Polisi waanza msako kung’oa namba za 3D kwenye magari

Askari wa kikosi cha usalama barabarani akibandua namba za magari zenye mfumo wa 3D kwa mmiliki aliyekaidi kuzibadilisha baada ya kupewa wiki mbili.

Muktasari:

  • Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, limeanza kuwachukulia hatua watu waliokaidi kuondoa vibao vya namba za usajili wa magari aina ya 3D kwa hiari baada ya muda uliokuwa umetolewa kumalizika.

Dar es Salaam. Baada ya wamiliki wa magari kupewa wiki mbili ya kuondoa kwa hiari namba za uzajili wa magari zilizoongezwa ukubwa maarufu kwa jina la 3D, Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama barabarani, limeanza kuwachulia hatua waliokaidi agizo hilo.

 Jana, Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Kamanda Ramadhani Nga’nzi alisisitiza kuwa muda wa wiki mbili uliotolewa kwa watu kuondoa 3D kwa hiari umemalizika, hivyo kuanzia leo Ijumaa Machi 15, 2024 wataanza msako utakaohusisha watengenezaji na wanaoendelea kukaidi kwa kuziweka. Pia watawaandikia faini ya Sh30,000 ya papo kwa hapo.

Kamanda Nga’nzi amesema miongoni mwa hatua watakazozichukua ni kupiga faini, kuwasaka, kuwakamata na kuwafikisha mahakamani watakaobainika kuendelea kuzitengeneza na kuzitumia.

Sababu zinazotolewa na polisi za kutotakiwa kwa namba hizo ni kutoidhinishwa na msajili wa magari kupitia mawakala na hazina ubora unaotakiwa, kwani zilizoiodhibishwa ni za 2D.

Mbali na polisi, Machi 4, 2024, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Jumanne Sagini alisema namba za 3D hazitengenezwi na wakala aliyepata kibali kutoka Shirika la Viwango Tanzania (TBS), huku akibainisha kuwa ukubwa wa herufi hizo unaleta ugumu wa kusomeka katika umbali usiopungua mita 100.

Leo Machi 15, 2024 Mwananchi Digital limeshuhudia polisi wakiwakamata wamiliki wa magari ambayo bado yana namba hizo na kuwaandikia faini pamoja na kubandua namba hizo.

Hata hivyo, baadhi ya madereva wamelalamika muda uliotolewa ni mchache, hivyo wangetakiwa kuongezewa angalau mwezi mmoja mbele.

 "Nilikuwa nimesafiri nimerufi jana, leo ndio natoka lakini hata ukiwaekeza askari, hawalewi," amesema mmoja wa dereva ambaye hakutaka kutaja jina lake.

Fadhil Mohamed, dereva wa teksi mtandao amelalamika kuandikiwa faini, wakati amepewa gari na tajiri yake ikiwa na namba hizo.

Amesema bado kuliwa na nafasi ya kuwaongezea muda angalau miezi miwili au mitatu, halikupaswa kuwa jambo la haraka hivyo kwani linawaumiza wananchi.

"Huku ni kuumizana, unapewa gari yenye namba hizo halafu unakamatwa na kuandikiwa hii sio sawa, tulipaswa kuongezewa muda hata wa mwezi mmoja au miwili," amesema Mohamed.