Matukio kama ya Hamza hayatolewi kauli haraka

Matukio kama ya Hamza hayatolewi kauli haraka

Muktasari:

  • Tukio la Hamza sio la kawaida. Linahitaji ushahidi usio wa kawaida ili kueleza ni kipi ambacho kilimsukuma kufanya mashambulizi yale kwa askari polisi.

Nadharia ya Sagan Standard, inaeleza kuwa “extraordinary claims require extraordinary evidence” – “Tuhuma zisizo za kawaida huhitaji ushahidi usio wa kawaida.”

Sagan Standard ni nadharia iliyotokana na mwanasayansi Carl Sagan, ambaye aliandika kwenye tamthiliya ya Cosmos, kuwa madai au tuhuma zozote zisizo za kawaida, huhitaji ushahidi ambao unakuwa si wa kawaida. Nadharia hiyo kwa kifupi huitwa ECREE.

Nadharia hiyo iwe muongozo kwenye kila tukio, kama si la kawaida, inahitaji utulivu kuliko kuwahi kutoa tamko. Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Simon Sirro, aliwahi kutoa tamko kuhusu Hamza Mohammed, kijana aliyeishangaza dunia kwa kuwafyatulia risasi polisi bila sababu kueleweka.

Tukio la Hamza sio la kawaida. Linahitaji ushahidi usio wa kawaida ili kueleza ni kipi ambacho kilimsukuma kufanya mashambulizi yale kwa askari polisi.

Usikimbilie kusema Hamza alipatwa na matatizo ya akili, kuna watakaohoji mbona hakufyatulia raia wengine, akawa anawalenga polisi tu? Au ‘wendawazimu’ wake ulimwelekeza kwa polisi peke yake? Tujiulize pia, umahiri ule wa kucheza na bunduki aina ya SMG, Hamza aliupata wapi?

Julai 5, mwaka huu, ofisa wa polisi, Sajenti Joseph Ologe, mkazi wa nyumba za polisi za Kasarani, aliripoti Kituo cha Polisi Nakuru, kwamba alipokuwa njiani kwenda kazini, aliliona gari Toyota Corolla, lenye namba za usajili KBV 735U, likiwa limepaki pembeni ya barabara.

Vioo vya gari hilo vilikuwa vimevunjwa. Ajabu, gari hilo lilikuwa bado injini yake inaunguruma. Sajenti Ologe alieleza kuwa alilitambua gari hilo kuwa ni mali ya askari polisi mwenzake, Konstebo John Ogweno. Ologe akabainisha kwamba alipochungulia ndani ya gari kupitia dirisha lililovunjika, alimuona Konstebo Ogweno, akiwa maiti tayari.

Ripoti ya uchunguzi kwenye eneo la tukio, ilikuwa na majibu haya; Konstebo Ogweno aliuawa kwa kupigwa risasi ya milimita tisa, pembeni ya gari kulikutwa jiwe pamoja na chuma, ambavyo vilibeba tafsiri kuwa ndivyo vilitumika kubomoa vioo vya gari lake. Konstebo hakuwa na bastola yake, ingawa mfuko wa kuhifadhia (holster) alikuwa nao. Hiyo ilijenga picha kwamba aliyemuua ndiye aliondoka na bastola yake.

Uchunguzi wa awali ukabaini kuwa bastola iliyotumika kumuua Konstebo Ogweno ni Ceska yenye namba 94676. Uchunguzi huo ambao ulifanywa na maofisa wa kitengo cha upelelezi wa makosa ya jinai, Kaunti ya Mashariki, Nakuru, ulikuta simu ya mkononi. Walipoichunguza, walikuta ni mali ya Koplo Caroline Kangogo.

Wapelelezi walipokwenda nyumbani kwa Caroline, hawakumkuta. Walipopekua ndani, hawakukuta silaha yoyote, ila baadhi ya nguo za Ogweno zilikuwepo nyumbani kwa Caroline. Hiyo ikaleta tafsiri kuwa Konstebo Ogweno alikuwa na kawaida ya kulala nyumbani kwa Caroline.

Julai 6, mwaka huu, mmiliki wa Hoteli ya Dedamax Kimbo, Peter Kiumi Mugeshi, alipiga simu Kituo cha Polisi Mugera, nje ya Jiji la Nakuru, ndani ya Kaunti ya Nakuru. Mugeshi aliripoti polisi kuwa kuna mtu alikutwa chumbani, hotelini kwake, akiwa amekufa.

Mtu huyo aliyekutwa amekufa chumbani, hotelini Dedamax, ni mwanamume, mfanyabiashara. Jina lake ni Peter Njiru Ndwiga, umri ni miaka 32. Taarifa zikaonesha kuwa Ndwiga, alichukua chumba namba 107, saa 10:22 alasiri, Jumatatu (Julai 5). Alipokaguliwa, mfukoni alikutwa na risiti ya Shilingi za Kenya 3,020, sawa na Sh65,000 za Tanzania.

Risiti hiyo ilitolewa na Hoteli ya Jogoo Kimakia Country, iliyopo Thika, Kaunti ya Kiambu. Uchunguzi zaidi ulibaini kuwa risiti hiyo mfukoni mwa Ndwiga, ilitolewa kwa malipo ya kibenki. Kadi ya benki iliyotumika kulipa ni ya Koplo Caroline. Risiti ni ya Julai 5, saa 9:29 alasiri.

Julai 16, mwaka huu, ilikuwa Ijumaa, asubuhi, mwili wa Koplo Caroline, ulikutwa bafuni, nyumbani kwao, Iten, kaunti ya Elgeyo Marakwet, ukiwa na jeraha la risasi. Kisha, ukapelekwa Hospitali ya Iten na kuhifadhiwa kwenye chumba cha maiti, mochwari.

Wengi waliamini Caroline alijiua baada ya kuwaua Konstebo Ogweno na Ndwiga. Je, kama aliuawa na kupelekwa kuhifadhiwa kwenye bafu la nyumbani ya familia yao? Inaaminika ndiye aliwaua Ogweno na Ndwiga, vipi kama muuaji ni mwingine, ila yeye aliingizwa kimazingira?

Sababu ya mauaji ni nini? Caroline ni askari polisi, anajua kila kitu kuhusu ushahidi. Ni kwa nini aliacha alama zake kwenye kila tukio?