Majaliwa aongeza siku saba uchunguzi moto Soko la Kariakoo

Janga la moto Kariakoo lafichua mambo mazito

Muktasari:

  • Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka wafanyabiashara wa Soko Kuu la Kariakoo, kuendelea kuwa na subira na wasifanye biashara kwenye eneo hilo mpaka serikali itakapotoa maelekezo.

Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameongeza siku saba kwa Tume aliyoiunda kuchunguza kuungua kwa soko la Kariakoo hadi Julai 25, mwaka huu.

Majaliwa aliunda tume hiyo Julai 11, 2021 alipofika katika soko hilo kujionea uharibifu iliofanyika na kuipa siku saba kukamilisha uchunguzi wake kuhusu chanzo cha moto huo ambao, umeteketeza sehemu kubwa ya soko hilo pamoja na mali za wafanyabiashara.

Tume hiyo itahusisha wajumbe kutoka Ofisi ya Rais, Waziri Mkuu, Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania, Jeshi la Polisi, Kitengo cha Maafa, Tamisemi, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (DPP) pamoja na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).

Akizungumza leo Jumatano Julai 21, 2021 wakati wa ibada ya Sikukuu ya Eid Al Adha iliyofanyika katika Msikiti wa Mtoro jijini Dar es Salaam, Majaliwa amesema kuwa tume hiyo ilimuomba iongezewe muda ili kuchunguza zaidi.

“Mtakumbuka niliunda tume nikaipa siku saba ikamilishe kazi hiyo. Nikiwa kule Morocco waliniomba ridhaa niwaongezee muda waingie kwenye shughuli za uhandisi wa kulipima jengo lenyewe kama bado zima au ule moto uliowaka siku nzima umeshaiunguza ile saruji na likawa sio salama.

“Kwa hiyo nikaridhia kuwaongezea siku saba nyingine mpaka tarehe 25 mwezi huu wakamilishe uchunguzi wao na taarifa ikikamilika tutaitoa hadharani, lakini pia serikali itatoa mwelekeo wa soko letu,” amesema Majaliwa.

Hata hivyo, amewataka wafanyabiashara kuendelea kuwa na subira na wasifanye biashara eneo hilo mpaka serikali itakapotoa maelekezo.

“Kwa wale ambao wanafanya biashara, tumeshasema eneo lile lisifanyike biashara iache tume ipite, na kama utaitwa kutoa maelezo kwa maana mtakuwa mnaitwa mmojammoja. Ila tunaomba muacha eneo liendelee kubaki wazi na wakishamaliza serikali itatoa maelekezo juu ya hilo,” amesema.