Prime
Hekaheka injini ya Airbus ya ATCL ikipata hitilafu angani na abiria 122

Muktasari:
- ATCL imesema tukio hilo limetokea dakika 25 baada ya ndege kuruka.
MAREKEBISHO: Toleo la awali la habari hii lilikuwa na kichwa kilichosema "Hekahela ndege ya ATCL ikiwaka moto ikielekea Mbeya ikiwa angani na abiria 122". Baada ya kufuatilia zaidi, tumefahamishwa kuwa ndege "haikuwaka moto" bali "ilipata hitilafu kwenye moja ya injini" ambayo marubani na wahudumu walifanikiwa kuidhibiti.
Habari hii imerekebishwa kuakisi taarifa hizi mpya.
Mhariri
Dar es Salaam. Abiria 122 wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), wamenusurika kifo wakiwa safarini baada ya ndege waliokuwa wamepanda kupata hitilafu kwenye moja ya injini zake.
Ilikuwa Jumamosi Februari 24, 2024, ndege ya ATCL Airbus A220-300 iliyoruka kutoka Dar es Salaam kwenda Mbeya iliponusurika kushika moto baada ya moja ya injini kupata hitilafu na kuanza kutoa moshi.
ATCL imesema tukio hilo limetokea dakika 25 baada ya ndege kuruka na kwamba, marubani na wahudumu walidhibiti hali hiyo na ndege kurejea na kutua salama jijini Dar es Salaam.
Awali, ndege hiyo ilipaswa kuanza safari saa 10.00 jioni, kabla ya kusogezwa mbele kwa takribani saa mbili kwa kilichoelezwa kuwa ilikuwa ikisubiriwa kutua ikitokea Moroni, nchini Comoro.
Abiria aliyekuwa ndani ya ndege hiyo aliyeomba jina lake lisitajwe, amesema baada ya kuruka umbali wa futi anazokadiria kuwa 12,000 walianza kuhisi harufu ya kitu kinachoungua.
Baadaye amesema moshi ulianza kuingia ndani ya ndege na wahudumu walitoa tangazo la kuwepo kwa tatizo huku wakieleza, marubani wanafanya jitihada kuhakikisha usalama unakuwapo.
Ameeleza wahudumu waliwasaidia abiria kuvaa vifaa maalumu vya kuvutia hewa, wakiwasisitiza kuwa na watulivu.
Hata hivyo, amesema hali ndani ya ndege kulikuwa na taharuki, abiria kila mmoja akiomba na kusali kwa imani yake.
Amesema baada ya muda mfupi, hali ilianza kuwa ya kawaida na harufu ya moshi ndani ya ndege ikapungua.
“Baada ya jitihada kubwa za marubani iliyochukua saa kadhaa angani (nadhani ya kupeleka ndege juu zaidi pasipo na hewa ya oksijeni), moshi ilikwisha ndege ikarejea na kutua salama uwanja wa JNIA saa 3.00 usiku,” amesema alipozungumza na Mwananchi.
Abiria huyo amesema kutokana na hofu ya kifo na taharuki, wengi waliahirisha safari na kurejea majumbani, na wengine kuendelea na safari kwenda Mbeya saa 6.00 usiku huohuo.
Shuhuda mwingine ndani ya ndege hiyo, amesema ratiba ya awali kwa mujibu wa tiketi walizokuwa wamekata ndege ilitakiwa kuanza safari saa 10:45 jioni, lakini walipewa taarifa kuombwa radhi na muda ulisogezwa mbele na kuanza safari saa 11:45 jioni.
Ameongeza kuwa kabla ya kupitia taharuki hiyo, ndege ilianza kupata mtikisiko mkali.
"Ghafla walianza kutangaza, tunapita kwenye hali mbaya ina mawingu mengi na tusiwe na wasiwasi, kweli tulipita ile hali baada ya muda moshi ulianza kuingia ndani ya ndege," amesimulia.
Amesema muda mchache baada ya kupaa, harufu ya kitu kiuunguacho ilianza, watu wakahamaki kuulizana ni jambo gani bila majibu ya moja kwa moja. Baadaye moshi ulianza kuingia ndani.
"Watu walianza kukohoa na moshi ukawa unazidi, ghafla tukaona wafanyakazi wanahangaika kuhakikisha usalama unarejea,” amesema.
Abiria huyo ameeleza wakati watu wanaendelea na taharuki walitangaziwa hali ya hatari wakielezwa rubani anahangaika kupata mawasiliano ili afahamu sehemu ya kwenda kutua kulingana na ukubwa wa ndege.
Amesema kila mmoja alikuwa anasali kwa imani yake na waliokuwa na tatizo la presha ilipanda kutokana na kile kilichokuwa kinaendelea.
Wakiwa bado wanahangaika angani, amesema muda wote taa ya hatari ilikuwa inazima na kuwaka, huku vilio vya abiria na ibada zikiendelea.
"Ghafla tukiwa huko angani tulitangaziwa rubani amepata mawasiliano sehemu salama ya kutua ni Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dar es Salaam hivyo tunarudi," amesema.
"Ile kurudi Dar es Salaam nilikuwa nahisi kama nimepotea angani kwa sababu tulichukua muda mrefu Dar es Salaam. Mpaka tunatua hakuna aliyeamini wengi walighairi safari baada ya kuambiwa tusubiri tuanze tena safari. Baadhi tuliomba mabegi yetu ila wengine waliendelea na safari katika muda mpya uliopangwa," amesimulia na kuongeza: "Tuliomba turudishiwe nauli zetu kwa kile kilichotokea, lakini mambo yakawa tofauti," amesema.
Kauli ya ATCL
Akizungumza na Mwananchi Digital, Ofisa Uhusiano wa ATCL, Sarah Reuben amekiri ndege hiyo aina ya Airbus A220 yenye usajili namba 5H-TCH iliyokuwa ikiruka kutoka Dar es Salaam kwenda Mbeya ilipata hitilafu kwenye injini moja.
Tofauti na inavyoelezwa na abiria, Sarah amesema tatizo hilo lilisababisha moshi ndani ya ndege kwa takriban dakika zisizozidi tano.
Amesema marubani walidhibiti tatizo hilo ikiwa ni pamoja na kuzima injini yenye hitilafu kama mwongozo unavyoelekeza.
“Rubani alirejesha ndege hiyo Uwanja wa Kimataifa wa Julius Nyerere (Dar es Salaam) ikiwa ndiyo kiwanja kilichokuwa karibu chenye uwezo wa ndege ya A220 kutua.
“Wahudumu wa ndege waliendelea kufanya kazi yao kwa weledi mkubwa, ikiwemo kutoa taarifa sahihi kwa abiria kuwa changamoto iliyojitokeza inadhibitika hivyo kuwaondoa hofu,” amesema Sarah.
Hata hivyo, amesema tofauti na inavyoelezwa katika tukio hilo hakuna abiria aliyeonyesha uhitaji wa vifaa saidizi vya upumuaji au kupoteza fahamu.
“Tukio zima lilichukua takriban dakika 60 tangu ndege kupaa angani hadi kurejea Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere. Hata baada ya kurejea Dar es Salaam hakukuwa na abiria yeyote aliyeonyesha changamoto ya kiafya au kuhitaji msaada wowote wa kimatibabu,” ameeleza Sarah.
Kuhusu abiria na safari yao, amesema 104 kati ya 122 waliendelea na safari, 18 wakiomba kubadilisha tarehe za safari, jambo ambalo ATCL ilifanya bila kuwatoza gharama za ziada.