Kichwa cha mlinzi wa shule aliyeuawa Arusha chapatikana

Muktasari:
Kichwa cha mlinzi wa shule ya Winnings Spirit, Issa Dinaiah (57) aliyeuawa kwa kuchinjwa kimepatikana baada ya msako wa Jeshi la polisi.
Arusha. Kichwa cha mlinzi wa shule ya Winnings Spirit, Issa Dinaiah (57) aliyeuawa kwa kuchinjwa kimepatikana baada ya msako wa Jeshi la polisi.
Mlinzi huyo wa shule hiyo inayomilikiwa na Meya wa Jiji la Arusha, Maximilian Iranghe aliuawa juzi Jumatano na watu wasiojulikana na kuondoka na kichwa hicho.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Justine Masejo amesema leo Februari 3, 2022 kuwa kichwa hicho kimepatikana baada ya kukamatwa mtuhumiwa mmoja ambaye pia alikuwa mlinzi wa shule hiyo.
"Ni kweli tumepata kichwa cha marehemu na uchunguzi bado unaendelea" anasema Kamanda Masejo
Msemaji wa familia ya marehemu, Bakari Kassim amesema familia imepata taarifa ya kupatikana kichwa cha ndugu yao.
"Tumepata taarifa Polisi kuwa kichwa kimepatikana na anayetuhumiwa ni mlinzi mwenzake kijana mwenye umri wa miaka kama 18 hivi" amesema
Amesema mazishi ya marehemu huyo yanafanyika leo katika makaburi ya Ngaramtoni wilaya ya Arumeru baada ya kukabidhiwa mwili.
Juzi akizungumza na waandishi wa habari, Meya Iranghe alisema alipata taarifa za kifo cha mfanyakazi huyo baada ya kupigiwa simu na alipofika shuleni iliyopo eneo la Muriet alikuta mwili na Polisi wakiwa katika uchunguzi.