Rais Samia akataa ombi la kuipandisha hadhi Mbalizi

Muktasari:

Rais Samia amesema wananchi wanataka vituo vya afya, maji. Wakianza kukata halmashauri, na Tanzania nzima inataka kukatwa maeneo, hawataweza, uchumi wa Tanzania bado haujaruhusu. Ameahidi kutekeleza hilo endapo watamaliza shida za wananchi.

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema Serikali yake haina mpango wa kukata maeneo kwa kuyapandisha hadhi, badala yake wanajielekeza kwenye utatuzi wa shida za wananchi hapa nchini.

Rais Samia ametoa msimamo huo leo Ijumaa Agosti 5, 2022 akiwa Mbalizi mkoani Mbeya baada ya kupokea ombi kutoka kwa mbunge wa Mbeya Vijijini, Oran Njeza la kutaka Mbalizi kupandishwa hadhi na kuwa halmashauri ya mji.

Mbunge huyo alimwomba Rais Samia kuupandisha hadhi mji wa Mbalizi ili uwe halmashauri ya mji akidai kwamba itasaidia kusogeza huduma za kijamii kwa wananchi wa Mbalizi na maeneo mengine ya jirani.

Akizungumzia jambo hilo, Rais Samia amesema alipokea ombi hilo kutoka kwa viongozi, hata hivyo amewaeleza wananchi wa Mbalizi kwamba Serikali yake imejielekeza kwenye utatuzi wa shida za wananchi.

“Nilipofika uwanja wa ndege, mkuu wa mkoa na mbunge waliniambia kuhusu halmashauri nikawaambia, halmashauri maana yake ni gharama zaidi, viongozi zaidi, mishahara zaidi, magari zaidi, gharama kwa Serikali, majengo zaidi, gharama kwa serikali.”

“Kwa sasa hivi, wananchi wangu wa Tanzania wana shida chungu nzima, wanataka umeme, wanataka madarasa. Mwaka jana tulijenga madarasa 15,000 sekondari na mengi katika shule za msingi.

“Lakini watoto wetu wanafanya mitihani karibuni hapa…mwakani natakiwa niwe na madarasa 8,000 Tanzania nzima. Yatabebwa na serikali ili msichangishwe, msibughudhiwe, serikali itafute hiyo pesa ikajenge madarasa,” amesema Rais Samia.

Kiongozi huyo amebainisha kwamba bado wananchi wanakabiliwa na changamoto nyingi kama vile vituo vya afya, madarasa, maji, umeme na barabara, hivyo kwa uwezo wa Serikali yake, haitawezekana kufanya yote kwa wakati mmoja.

“Wananchi mnataka vituo vya afya, mnataka maji. Tukisema tunakatana halmashauri, na Tanzania nzima inataka kukatwa maeneo, hatutaweza, uchumi wetu bado haujaruhusu. Acha tumalize shida za wananchi, tukishamaliza tutakwenda kukatana kwenye maeneo.

“Kwa sasa hivi kipaumbele nilichoagizwa na Chama cha Mapinduzi ni shida za wananchi, kwa hiyo hilo la halmashauri litabaki hivyo,” amesema Rais Samia wakati akizungumza na wananchi wa Mbalizi.