Arusha. Donald Trump Jr ambaye ni mtoto mkubwa wa kiume wa Rais Mstaafu wa Marekani, Donald Trump, amefika nchini kutembelea maeneo mbalimbali huku kueleza kuvutiwa na vivutio vya utalii vilivyopo nchini.

 Taarifa zinasema Trump Jr maeneo aliyovutiwa nayo ni eneo linalosimamiwa na Mamlaka ya Usimamizi Wanyamapori (TAWA) la Lake Natron wilayani Longido mkoa wa Arusha, Hifadhi ya Ngorongoro lakini pia na maeneo mengine ya utalii.

Akiwa nchini, leo, Juni 7, 2023 Trump Junior amefanya mazungumzo na Waziri wa Maliasili na Utalii, Mohamed Mchengerwa na kuelezwa fursa za utalii zilizopo nchini.

Waziri Mchengerwa alimuomba mtoto huyo wa Trump kuendelea kuwa balozi wa Utalii wa Tanzania kwani imejaliwa kuwa na vivutio vingi vya utalii ambavyo havipatikani sehemu nyingine.

Waziri Mchengerwa alimweleza mgeni huyo mashuhuri mwelekeo wa sekta ya utalii na fursa mbalimbali za uwekezaji.

"Tanzania tuna mwelekeo mzuri katika kukuza utalii na kuvutia watalii zaidi, kwa kuboreshwa huduma za utalii ikiwepo miundombinu ya hifadhini," amesema.

Kwa upande wake Trump Junior ambaye pia ni mfanyabiashara mkubwa nchini Marekani na Makamu wa Rais Mwandamizi katika kampuni kubwa ya baba yake, huku akitajwa kuwa na utajiri unaofikia Dola Milioni 350 (zaidi ya Shilingi Bilioni 750), ameeleza kufurahishwa na Tanzania.

Trump ameahidi kutembelea maeneo mbalimbali zaidi ikiwemo eneo la Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro na hifadhi nyingine.