Sheikh Mjaila: Kukosa imani chanzo cha kuongezeka matukio ya mauaji

Wednesday July 21 2021
iddi tanga

Wanafunzi wa shule ya sekondari Handeni wakiwa wamebeba sadaka ya nyama waliopewa kutoka msikiti mkuu wa Ijumaa wilayani humo jana katika kuadhimisha sikukuu ya Eid Al Adha.Picha na Rajabu Athumani

By Rajabu Athumani

Handeni. Imeelezwa kuwa kitendo cha wananchi kuacha kufanya ibada na kufuata miongozo ya dini, ndio chanzo cha kutokea matukio mbalimbali ya mauaji, kwani waumini wamekosa hofu kwenye mioyo yao na wala hawamuogopi Mungu.

Hayo yamesemwa na imamu wa msikiti mkuu wa Ijumaa wilayani Handeni mkoani Tanga, Alhaj Sheikh Ali Mjaila, kwenye ibada ya swala ya Eid Al Adha mjini hapa leo Julai 21 na kusema kuwa, kila mmoja amrudie Mungu na kufahamu kuwa kufanya hayo ni makosa kutokana ma maandiko ya dini zote.

SOMA: Majaliwa awataka Watanzania kuchukua tahadhari ya corona, kupiga nyungu

Amesema licha ya matukio ya watu kuuawa maeneo mbalimbali nchini kwa kupigana risasi, kunyongana na hata mapigano ya wakulima na wafugaji ni ukosefu wa imani kwenye mioyo yao na kutokuwa na hofu ya kumuogopa Mungu, hivyo watu wajitahidi kumrudia Mungu ili kurejesha amani za familia zao.

SOMA:Sheikh wa Mkoa wa Dodoma ataka watu wasife kizembe

"Tunasikia kwenye vyombo vya habari kila kukicha mara huko wameuana, amepigwa risasi, amechomwa moto, amenyongwa, haya matukio zamani ni nadra kuyasikia, hii inasababishwa hatuna hofu ya Mungu kwenye mioyo yetu na tumekosa imani, tumrudie Mungu, tupendane na tujenge hofu hili litarejesha  amani kwenye nyumba zenu," amesema Alhaj Mjaila.

Advertisement

Kuhusu kuwepo ugonjwa wa corona Sheikh Mjaila amesema watu wanakumbushwa kuhusu usafi wa mazingira na miili yao, kila mmoja ajiulize ni kwa nini anasisitizwa anawe mikono na sabuni, kwa sababu wananchi wanajisahau kuhusu usafi wao.

SOMA: Sheikh Mkoa wa Mbeya ataka viongozi wa dini kuliombea Taifa

"Ina maana kama utaepuka mikusanyiko isiyo ya lazima, utanawa mikono yako kwa maji safi na sabuni tayari umefuata kanuni za afya za usafi wako binafsi pamoja na mazingira hivyo kuepuka huu ugonjwa, haya ni makumbusho kwamba tunatakiwa kuwa wasafi muda wote.

Muumini Halfa Kaduka amesema Serikali na viongozi wa dini waongeze msisitizo wa kihakikisha sheria za usafi zinafuatwa ili kuweza kuepukana na ugonjwa wa corona.

Advertisement