Gaddafi aandaa vikosi vya siri akiwa shuleni

Gaddafi aandaa vikosi vya siri akiwa shuleni

Muktasari:

  • Katika toleo lililopita tuliona jinsi kizazi kipya cha wanasiasa wa Libya kilivyoathiriwa na vuguvugu la mageuzi katika ulimwengu wa Waarabu, hususan baada ya mapinduzi yaliyofanywa na Gamal Abdel Nasser nchini Misri kwa kumpindua Mfalme Farouk I Julai 23, 1952 na yale yaliyofanywa na Abdul Karim Kassem wa Iraq kwa kumpindua Mfalme Faisal II wa Iraq katika mapinduzi ya Julai 14, 1958.

Katika toleo lililopita tuliona jinsi kizazi kipya cha wanasiasa wa Libya kilivyoathiriwa na vuguvugu la mageuzi katika ulimwengu wa Waarabu, hususan baada ya mapinduzi yaliyofanywa na Gamal Abdel Nasser nchini Misri kwa kumpindua Mfalme Farouk I Julai 23, 1952 na yale yaliyofanywa na Abdul Karim Kassem wa Iraq kwa kumpindua Mfalme Faisal II wa Iraq katika mapinduzi ya Julai 14, 1958.

Mapinduzi hayo yalileta mwangwi katika ulimwengu wa Kiarabu. Sauti ya Cairo, ambayo ndiyo redio pekee iliyokuwa ikisikika nchini Libya, na ambayo mmoja wa wasikilizaji wake ni Muammar Gaddafi akiwa katika Chuo Kikuu cha Kijeshi cha Beghazi, ilikuwa ikieneza propaganda za Kiarabu za mapinduzi ya Misri na yale ya Iraq kiasi kwamba, Gaddafi na watu wake waliamini wangeweza kufanya kile kilichofanyika Iraq na Misri.

Katika hatua hii, Serikali ya Mfalme Idris wa Libya haikuweza kutuliza wimbi la harakati za utaifa lililokuwa limeanza kusambaa kwa kasi.

Vita vya Siku Sita na Israeli mwaka 1967 vilisababisha mlipuko mwingine wa ghasia za harakati za utaifa katika mitaa ya mjini mbalimbali ya Libya. Juni 5 umati wa raia wa Libya uliochochewa na matangazo ya redio ya Misri ulijaa katika mitaa ya Tripoli. Ghasia hizo zilisababisha mauaji ya Wayahudi kadhaa walioishi Libya na wengine walishambuliwa na kuporwa mali zao na nyingine kuharibiwa.

Waandamanaji wenye hasira pia walishambulia mali za Waingereza na Wamarekani huko Tripoli na Benghazi, kwa kuamini nchi mbili zilishiriki katika vita kwa upande wa Israel.

Marekani ilishtushwa na tukio hilo na ikawahamisha raia wake 6,300 kutoka Libya. Hasira ya raia hao ilichochewa zaidi na kitendo cha Libya kushindwa kuwasaidia Waarabu katika vita yao dhidi ya Israel.

Hatimaye wakati kikosi cha Libya kilipopewa ruhusa ya kwenda kujiunga na vikosi vya Waarabu ambavyo vilikuwa vikipambana na Israel, tayari walikuwa wamechelewa kwa sababu hata kabla ya kikosi hicho kufika kwenye kituo chake cha mapambano, tayari jeshi la Misri lilikuwa limeshazidiwa na vita ikawa imeisha kwa ushindi wa Israel.

Miongoni mwa wale ambao walikuwa wamejiunga na kikosi hiki alikuwa ni Gaddafi, ambaye baadaye alidai alikuwa amerejea Libya kutoka kikosini ili kujiandaa na shambulio dhidi ya nchi zilizoisaidia Israel kushinda vita hiyo.

Kwa wakati huu ilikuwa inazidi kuonekana kama mfalme hawezi kuhimili nguvu ya itikadi ya harakati iliyosambaa kwa kasi. Ni kweli mfalme anayeungwa mkono na mataifa ya Magharibi angejitahidi kukabiliana na itikadi kali kama hizo. Lakini kwa Mfalme Idris kufanya hivyo kulimletea hasara nyingi zaidi.

Kadhalika alivyozidi kuwa mzee na dhaifu ndivyo alivyozidi kuweka madaraka yake mikononi mwa familia ya Al-Shelhi ambayo washauri wengi walikuwa watu wake.

Kwa kuwa Idris alishindwa kumwandaa mrithi wake, wanaharakati walihofu kuwa Al-Shelhis alikuwa akijipanga kuchukua uongozi wa nchi. Kwa Walibya wengi, mfumo mzima ulikuwa ukionekana kuwa umeoza kabisa ndani na nje.

Hiyo haimaanishi kuwa utawala wa Idris haukuwa na mafanikio, la hasha huyu mfalme wa kwanza na wa pekee wa Libya alisimamia mabadiliko makubwa na magumu ambayo yalifanya makabila mengi ya nchi hiyo kuwa kitu kimoja na alijenga hisia za utaifa japo kidogo.

Wakati hisia za utaifa zilipopata nguvu zaidi, ziliibua hata hisia za kuleta mapinduzi kamili. Njia ambayo wanaharakati wengi waliifikiria ni ile ya mapinduzi ya kijeshi.

Serikali zilizokuwa zimewapindua watawala wa kifalme wanaoungwa mkono na nchi za Magharibi katika eneo lote la nchi za Kiarabu kwa sehemu kubwa ziliingia madarakani kupitia mapinduzi ya kijeshi, hii ikiwa njia ya haraka kuchukua nchi. Kama vile Gaddafi mwenyewe alivyokumbuka baadaye: “Jeshi ndilo lilikuwa chombo chenye uwezo wa kulazimisha mapenzi ya wananchi yatimie kwa haraka na kwa nguvu.”

Ukweli ulijulikana pia kwa wafadhili wa Ufalme wa Libya. Mapema mwaka 1967, Wamarekani walionyesha hofu juu ya uwezekano wa uasi nchini Libya. Waliwasihi Walibya kuboresha vyombo vyao vya usalama ili waweze kukabiliana na hali hiyo.

Kufikia wakati wa kiangazi cha mwaka 1969, wakati mfalme Idris akifuatana na mkewe, Malkia Fatima, walipoamua kwenda mapumziko ya muda mrefu, kwanza nchini Ugiriki na kisha Uturuki kwa sababu za kiafya, hali ya hewa ya kisiasa huko Tripoli na Benghazi ilikuwa mbaya huku uvumi juu ya njama za mapinduzi ya Serikali zilikuwa zimeanza kusambaa.

Uvumi kama huo haukuwa na msingi. Kulikuwa na vikundi kadhaa vilivyokuwa vikipanga njama kwa wakati huo. Miongoni mwao kulikuwa na kikundi cha maafisa vijana katika jeshi, wakiongozwa na Gaddafi. Njama yake ilikuwa imeandaliwa kwa muda mrefu ikisubiri wakati muafaka wa kuitekeleza.

Njama hizo zilikuwa zimeanza karibu mwongo mmoja uliokuwa umepita wakati Gaddafi na wanamapinduzi wenzake wakiwa katika shule ya Sekondari ya Sebha huko Fezzan.

Wakiwa wameleweshwa na hamu ya utaifa, wavulana hawa wa shule waliuchukulia utawala wa kifalme wa Libya kuwa kielelezo cha udhaifu na kizuizi kikubwa cha Serikali ya kisasa ya Kiarabu ambayo wao waliitamani sana.

Gaddafi mwenyewe alikaririwa wakati fulani akisema: “Nafsi zetu zilikuwa kwenye uasi dhidi ya wanaofunika na nchi yetu na ardhi yake, nchi ambayo watu wake walikuwa wanaporwa zawadi bora waliyopewa na Mungu na utajiri uliokuwa unaporwa na waporaji, na dhidi ya watu wetu kutengwa na kulazimishwa kutoka kwenye njia ya Waarabu.”

Huu ndio wakati ambao Gaddafi aliamua kufanya mapinduzi yake mwenyewe-mapinduzi ambayo kipenzi chake, Rais Nasser, angeweza kujivunia. Alianza kupanga kikundi kidogo cha wanafunzi wenzake kuanzisha harakati za mapinduzi ya chini kwa chini, na akawagawa katika vikundi vidogo mbalimbali ambavyo mwenyewe (Gaddafi) alivielezea kama mwanzo wa ‘kupanga na kuandaa mapinduzi’.

Hakuweka vigezo vigumu kwa waliotaka kujiunga na harakati hizo za mapinduzi. Badala yake, Gaddafi aliwaita wale waliotaka kufuata siasa za Nasser, ambao walikubali kuunga mkono harakati za utaifa.

Masharti makubwa aliyowapa waliotaka kujiunga na harakati zake ni sharti wasiwe wanakunywa pombe au kufuatana na wanawake kwa maana ya kufanya nao ngono.

Inaonekana kuwa vijana hawa walikuwa na hamu ya mabadiliko ya utawala, lakini hawakuwa na mtu wa kuwaongoza kama Gaddafi.

Mohamed Belqassim Zwai, ambaye alikuwa katika shule ya sekondari ya karibu huko Sebha na ambaye alishikamana na Gaddafi hadi mwisho alipouawa 2011, akielezea alivyokutana na Gaddafi enzi za ujana wao, alisema kikundi kilianza kufanya mikutano ya siri.

Gaddafi mwenyewe aliwahi kusimulia: ‘Tulikuwa tukikutana chini ya mtende karibu na Ngome ya Sebha tukitumia taa tuliyoitengeneza wenyewe kwa mikono. Kwa kutumia mwanga wa taa hiyo nilikuwa nikiwapa somo wenzangu namna ya kufanya mapinduzi.”

Gaddafi aliweka nidhamu kali. Aliwakataza washirika wake kupenda starehe ikiwa ni pamoja na kwenda klabu za usiku, kucheza kamari na maovu mengine. Pia aliwataka wafanye mambo yao kwa utii kamili na usiri mkubwa ili kukamilisha mpango bila siri kuvuja.

Je, nini kiliendelea? Usikose kuendelea na simulizi hii kesho.