Huyu ndiye Dk Moremi na kibarua kipya Maabara ya Taifa

Muktasari:

  • Wadau wa afya waeleza wanavyomfahamu Dk Nyambura Moremi, wananchi wataka sayansi isiingiliwe na siasa.

Dar es Salaam. Siku moja baada ya Wizara ya Afya kumrejesha kwenye nafasi yake aliyekuwa Mkurugenzi wa Maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii (NPHL), Dk Nyambura Moremi, wadau wa afya wametaja kazi inayomsubiri, huku wananchi wakitaka sayansi isiingiliwe na siasa.

 Mei 4, 2020, Dk Moremi alisimamishwa kazi kupisha uchunguzi na Waziri ya Afya, baada ya Rais wa wakati huo, hayati John Magufuli kutia shaka usahihi wa vipimo vya Mabara ya Taifa vilivyothibitisha kuwapo Uviko-19 katika sampuli za wanyama na mimea.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wadau wa afya wameeleza kile kilichotokea na usahihi wake na kazi iliyo mbele ya mkurugenzi huyo, wakati nchi ikiwa imeanzisha Tume ya Taifa ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi katika mifumo ya Tehama.

Aliyekuwa Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT) mwaka 2020, Dk Elisha Osati amemwelezea Dk Moremi kama mtaalamu aliyebobea katika biolojia na maabara ya masuala ya magonjwa ya maambukizi.

“Namfahamu Nyambura tangu tuko shule, yeye amesoma chuo cha afya Bugando tukafanya mafunzo kwa vitendo Muhimbili, ni mwanamke imara anayetekeleza majukumu yake kwa matokeo chanya katika sekta ya afya,” amesema.

Dk Osati amesema Dk Moremi anastahili katika nafasi hiyo, kwani alikuwa anafanya kazi nzuri na yaliyotokea ilikuwa ni ajali ya kisiasa au kitaaluma.

Amesema katika masomo yake ya Shahada ya Uzamili na Shahada ya Uzamivu amebobea katika eneo hilo, hivyo ni nafasi inayomtosha.

Dk Osati ambaye ni miongoni mwa wataalamu waliotoa elimu ya kujikinga na Uviko-19, amesema kilichotokea wakati huo kilitokana na nchi kuhamaki.

“Dunia nzima ilipaniki kama Tanzania katika kupambana na ugonjwa wa Uviko-19, yeye kuondolewa katika ile nafasi ilikuwa sehemu ya nchi kupaniki. Nadhani kurudi kwake ni jambo zuri tunamuombea aendelee kusikilizana na wenzake waliokuwepo na kushirikiana na wanataaluma wengine,” amesema.

Amesema Dk Moremi ana kazi kubwa ya kuendeleza taaluma na kusaidia wananchi, kwani yupo katika kitengo muhimu kinachosaidia kugundua magonjwa ambayo nchi inapambana nayo.

Dk Osati amesema kiongozi huyo ana wajibu wa kushirikiana na wenzake na kuhakikisha wanajenga timu nzuri, pia kutengeneza ushirikiano kimataifa wenye manufaa kwa Taifa.

“Kwa sasa ukiangalia tunayo Tume ya Taifa ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi katika Mifumo ya Tehama, maana yake sasa utafiti tutakaofanya itabidi usajiliwe huko, sasa yeye nadhani atakuwa kwenye nafasi nzuri ya kuangalia sampuli tunazozichukua kwa ajili ya kuzichakata zinapita kwenye Maabara ya Taifa,” amesema na kuongeza:

“Yupo katika nafasi nzuri kwa hiyo tume kuhakikisha wakati wote wanasayansi wanapata mazingira mazuri ya kufanya utafiti bila kuingiliwa, lakini kulinda nchi kuhakikisha utafiti hauendi kokote kule, ubaki kwa ajili ya Tanzania bila kutumika na watu wengine nje ya nchi.”

Maoni ya wananchi

Kupitia ukurasa wa mtandao wa kijamii wa Instagram (mwananchi-official) wananchi wameeleza namna utafiti wa maabara hiyo ulivyotiliwa shaka, wakitoa angalizo kwa wenye mamlaka kutowahukumu wanasayansi kupitia matokeo ya utafiti wa kitaaluma.

Kadoda Stan amesema ni vema walio karibu na uongozi wakawashauri viongozi, ili kutoharibu taaluma, hasa ya afya ambayo ndiyo inaamua uhai wa Watanzania.

Wengi wamepongeza uteuzi wa Dk Moremi wakitaka utendaji kazi uliotukuka kutoka kwake, ili kulisaidia Taifa.

“Doa hili la kiutawala halitasahaulika kwenye historia ya nchi hii. Unapeleka sampuli ya papai na damu ya mbuzi? Sampuli ina kanuni zake jamani, Serikali iliteleza,” amesema mwananchi anayejitambulisha Doni802000.

Sayansi kuingiliwa na siasa

Miongoni mwa wataalamu wameeleza namna ambavyo Serikali imekuwa ikitia mkono katika masuala ya kisayansi, wakishauri taaluma zipewe nafasi katika kutekeleza yale wanayotakiwa kwa manufaa ya nchi.

“Ningekuwa madarakani Dk Mwele Malecela asingefukuzwa kazi wakati ule, ningeenda kwa Mheshimiwa Rais na kumpa ushauri, Zika ilikuwepo tangu mwaka 1953 leo mtu anasema kuna Zika unamuondoa jukumu la wanasayansi liko wapi?” Amehoji mtaalamu wa Afya ya Jamii, Dk Ali Mzige aliyewahi kuwa Mkurugenzi wa Kinga Wizara ya Afya kabla hajastaafu mwaka 2005.

Dk Mzige amesema vipimo vya Uviko-19 vilitengenezwa kupima sampuli za binadamu, kisayansi unapopeleka kupima kitu kingine waweza kupata majibu yoyote.

“Dk Moremi hakukosea shida ni kwamba tunaingiza siasa kwenye sayansi,” amesema.

Akizungumzia hilo, Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Deus Ndilanha amesema mamlaka inateua na kutengua, hivyo haipaswi kuhojiwa, kwani wana nyenzo ya kupata taarifa na kufanya maamuzi.

“Kama mamlaka inaamua kukuweka pembeni kwa ajili ya uchunguzi kwa taarifa ambazo walikuwa nazo, moja kwa moja wakija kupata taarifa sahihi na wakajiridhisha kwa kuthibitisha walipewa taarifa zisizo kweli, ukafuatiliwa ulionekana unasaidia taasisi moja kwa moja wanakurudisha,” amesema.

Dk Ndilanha amesema si mara ya kwanza kwa watu kuteuliwa, kutolewa na kurudishwa, hivyo ni ndani ya mamlaka ya anayeteua na kutengua.

Rais wa Chama cha Wafamasia Tanzania (PST), Fadhili Hezekiah amesema wakati inasemwa mambo ya mapapai kukutwa na Uviko-19 hapakuwa na ushahidi kwamba kuna mambo ya kisiasa yameingia kwenye taaluma.

Hezekiah amefafanua kuwa kila eneo lina nafasi yake katika kuhakikisha nchi inaenda vizuri iwe katika siasa au taaluma, eneo moja likitumika vibaya dhidi ya lingine lazima changamoto zitokee.

“Tunaona mifano mingi duniani wanasayansi wanaweza wakatengeneza genge au majibu yasiyofaa wakawadanganya mamlaka, pande zote zinaweza kuvutia kwenye masilahi, lakini ninachokisema hapa kila mmoja achukue nafasi yake kwa kuheshimu mipaka na kwa uaminifu kutekeleza majukumu yaliyo ndani ya uwezo wao,” amesema.

“Kuteua au kutengua kwa uwezo wa mtu pia kuna vitu vinavyoendana na usalama wa Taifa letu, kwa hiyo kiongozi na mwenye nafasi, taasisi kubwa za kiuchunguzi, kitabibu, mamlaka pengine kabla hajasema jambo ajiridhishe na wenzake, viongozi na mamlaka ya uteuzi kwamba hili jambo lipo kama lilivyo tukiliweka linaweza kuleta changamoto ipi kwenye jamii,” amesema.

Hezekiah amesema kuna mambo yana uhalisia, lakini yakienda kwenye jamii yanaleta taharuki, kuliko kuleta utulivu, hivyo amesisitiza kujiridhisha ni muhimu.

Amesisitiza kila taasisi ina umuhimu wake, ni vema ikapewa nafasi ndani ya wigo wake bila kuingiliwa na wao wajue wana wajibu katika mifumo ya kiserikali.


Wasifu wa Dk Moremi

Dk Nyambura Moremi, Mkurugenzi wa Maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii alisimamishwa kazi akiwa na umri wa miaka 35.

Alipata shahada ya kwanza katika Chuo cha Kikatoliki cha Afya na Sayansi Shirikishi (CUHAS) Bugando.

Alipata Shahada ya Uzamivu (PhD) katika Chuo Kikuu cha Julius Maximilian Würzburg, nchini Ujerumani kupitia andiko lake 'The upsurge of Antimicrobial Resistance in Tanzania.'

Ni miongoni mwa wabobezi katika fani ya maabara na ni mtaalamu wa magonjwa ya kuambukiza.