Rais Samia aridhia nyongeza ya mishahara kwa asilimia 23.3

Muktasari:

  • Taarifa ya Ikulu imesema Serikali itatumia Sh9.7 trilioni katika mwaka wa fedha 2022/23 kwa ajili ya mishahara, ambapo kati yake Sh1.59 trilioni sawa na asilimia 19.51 ni ongezeko katika bajeti hiyo.

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan ameridhia mapendekezo ya kuongeza mishahara ikiwemo kima cha chini kwa watumishi wa umma kwa asilimia 23.3, ambapo Sh1.59 trilioni itatumika kwa ongezeko hilo.

Taarifa iliyotolewa leo Mei 14 na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Zuhura Yunus inasema mapendekezo hayo ni mwendelezo wa kikao cha Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alichokifanya hivi karibuni mkoani Dodoma na kupokea taarifa kutoka kwa wataalamu kuhusu ongezeko la mishahara.

Taarifa hiyo imesema Serikali imepanga kutumia kiasi cha Sh9.7 trilioni katika mwaka wa fedha 2022/23 kwa ajili ya kugharamia malipo ya mishara ya watumishi wote katika Serikali Kuu, Serikali za Mitaa, Taasisi na Wakala za Serikali.

“Bajeti ya mishahara ya mwaka 2022/23 inaongezeko la Sh1.59 trilioni sawa na asilimia 19.51 ikilinganishwa na bajeti ya mwaka wa fedha wa 2021/22,” imesema taarifa hiyo.