Cleopa Msuya atamani mrithi wa Rais John Magufuli avae viatu vyake

Muktasari:
- Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Magufuli amefariki dunia Machi 17, 2021 katika Hospitali ya Mzena jijini Dar es Salaam ambako alikuwa amelazwa akipatiwa matibabu.
Moshi. Waziri mkuu mstaafu ambaye alipata pia kuwa makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Cleopa Msuya amesema kifo cha Rais John Magufuli ni mshituko mkubwa kwa Taifa, lakini akataka Watanzania wajipe moyo ili kupata kiongozi atakayevaa viatu vyake.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Magufuli amefariki dunia Machi 17, 2021 katika Hospitali ya Mzena jijini Dar es Salaam ambako alikuwa amelazwa akipatiwa matibabu.
Kwa mujibu wa katiba Ibara ya 37(5) inasema endapo kiti cha Rais kitakuwa wazi kutokana na Rais kufariki, makamu wa Rais ambaye sasa ni Samia Suluhu ataapishwa na atakuwa Rais kwa muda wa miaka 5 iliyobaki wa kipindi cha urais.
Akizungumza kwa simu leo Machi 18, 2021 Mzee Msuya ambaye aliwahi kuwa Mbunge wa Mwanga na kushika nyadhifa kadhaa ndani ya Serikali ya awamu ya kwanza na ya pili, alisema taarifa za msiba zimekuja kwa mshtuko mkubwa.
“Ni jambo ambalo limekuja kama mshtuko mkubwa kwa Taifa maana alianza vizuri kipindi chake cha kwanza na matumaini ya watu wengi ilikuwa kwamba ataendelea na msukumo ule ule ambao watu walikuwa na matumaini makubwa.”
Mzee Msuya aliongeza kusema kuwa, “Watanzania walikuwa na matumaini ya manufaa ya nchi na watu yatakuwa makubwa. Sasa mwenyezi Mungu amemuita tunachoweza kufanya ni kuwapa pole wana familia na jamii yote ya Watanzania.”
“Lakini sasa tujipe moyo na tuombe taratibu za kikatiba za kutafuta kiongozi mwingine atakayevaa viatu vyake. Tumpate mtu atakayeweza kuyashika yale yote mazuri aliyoyafanya na nia aliyokuwa nayo ya maendele nayo,” alisisitiza.