Idadi miamala ya simu yapungua

Muktasari:

  • Imeelezwa kuwa tangu kuanzishwa kwa tozo ya miamala ya simu Julai 15 mwaka huu, idadi ya miamala imepungua.

Dar es Salaam. Imeelezwa kuwa tangu kuanzishwa kwa tozo ya miamala ya simu Julai 15 mwaka huu, idadi ya miamala imepungua.

Juzi, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ilieleza gazeti hili kuwa, miamala hiyo milioni 9.9 ni wastani wa miamala kwa siku moja, hivyo kwa siku 28 miamala iliyofanyika ni zaidi ya milioni 277.2.

Mkurugenzi wa Mtendaji wa TCRA, Jabir Bakari alisema upungufu huo ni mdogo kama alivyoeleza Waziri Mwigulu ikilinganishwa na takwimu za kipindi cha nyuma.

Juzi, katika mkutano wake na waandishi wa habari, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba alisema Watanzania wameendelea kutumia huduma za miamala kama kawaida na kwa kipindi cha wiki nne tangu kuanzishwa kwa tozo hizo huku Serikali ikikusanya Sh48.48 bilioni.

“Katika wiki nne za mwanzo jumla ya miamala milioni 9.9 ilifanyika, haina tofauti sana na siku za nyuma ilipokuwa milioni 10 na milioni 11, tofauti sio kubwa,” alisema Dk Mwigulu, bila kueleza mlinganisho wa thamani ya miamala katika kipindi hicho na kilichopita.

“Kama idadi ya miamala iliyofanyika haina tofauti ina plus (ongezeko) na minus (pungufu) kidogo tu ikilinganishwa na mwenendo wa siku za nyuma, hivyo hata thamani ya miamala nayo huenda ni ileile,” alisema Dk Nchemba.

Kwa mujibu wa takwimu za mawasiliano za robo mwaka za TCRA, Julai 2020 jumla ya miamala ni milioni 288.35 yenye thamani ya Sh11.3 trilioni.

Kwa Agosti jumla ya miamala iliyofanyika ilikuwa 288.56 yenye thamani ya Sh11.07 trilioni na Septemba miamala ilikuwa 299.25 ya Sh11.55 trilioni.

Hata hivyo, katika takwimu hizo za TCRA ambazo hutolewa kila baada ya miezi mitatu, hivi karibuni zimekuwa hazichapishi idadi ya miamala iliyofanyika kwa kipindi husika, lakini kwa kuangaliwa rekodi za mwaka uliopita matumizi ya huduma za miamala yalikuwa makubwa kuliko sasa.

Takwimu za mawasiliano zilizotolewa hivi karibuni na TCRA mpaka Juni, 2021 watumiaji wa huduma za simu nchini walikuwa 53,182,651, wakiwa na akaunti za miamala ya simu 33,282,544.

Kuhusu hatima ya tozo hizo, juzi Nchemba alisema suala la mapitio ya tozo za simu kama ilivyoagizwa na Rais Samia Suluhu ndani ya kipindi kifupi, taarifa itatolewa kwa kuwa kuna kipengele kimoja kilitakiwa kufanyiwa kazi zaidi na tayari imekamilika ipo kwa Waziri Mkuu.

Tayari kituo cha sheria na haki za binadamu kimefungua kesi kupinga tozo hizo, lakini Julai 27, 2021 Rais Samia Suluhu akizungumza kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwa tozo hizo alisema suala la tozo za miamala ya simu lipo palepale.

Pia, alisema Serikali inakwenda kuangalia njia ya kulitekeleza.

“Makato haya tuliyaweka kwa nia njema tu, nchi yetu sasa hivi wakulima wameamka na kilimo kikubwa, lakini wakivuna wanashindwa kutoa mazao yaliko kuleta kwenye maeneo ya masoko, tatizo ni njia za vijijini hakuna, kwa hiyo sehemu kubwa ya fedha hizo inakwenda kujenga njia za vijijini,” alisema Rais Samia.

Pia, katika mwaka huu wa bajeti, Serikali ilianzisha tozo katika miamala ya simu ya Sh10 hadi Sh10,000 ikilenga kukusanya Sh1.25 trilioni, kiasi ambacho ili kifikiwe kwa kila mwezi, chanzo hicho cha mapato kinapaswa kuzalisha wastani wa Sh104.16 bilioni.