Dk Gwajima: Sijutii kujifukiza kujikinga na corona

Muktasari:

  • Waziri wa Afya amesema kuwa hawezi kujutia uamuzi wake wa kutumia tiba za asili kwajili ya kupambana na ugonjwa wa corona kabla ya kuwepo kwa chanjo ya ugonjwa huo.

Musoma.  Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Dorothy Gwajima amesema, hatajuii kitendo cha kujifukiza ikiwa ni sehemu ya kujikinga na maambukizi ya ugonjwa wa corona.

Dk Gwajima ameyasema hayo leo Agosti 16 mjini hapa, akiongeza kuwa hajutii pia kutumia dawa za asili kama ambavyo alionekana siku za nyuma akifanya hivyo kama njia mojwapo ya kujikimga na ugonjwa huo.

Amesema kuwa aliamua kutumia njia hizo za asili kutokana na ukweli kuwa tiba za asili zimethibitshwa na mamlaka husika na zinafanyika kwa mujibu wa sheria na taratibu huku akiwataka Watanzania kutokupotosha maelekezo aliyoyataoa aliyekuwa Rais wa awamu ya Tano hayati Dk John Magufuli.

"Kwa nini hamsemi kuwa Hayati (Magufuli) aliitaka Wizara ya Afya kujiridhisha kwanza kabla ya kuruhusu chanjo hizo? Yaani ninyi mnasema tu kwamba alisema chanjo ni mbaya, wakati alisema hivyo na kutoa angalizo kwamba kabla hazijaruhusiwa lazima wataalam wetu wajiridhishe na ubora wake na ndio kazi iliyofanyika kabla ya serikali ya awamu ya sita kuruhusu chanjo kuanza kutolewa," amesema Dk Gwajima.

Amesema kuwa wakati janga la corona linaingia nchini Aprili mwaka jana hakukuwa na namna ambavyo watu wangeweza kujikinga na ugonjwa huo kutokana na ukweli kuwa chanjo hazikuwepo duniani.

"Hivi mbona mnanisema tu mimi? Kwani nilikuwa najifukiza na kutumia dawa za asili mimi mwenyewe? Kwani nyie hamkujifukiza wangapi mlikuwa mkitembea na dawa za bupiji, covidal na nyingine nyingi za asili.

“Mbona ninyi hamjisemi maana sote tulitumia na kutembea nazo kwenye mikoba, mimi wala sijutii maana dawa zile zile zimethibitishwa na maabara ya tiba za asili nchini," amesema.

Ameendelea kusema, baada ya wanasayansi kufanya utafiti na kuja na chanjo hakuna haja ya kubishana nao isipokuwa watu wanatakiwa kuchanjwa ili kuondokana na athari za ugonjwa huo kwa maelekezo kuwa hakuna mtu wa kushindana na sayansi.